Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) na kituo cha Urithi wa Dunia (WHC) wameikubalia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) ifanye upembuzi yakinifu wa barabara ya Lodoare-Serengeti.

Katika makubaliano hayo, NCAA imeridhia ukarabati wa barabara kutoka lango la Lodoare kuelekea lango la Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) kwa kiwango cha changarawe yenye uimara wa hali ya juu.

 

Kaimu Mkuregenzi Uendeshaji, Mhandisi Joseph Mallya, ameeleza hayo katika kikao cha 32 cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Arusha, hivi karibuni.

 

”Kwa kuzingatia hali halisi na changamoto zilizopo, barabara hii inahitajika kujengwa kwa kiwango cha changarawe chenye uimara wa kudumu,” amesisitiza.

 

Amefafanua kuwa tayari NCAA imeshawasiliana na kituo cha WHC na UNESCO ambao ni wadau wakuu wa kimataifa katika suala la changamoto za barabra ndani ya hifadhi, na hasa barabara kuu kupatiwa matengenezo ya kiwango stahiki.

 

”Kimsingi UNESCO wamekubali NCAA ifanye upembuzi yakinifu wa maradi huu, ikiwa ni pamoja na kuangalia athari za kimazingira na kijamii na kuahidi kutoa ushauri au mapendekezo na hatimaye maamuzi ya mbinu bora ya kuimarisha barabara hii,” amesema.

 

Ameongeza kuwa tayari mamlaka hiyo imeshaanza mchakato wa kuandaa hadidu za rejea kwa wataalamu watakaofanya kazi hiyo, kwa kuzingatia taratibu za Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2004.

 

Kwa muda mrefu ubovu wa barabara hiyo umekuwa ukilalamikiwa na madereva kwamba unasababisha magari kuharibika ovyo.

 

Please follow and like us:
Pin Share