Kuna maswali mengi unayoweza ukajiuliza kwa wachezaji wa Tanzania pale wanapoona mafanikio ya Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu. Miongoni mwa maswali hayo ni kwamba wanawaza nini? Wanajifunza nini?

Samatta kwa sasa anacheza soka la mafanikio katika Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, wakati Ulimwengu angali lulu katika timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kama Samatta aliyeanzia kukuza soka lake Mbagala Market, Dar es Salaam na Ulimwengu aliyekuwa akishinda kutwa nzima akijifua Uwanja wa Karume, Ilala wanawaza, inakuwaje Ibrahim Ajib na Simon Msuva washindwe?

Nimepata kuona maoni ya wadau kadhaa wa soka wakiwazungumzia wachezaji hao wanaokipiga Simba na Yanga kwamba ni zamu yao kwenda kwenye soka la ushindani zaidi.

Mashabiki wa soka Tanzania wanaendelea kutafuta wanapokwamia wachezaji kama Ajib na Msuva. Sababu mbalimbali zimekuwa zikitolewa kwa muda mrefu sasa, lakini sasa ni wakati wao kutoa majibu ya sababu ya kushindwa kunaswa huku nje. Je, wanataka kusema uongozi ni mbovu ukianzia kwenye kamati tendaji za klabu hadi benchi la ufundi? Ajib na Msuva wana majibu kwamba wanakwamia wapi.

Mara kadhaa viongozi wa soka wameelezwa kuwa na maslahi binafsi  wanapopata uongozi, kiasi kwamba husahau majukumu ya kuwaongezea ufanisi nyota wetu hadi kufikia mafanikio.

Eti wanadaiwa kuwa hawajali maslahi ya wachezaji na yale ya wapenzi wa soka katika nchi zao. Ajib na Msuva wana majibu.

Kuna hili linaloelezwa kuwa soka la Tanzania limetawaliwa na siasa chafu zisizo na tija wala maendeleo kwa wachezaji, hivyo kusababisha nyota kama Ajib na Msuva wasisonge kusonga mbele.

Itabidi tulazimike tu kuamini kwamba wadau wa soka wanaowania uongozi wa kisiasa kama vile ubunge na udiwani, hutumia nafasi hiyo kujipatia umaarufu, na wakifanikiwa huenda majimboni na kwenye kata kuendeleza fani ya siasa.

Kuna hili la maandalizi ya michuano ya kimataifa ambalo hufanyika kwa muda mfupi kwa wachezaji kujiandaa kana kwamba tarehe ya mechi haijulikani!

Je, sababu nyingine inaweza kuwa kiwango cha soka katika Ligi Kuu Vodacom Tanzania (VPL)? Maana wachezaji wengi hung’ara kutoka katika ligi na pia hufanya vema kwenye michuano ya kimataifa.

Labda nidhamu, inawezekana kweli Ajib na Msuva wakawa sehemu ya wachezaji wasio na nidhamu nzuri ndani na nje ya uwanja?

Hakuna ubishi kwamba kuna wachezaji wanaokunywa pombe, kuvuta sigara au hata bangi, lakini sidhani kama Msuva na Ajibu wamo kwenye kundi hilo. Kama wana nidhamu, hakuna shaka watakuwa na uzalendo, sifa itakayowasukuma kusonga mbele.

Tayari Mshauri wa Benchi la Ufundi la Taifa Stars na Kocha Mkuu wa JKT Ruvu, Abdallah ‘King’ Kibadeni, amemzungumzia Ajib akisema “Anahitaji juhudi kidogo tu uwanjani na kujitambua, atafanikiwa.”

Kwa mtazamo wa Kibadeni, mchezaji bora hana budi kujitambua na kutoa mchango wake katika timu, vitu ambavyo Ajib anavyo na anahitaji juhudi kidogo kusonga mbele. Ajib ana sifa hizo hivyo atujibu sababu za kutosonga mbele.

Msuva naye ana sifa hizo alizozionesha tangu msimu wa 2014/15 alipoibuka mfungaji bora kwa kupachika mabao 17, huku msimu huu akiwa na mabao sita baada ya kusugua sana benchi. Si mchezaji wa kubahatisha, na kwa msingi huo hana budi kutoa majibu sababu za yeye kushindwa kusonga mbele.

1387 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!