trio-madjesi_1554198

 

Bendi ya Trio Madjes 'Sosoliso' ilikuwa imesheheni vijana na kuweza kulitikisa jiji la Kinshasa huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo katika muziki.
Chanzo cha kuanzishwa kwa bendi hiyo kunaelezwa kuwa kulitokana na kuporomoka kwa Bendi ya Orchestra Veve baada ya wanamuziki wake wengi kuiacha bendi hiyo.


Mwanamuziki Kiamungwana Wazolambongo Mateta Verckys, alikuwa kiongozi wa bendi hiyo ya Orchestra Veve iliyotamba kuanzia miaka ya mwanzoni ya 1970.
Sifa kubwa ya Verkys ni kwamba alikuwa bingwa wa kulipuliza saxophone aliyesifiwa kuwa alikuwa na mapafu ya chuma. Alikuwa na umaarufu wa hali ya juu akiwa na bendi yake Orchestra Veve iliyotamba kila pembe za nchi hiyo.


Chini ya uongozi wake, Orchestra Veve ilikuwa na utaratibu wa kutoa kibao baada ya kibao ambavyo vyote hivyo vilitingisha nchi yake ya Kongo na nchi za jirani, Tanzania ikiwa mojawapo.
Msomaji wa makala hii ninadhani unazikumbuka nyimbo za 'Baluti', 'Vivita', 'Nakoma Juste', 'Ndona' na 'Kalala'. Kazi yao haikuishia hapo bali ilikuja pia na nyimbo za 'Mwanambulu', 'Mikolo Mileki mingi', 'Zonga Andowe', 'Nakomi tunaka', 'Likambo ya Kakokamwa'. Ana vibao vingi balaa.


Kama methali ya Kiswahili isemayo ngoma ikivuma sana hupasuka, ndicho kilichoisibu Orchestra Veve wakati waimbaji wake nyota watatu walipoona wanabanwa, wakachoropoka na kuanzisha kundi lao.
Wanamuziki hao walikuwa akina Matadidi 'Buana Kitoko' Mario,  Djeskin Loko Masengo na  Tshekabu 'Saak Sakoul' Bonghat. Nyota hao walipochomoka wakaenda kuanzisha bendi walioiita Orchestra Sosoliso. Inasemekana jina la Madjes lilitokana na mianzo ya majina yao — Mario Matadidi (Ma); Djeskin (Dje); Saak Sakoul' Bonghat (S) — Madjes. Trio Madjes.  


Pamoja na uchanga wake,  bendi hiyo ilipata umaarufu mkubwa mara baada ya kuanzishwa kwake. Wakiwa katika bendi hiyo walitengeneza nyimbo kabambe zilizokuwa tishio kwa bendi kubwa za Kinshasa. Nyimbo hizo zilikuwa za 'Bibie', 'Mousa', 'Sonie', 'Pambeni', 'Photo ya Madjesi', 'Toboye Africa', 'Matadidi' na 'Shery Nnuter'.


Maonesho ya Trio Madjesi kwenye maeneo ya Vile Place de la Voix du Zaire au maeneo ya Itaga katikati ya jiji la Kinshasa, yalichengua vilivyo watu waliokuwa wakijazana kwenye maonesho yao.
Inasimuliwa kwamba kuna siku walipokuwa wakifanya onesho, kundi la mashabiki walikuwa wamepanda juu kwenye paa la Kanisa la Mtakatifu Andrew maeneo ya Mature, ili wawaangalie. Paa la Kanisa lilikavunjika na baadhi ya vijana hao waliokuwa juu wakajeruhiwa na yasemekana hata vifo vilitokea baadaye.
Trio Madjesi na Sosoliso wakaendelea 'kuwasha moto' maeneo mengine nchini mwao wakiwa na vibao vyao vipya. Muziki wao uliwaingia wapenzi wengi na ndipo wakaanza kupata mialiko hata nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwenda kutoa burudani.


Wakongwe wa muziki wa Kongo hawakufurahia umaarufu wa ghafla waliokuwa wakipata hawa vijana hao. Wakaapa kulimaliza kundi hilo, hasa pale kundi lilipopata mwaliko wa kukaribishwa katika mji wa Paris na kupiga katika Ukumbi wa Olympia.
Wakongwe hao waliokuwa wakijiita The Three Musketeers waliwafanya akina Luambo Makiadi Franco, Tabu Ley Rochereau na Kiamungwana  Mateta Verckys, wajione kama vile utawala wao katika muziki wa Kongo ulielekea kuvurugwa kwa kuundwa bendi hiyo ya Trio Madjesi Sosoliso.


Aliyekuwa mmoja wa makatibu, alifanya mipango kiujanjaujanja hadi akajiunga katika bendi ya Trio Madjesi kwa nia ya kujua siri za bendi hiyo pasipo wenyewe kubaini kuwa yeye ni hasimu wao. Hasimu huyo baada ya kupata kazi hapo, akawa anapeleka taarifa za mipango yote ya Sosoliso Trio Madjesi kwa wazee.
Siku moja Trio Madjesi wakakaribishwa kwenye onesho walilolifanya Bangui nchini Chad. Walipolipwa fedha zao kwa pesa ya Kifaransa, wakaamua kubadilisha fedha zao kuwa za Zaire kwa njia ya magendo badala ya kutumia benki ya Zaire ili wapate fedha nzuri, jambo ambalo lilikuwa ni kosa la jinai.
Hasimu ndani ya bendi yao akapeleka taarifa kwa wazee wa Three Musketeers, haraka sana mambo yakasukwa na chama cha Wanamuziki cha Kongo wakati huo kikiitwa UMUZA (Union des Musiciens du Zaïre), kikatoa adhabu ya kuifungia bendi ya Sosoliso.


Aidha, adhabu hiyo iliambatana na ya viongozi wake kutofanya shughuli za muziki kwa miezi sita, hivyo safari ya Paris ikafa na mwanzo wa mwisho wa Sosoliso ukawadia.
Baada ya muda Matadidi Mario akaamua kurudi kwao Angola. Loko Masengo akahamia Congo Brazzaville, mpiga gitaa Makoso akajiunga na T.P. OK. Jazz. Saak Sakoul akapanda ndege na kuelekea Ufaransa. Wanamuziki nao wakasambaratika. Hasimu huyo aliyejulikana kwa jina la Manzenza Nsalamu Nsala naye alirejea katika bendi ya Luambo Makiadi baada ya kumaliza kazi aliyotumwa.
 
Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba: 0784 331200 na 0767 331200.

By Jamhuri