CONGO-DEMOCRATIC/Baada ya kundi la waasi la Allied Democratic Forces (ADF) kuua askari mahiri wawili wa Tanzania, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) sasa limetangaza mkakati mzito wa kusambaratisha kundi hilo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya JWTZ zinasema waasi hawa wamechokoza nyuki na kama walikuwa wanalilia wembe sasa watapewa.
 “Kwa kweli baada ya kuwadhibiti M23 kishujaa kabisa, ambao walithibitika kuwa chui wa karatasi, tulidhani waasi wengine wamejifunza, kumbe wapo hata hawa wanaoweza kuchapwa na mgambo wetu.


“Kwa kuwa wameua makamanda wetu watiifu wawili na kujeruhi wengine 16, sasa tunakamilisha mipango… watafute pa kwenda. Tutawasaka hadi kwenye mapango na kuhakikisha wanasambaratishwa,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya JWTZ kilichopo DRC.
“Kama ni silaha tunazo za kutosha. Tunazo silaha nzito na za kisasa. Tunachotaka ni wananchi kuendelea kuwa salama na kuishi kwa amani, sasa kama waasi hawa wameamua kutuchokoza, sisi hatuna jinsi zaidi ya kujitetea.
“Wangewauliza M23 kuwa JWTZ wakijitetea huwa inakuwaje? Majibu wangepata na wasingethubutu kuua askari wetu kwa kuwavamia wakiwa hawako vitani,” kiliongeza chanzo chetu.
Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Masanja, alizungumza na JAMHURI na kusema, “Wapiganaji wetu waliobaki wako salama.


“Na niseme tu taarifa kutoka huko DRC zinasema kwamba wapiganaji zaidi wamepelekwa huko Kivu baada ya shambulio. Umakini pia umeongezeka.”  
Meja Masanja anasema walichogundua haraka ni uelewa mdogo wa waasi hao “wasiotaka suluhu na Serikali ya DRC,” inayoongozwa na Rais Joseph Kabila.
Meja Masanja ameelezea kusikitishwa na waasi hao kuwavamiwa wanajeshi wetu 46 na kuua wawili huku wakijeruhi wengine 16.


“Kilichotokea kwenye jeshi tunaweza kuiita ni ajali. Maana unajipanga, lakini ukivamiwa na kujeruhiwa ni kama ajali ambazo hutokea kila siku,” anasema Meja Masanja na kuongeza: “Nadhani hawa ADF wanashindwa kuelewa kabisa kazi kubwa inayofanywa na majeshi ya Umoja wa Mataifa. Tumeongeza nguvu na umakini katika kukabiliana na hali hii, ili huku kuvamiwa kusirudiwe tena.”
  Anasema kasi ambayo majeshi ya UN yatakuwa nayo kwa sasa ni umakini zaidi kama waliofanya mwaka juzi walipokuwa wakikabiliana na waasi wa M23.


  “Nguvu ya M23 itaongezeka. Wapiganaji sasa watakuwa macho saa 24. Nadhani kwa kusema hayo tu inatosha na zaidi labda usikie kutoka huku. Lakini imesikitisha sana, lakini ifahamike tu kuwa hiyo ni ajali.
 “Watanzania wasiwe na wasiwasi kabisa juu ya wapiganaji wetu wanapokuwa kwenye mapambano hayo DRC,” anasisitiza Meja Masanja.
  Akisimulia kwa undani jinsi wanajeshi walivyovamiwa, Meja Masanja anasema wapiganaji hao walikuwa 46 ambao ni walinzi wa amani.


 “Of course (bila shaka) walikuwa wakisafiri kwa helikopta kutoka mji wa Abialose kuelekea Mavivi na baada ya kufika walikwenda Mayimoya kwa gari. Sasa wakiwa njiani walishambuliwa na ADF kwa silaha za kivita na gari moja kuteketezwa na kusababisha vifo vya askari wetu wawili na wengine 16  kujeruhiwa,” anasema.
  Anasema eneo ambalo wanajeshi hao walipigwa ni katika Kijiji cha Kikiki kilichoko kilomita 37, Kaskazini-Mashariki mwa mji wa Kivu.
  Taarifa kutoka DRC zinasema wapiganaji watiifu na wazalendo waliouawa ni pamoja na Private Juma Ally Khamis na Koplo Leonard Mkude.
Mpaka Jumamosi iliyopita, Meja Masanja alisema walikuwa wanasubiri taarifa zaidi kutoka DRC kujua taratibu za kurejesha miili ya mashujaa hao nchini.


