Mchungaji+peter+msigwa+(5)Wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge ikitarajiwa kumwita kwa mara ya tatu Waziri wa Maliasili na Utalii kujadili mipango ya bajeti yake, ‘swahiba’ wake, Mchungaji Peter Msigwa, amemgeuka.
  Mchungaji Msigwa, Waziri wa Kivuli wa wizara hiyo, ameshtushwa na hasara ya Sh bilioni 90 aliyoisababisha Nyalandu.


 Kutokana na hali hiyo, Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira anayoiongoza James Lembeli, ilimwita Nyalandu mara mbili wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na kutoridhishwa na majibu yake.
  Hasara ya fedha hizo inatokana na Serikali kutokusanya tozo ya kitanda ambayo ni wastani wa dola 10 (Sh 20,000) kwa siku kwa kila mtalii katika hoteli za kitalii nchini, na kwamba ‘huruma’ ya Nyalandu kwa wawekezaji inatia shaka na kuzua maswali mengi yasiyo na majibu.
  Akizungumza na JAMHURI jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mchungaji Msigwa amesema Waziri Nyalandu anafanya uzembe kwa kutokutekeleza maagizo ya Mahakama.


  Septemba 2014, Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, iliamuru wamiliki wote wa hoteli za kitalii kulipa tozo ya kitanda baada ya kuwa wameishitaki Serikali kortini wakashindwa.
  Licha ya wamiliki hao kushindwa, Nyalandu ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii, ameshindwa kutekeleza agizo la Mahakama na Bunge, hivyo kukiuka malengo ya Serikali ya kukusanya kodi huku maliasili zilizopo zikigeuka mapambo kwa nchi.
 “Lengo la Serikali ni kukusanya kodi, lakini Waziri wa Malisili na Utalii badala ya kukusanya kodi anatupa maswali siyo majibu,” anasema Mchungaji Msigwa na kuonesha mshangao.


  Mchungaji Msigwa ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), anasema kitendo cha waziri kutokusanya hizo fedha kinatia ukakasi hasa takwimu zikionesha kwamba maliasili zilizopo zingekuwa zinainufaisha Serikali.
  Anasema Tanapa walitaka fedha hizo zisaidie kutengeneza barabara, lakini hawajafanikiwa huku miundombinu ikizidi kuwa mibovu.
 Alipoulizwa ukaribu wake na Nyalandu na kuwa amewahi kumtetea kuwa mtendaji mzuri, Mchungaji Msigwa akajibu kwa haraka: “Kamwe sijawahi kumtetea Nyalandu na wala sijawahi kusema kuwa Nyalandu  ni mtendaji mzuri.”
  Ila akaongeza akisema katika suala la kupambana na ujangili nchini, wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na itakuwa hivyo daima.


  Hata hivyo, anasema kuwa  suala ambalo hakubaliani nalo ni Waziri Nyalandu kutokuwa na msimamo wa kusimamia maliasili za nchi.
“Double entry’ inakosesha Taifa mapato makubwa yanayotokana na kuingia kwa watalii katika hoteli za kitalii zilizopo mbugani.
  “Kwanini waingie mara mbili bila kutozwa [mara mbili]? Nyalandu anapingana na Kamati ya Kudumu ya Bunge Ardhi, Maliasili na Utalii ambayo inasimamia kuwapo kwa mfumo wa ‘single entry’ ambayo kila mtalii [anapotoka kwenye mbuga akirejea] atatakiwa kulipia mara aingiapo mbugani bila kujali kama alikwishaingia hapo awali,” anasema.


  “Ukiingia mara moja lazima ulipe, na iwapo utaingia tena utatakiwa kulipia maana haiwezekani kuingia mara mbili kwa fedha ile ile, ni lazima tuwe na utaratibu wa ‘single entry’ yenye tija kwa Taifa, suala la Waziri Nyalandu kung’ang’ania ‘double entry’ kwa kisingizio cha kuua hoteli za kitalii hakina maana.
 “Iwapo mtalii atataka kurudi kununua chakula basi akiingia mara ya kwanza anaweza kwenda akanunua chakula na kuondoka na ‘take away’ hivi visingizio vingine vina harufu ya rushwa siyo bure,” anasema Msigwa.
  Akizungumzia Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) kutokuwa na Bodi ya Wakurugenzi, anasema kuwa kunatoa mwanya huo kwa Waziri Nyalandu kujichukulia uamuzi na mazingira ya ukiukwaji wa uwajibikaji.
 Anasema Waziri anakuwa na mamlaka ya kufanya mambo anavyotaka kinyume na bodi inapokuwapo. Hivyo kutokuwa bodi kunachangia kutokuwapo kwa uzingatiaji wa sheria na kanuni.


JAMHURI ilipotaka kujua ni sahihi kwa Waziri Nyalandu kusafiri na viongozi wa dini, wabunge kwenda nje ya nchi, Mchungaji Msigwa anabainisha kuwa huo ulikuwa mkakati wa kusaidia kupambana na kushamiri kwa vitendo vya ujangili nchini, hivyo hakukuwa na shida yoyote.
  “Ilikuwa inatengenezwa filamu ya kupambana na ujangili, mashirika ya nje tayari yamechangia zaidi ya Shilingi bilioni 200 kwa ajili ya kudhibiti ujangili nchini.
 “Lakini nina shaka kama fedha hizo zinaweza kutumika katika kampeni za uchaguzi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) badala ya kupelekwa sehemu sahihi,” anasema Msigwa.
 Akizungumzia kuwapo kwa ukaribu wake na Waziri Nyalandu anasema kuwa aliyeanzisha ukaribu wa Mchungaji Msigwa na Waziri Nyalandu ni gazeti la JAMHURI.


