Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Dk. Akwilina Kayumba, amelalamikiwa mbele ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE), kuwa anawaongoza kimabavu wafanyakazi wa taasisi hiyo ya Serikali.

Pamoja na mambo mengine, Dk. Kayumba analalamikiwa kuwa amewagawa na kuwanyanyasa wafanyakazi wa OSHA, amesimamisha maslahi yao na kuendekeza upendeleo katika kuwapandisha madaraja.

 

Malalamiko hayo yamo kwenye risala ya tawi la wafanyakazi wa OSHA-TUGHE iliyosomwa kwa Mwenyekiti wa TUGHE, Dk. Diwani Mruttu, alipozuru ofisi za OSHA Dar es Salaam, wiki iliyopita.

 

“Kusimamishwa kwa maslahi ya wafanyakazi (incentives) kumesababisha wafanyakazi kukosa ari ya kazi na kukata tamaa, mfanyakazi anakaa katika ngazi moja bila kupandishwa daraja kwa muda mrefu.

 

“Utawala wa OSHA umewagawa wafanyakazi, kuna wafanyakazi wanaopata upendeleo wa wazi wa kimaslahi huku wengine wakitaabika. Mara kadhaa Mtendaji Mkuu amekuwa akisikika kwa wafanyakazi akisema “Asiyekuwa upande wangu hatafaidi OSHA”.

 

“Mtendaji Mkuu ameamua kufuta utaratibu wa wafanyakazi wa OSHA wa kushiriki mashindano ya Shimiwi. Baadhi ya kero za wafanyakazi na tofauti zilizopo kati ya Mtendaji Mkuu na wafanyakazi hazitatuliwi,” inaeleza sehemu ya risala hiyo.

 

Wafanyakazi hao walimwomba Dk. Mruttu kuingilia unyanyasaji na uonevu wanaofanyiwa na Mtendaji Mkuu huyo wa OSHA, ili kunusuru kuparaganyika kwa taasisi hiyo ya Serikali.

 

Akijibu malalamiko hayo, Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Mruttu, alieleza kusikitishwa na vinavyodaiwa kutekelezwa na kiongozi huyo wa OSHA, na kuahidi kufuatilia na kuchukua hatua zinazostahili.

 

Alisema atatumia kofia ya TUGHE kushughulikia malalamiko hayo kwa ufanisi kama hatua mojawapo ya kurejesha ari ya kazi kwa wafanyakazi wa OSHA.

 

Awali, katika tukio lisilo la kawaida, Dk. Kayumba aliwazuia waandishi wa habari waliofuatana na Dk. Mruttu kushiriki katika mkutano wa Mwenyekiti huyo wa TUGHE na wafanyakazi wa OSHA.

 

“Mimi kama Mtendaji Mkuu wa OSHA na familia yangu sijawaalika waandishi wa habari kuja hapa, nimemwalika Mwenyekiti wa TUGHE na si waandishi,” alisema Dk. Kayumba huku akionekana mwenye wasiwasi kubwa.

 

Hata hivyo, waandishi wa vyombo mbalimbali waliokuwa wamefuatana na Mwenyekiti huyo wa TUGHE, waliamua kuondoka lakini baada ya mkutano huo alikutana na kuzungumza nao ambapo alilaani kitendo hicho.

 

Kitendo cha Dk. Kayumba kuwazuia waandishi kushiriki mkutano huo licha ya kuwa walifuatana na Mwenyekiti wa TUGHE, huenda kililenga kuficha uovu unaolalamikiwa na wafanyakazi wa OSHA.

 

By Jamhuri