JWTZ ni sehemu ya majeshi yaliyoko DRC yakiunda kikosi cha Umoja wa Mataifa kwenye operesheni ya kulinda amani kwa mujibu wa makubaliano ya mikataba ya kimataifa katika ushirikiano. Wanajeshi wengine wanatoka nchi za Afrika Kusini na Malawi.
  Kuuawa kwa askari hao nchini DRC kunafanya idadi ya makamanda shujaa waliouawa katika uwanja wa vita kufikia wanne. Wengine waliouawa ni Khatibu Mshindo aliyeuawa na waasi wa M23 hivyo majeshi hayo kupata hasira za kulisambaratisha kundi hilo.
 Mshindo alikuwa miongoni mwa askari wa JWTZ alipofikwa na mauti na wapiganaji wengine 10 walijeruhiwa kabla ya Luteni Rajabu Ahmed Mlima naye kuuawa.


  Vikosi hivyo vya UN vinashirikiana na Jeshi la Serikali la FRDC kukabiliana na waasi wanaoendesha vitendo vya uasi, mauaji na utekaji nyara raia mbalimbali wakiwamo huko DRC.
  Mikakati ya kundi hilo ilianza Oktoba, mwaka jana baada ya kudaiwa kuua wanakijiji zaidi ya 400 ‘waliowachoma’ juu ya uasi wao kwa serikali ya Kabila.


  Uongozi wa operesheni ya kulinda amani chini ya vikosi maalum vya Umoja wa Mataifa (MONUSCO), umetuma salamu kwa Watanzania ukiondoa hofu juu ya hali ya askari walioko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
  Katika salamu zilizotolewa na Kanali Felix Basse, vikosi ya UN kwa sasa vinafungua mapambano mapya kukabiliana na waasi wa kundi la ADF kama walivyofanya kwa kundi la M23, mwaka juzi.


  Amesema wapiganaji wote wakiwamo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa sasa wanachukua tahadhari kubwa kukabiliana na waasi hao wa ADF wanaoelezwa kuwa na mizizi yake nchini Uganda.
  JWTZ na majeshi washirika wamekunjua makucha huku Kanali Basse akisema mikakati ya operesheni ya kulinda amani chini ya vikosi maalum imeiimarika na itazidi kuimarika.


  Anasema makamanda walioko DRC wako zaidi 3,000 wanaounda jeshi la UN sasa wamepata kibali cha taasisi hiyo kubwa inayosimamia amani ya dunia.
  Basse katika salamu hizo amesisitiza, “Ni lazima kuendelea na mapigano.”
  JWTZ inayoundwa na wapiganaji mahiri imekuwa mstari wa mbele kuitikia wito na kujitolea pale inapobidi kulinda amani katika nchi zenye machafuko kama DRC.


Harakati za JWTZ zilianza tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere katika kuongoza Kamati ya Ukombozi kwa nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara wakati huo chini ya mwavuli wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU).
  Brigedia Jenerali Hashim Mbita (82) aliyefariki Aprili 26, mwaka huu kwa maradhi ya moyo, alipata kuwa Katibu Mtendaji wa kamati hiyo ya OAU kwa mafanikio makubwa.


  Brigedia Jenerali Mbita aliyejenga jeshi imara katika ukombozi, alizikwa kwa heshima zote za Serikali, Jeshi na dini Aprili 29, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
  Kamati hii iliyoongoza mapambano ya kupigania uhuru katika nchi za Afrika Kusini, Msumbiji, Zimbabwe (Rhodesia), Namibia na Angola, ambako majeshi ya Tanzania yalishiriki kikamilifu kumwondoa mkoloni.
  Tanzania ikiwa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi, ilifanikisha uhuru wa nchi zote za Kusini mwa Afrika na tangu wakati huo imekuwa sera ya Tanzania kushiriki ukombozi au kurejesha amani katika nchi mbali duniani.


Tanzania imeshiriki harakati za ukombozi katika nchi za Lebanon, Sudan katika Jimbo la Darfur na huko Comoro wakati wa kumwondoa madarakani Kanali Bacar. Uzoefu mkubwa ilioupata ndiyo inaoutumia kuwadhibiti waasi huko DRC.
Kundi la ADC litakuwa kama limechokoza nyuki kwa kuua askari hao wawili na mipango iliyotajwa ni kwamba ikianza kutekelezwa kundi hilo litasambaratishwa baada ya muda mfupi ujao.

By Jamhuri