“Aliyeanzisha ukaribu wangu na Nyalandu ni ninyi JAMHURI. Kwanza niwaulize ukaribu wangu huo mnaousema ni upi? Nimekuwa nikifanya kazi na mawaziri wote wa wizara hii tangu enzi za Waziri Ezekiel Maige.
  “Niliweza kwenda Las Vegas, Marekani, wakati wa Waziri Balozi Khamis Kagasheki, nilikwenda Urusi na wakati huu wa Nyalandu nimekwenda Uarabuni na Marekani.  
  “Safari nyingine ambazo nimesafiri ni safari za kawaida na nyingine ni za Kamati za Kudumu za Bunge kama wabunge wengine wanavyosafiri.


“JAMHURI ndiyo iliyonizushia, sikuona haja ya kulipeleka mahakamani kwa sababu niliona ni upuuzi kwenda mahakamani, pia nilimdharau mwandishi wake maana hakufanya utafiti wa kina”.
  Pia akiongelea Wizara ya Maliasili kutokupeleka fedha Hazina zinazopatikana kutokana na mapato ya wizara hiyo, Msigwa anasema iwapo fedha hizo haziendi Hazina basi ni ukiukwaji wa taratibu.
  “Lakini ni lazima kutambua kuwa Hazina wakipelekewa fedha zimekuwa hazirudi kufanya kazi husika katika wizara. Sitetei kutokupelekwa fedha hizo Hazina, ni lazima Hazina wajitizame kwanini hawapokei fedha hizo, ni hatua zipi wamechukua kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa?” Anahoji Msigwa.
 
Jimboni
Akizungumzia masuala ya jimboni kwake na nafasi yake ya ubunge katika uchaguzi wa mwaka huu, Msigwa anasema anaamini uongozi unatolewa na Mwenyezi Mungu na kama hataki uwe kiongozi kamwe hutoweza kuwa kiongozi.  
 “Nimetimiza wajibu wangu, nimeweza kuungana na wenzangu, tumelifanya Bunge kuwa la kimapinduzi, jimboni nipo sawa natimiza wajibu wangu, lakini mwisho wa siku naamini uongozi unatoka kwa Mungu.”


  Anabainisha kuwa iwapo wananchi wa Iringa Mjini watataka kubadilisha uongozi basi apatikane mtu mwenye uwezo mkubwa kuliko yeye, uwezo wa kiuongozi na hoja si rangi ya nguo wala fedha.
 “Kama watataka kunibadilisha kama atatokea mtu mwenye uwezo zaidi yangu, nitamuunga mkono iwapo atanishinda.
  “Mwenye uwezo wa hoja siyo rangi ya shati na fedha zake, nipo tayari kukubaliana naye na kufanya naye kazi.”


  Kadhalika, alizungumzia maandamano ya wafanyabiashara wadogo wadogo (wamachinga) na kusema kuwa yalisaidia wananchi wa Jimbo la Iringa kujitambua.
  Anasema, “Haiwezekani mama ambaye anahangaika kutafuta mlo wa watoto wake asumbuliwe. Haya mambo ya kutoa fursa kwa wafanyabiashara yapo duniani kote, hii nilifanya kwa mapenzi mema kwa wananchi siyo kwamba sikuwa na kitanda cha kulalia nyumbani kwangu nikaenda kulala mahabusu na kesi ipo mahakamani, najivunia kwa hilo.”


  Aidha, Mchungaji Msigwa anasema kuwa Serikali ya Awamu ya Nne imeshindwa kudhibiti miundombinu nchini hasa Jiji la Dar es Salaam na kusababisha maafa makubwa.
  Anaeleza kuwa hii yote inatokana na viongozi upeo wao wa kufikiri kufikia mwisho.
  Pia anadai Rais Jakaya Kikwete ameshindwa kutimiza majukumu yake, zaidi amekuwa akikimbilia nchini Marekani huku nchi ikikumbwa na changamoto za migomo na maafa bila yeye kuwapo wakati amechaguliwa nchini Tanzania siyo Marekani.
  Anasema kuwa nchi imejaa madeni, ambapo deni la Taifa limefikia trilioni 40 kwa sasa, hivyo kila Mtanzania anadaiwa kiasi cha shilling laki 8.


 “Badala ya Rais kukaa na wataalamu kutatua changamoto za nchi yeye ‘anazurura’ na katika kipindi cha miezi saba amekwenda nchini Marekani mara tatu… kufanya nini hasa?”
 Mchungaji Msigwa anasema bajeti ya Serikali ya mwaka 2015/2016 ni kiasi cha Sh trilioni 22, ambazo ni sawa na nusu ya deni la Taifa, huku deni la wakandarasi likiwa Sh trilioni nane.
  “Miji yote duniani imejengwa kwa akili, hapa kwetu hatutumii akili ndiyo maana unaona unayoyaona. Hebu fikiri bajeti ya Wizara ya Maliasili itasomwa na kujadiliwa kwa siku moja tu, tena kwa masaa machache maana siku hiyo hiyo itasomwa na bajeti ya wizara nyingine, huu ni ulipuaji,” anasema Mchungaji Msigwa.

2750 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!