Muuguzi Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Geita (DNO), Ifigenia Chagula, analalamikiwa na baadhi ya wamiliki wa vyuo binafsi vya uuguzi na ukunga kwa kuomba rushwa kwa kushinikiza.
  Hata hivyo, wamiliki hao hawajatekeleza maagizo ya Chagula ambaye sasa inadaiwa anatumia nafasi yake kama 'fimbo' ya kuwaadhibu wamiliki hao kwa kutimua wanachuo wanaofika hospitalini hapo kuchukua mafunzo kwa vitendo.
  Kutokana na hali hiyo, wamiliki hao walilazimika kutafuta nafasi ya mafunzo kwa wanachuo wao katika hospitali nyingine, nje ya Mkoa wa Geita na kufanikiwa.


  Dk. Paul Alphonce, anayemiliki Chuo cha Uuguzi na Ukunga cha Geita (GMLTC), kilichopo maeneo ya General Tyre katika mtaa wa Rwenge Mseto, Kata ya Kalangalala wilayani hapa, ni miongoni mwa walalamikaji.


  Mkurugenzi huyo alitoa pongezi kwa uongozi wa hospitali za Mnazi Mmoja Zanzibar, Nkinga Referral Miltalare (MH-Mwanza), Aga Khan Mwanza, Kitete Singida, Sekou-Toure Mwanza, Bunda DDH pamoja na Ndala ya Tabora kwa kuwapokea wanachuo wake kufanya mafunzo kwa vitendo.
  Mbali ya kuwanyima nafasi wanafunzi, muuguzo huyo anadaiwa pia kukifungia Chuo cha Uuguzi na Ukunga cha Saint Bernard kilichopo Mji Mdogo wa Katoro wilayani Geita.
  Hata hivyo, sababu za kufungwa kwa chuo hicho bado ni kitendawili kutokana na muuguzi huyo kutokuwa na mamlaka ya kufunga chuo kilichosajiliwa kwa mujibu wa sheria.
 
Dk. Alphonce aanza na onyo

Dk. Alphonce anasema kwamba iwapo Serikali haitaingilia kati na kumwajibisha muuguzi huyo, kuna hatari ya wanachuo wake kukosa mtihani wa usajili wa Baraza la Uuguzi Tanzania mara baada ya kuhitimu na hata kutokea machafuko.
  Anadai kuwa mbali na chuo chake kusajiliwa Baraza la Mafunzo Tanzania (NACTE) kwa usajili Na. Reg/HAS/147P, muuguzi huyo anadai hakitambui chuo hicho kisheria huku akishinikiza apewe hisa ili “amlinde mmiliki.”


  Dk. Alphonce anadai kuwa muuguzi huyo amemhakikishia kuwa hata wanafunzi wake watapokewa bila ya shaka kufanya mafunzo kwa vitendo endapo atapewa hisa katika chuo hicho.
  “Kinyume na (cha) hapo hataruhusu wanafunzi kukanyaga hospitalini hapo na pia atafanya mpango ili wanachuo wake wasisajiliwe na Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania mara watakapohitimu mafunzo yao,” anasema Dk. Alphonce.
  Dk. Alphonce anasema chuo hicho kilianzishwa Januari 5, 2014 na kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 70, kati ya hao 40 ni wasichana ambao wameingia Oktoba, mwaka jana.
 
Asimulia kisa na mkasa

Akisimulia kwa kina suala hilo, Dk. Alphonce anasema kwamba Juni, mwaka jana, Tabibu Mwandamizi wa Geita, Dk. Ndaki, na Ofisa Afya wa Masesa walifunga ghafla na kudai kwamba wao ndiyo wenye mamlaka ya kutoa usajili wa chuo.
  Kutokana na hali hiyo Dk. Alphonce alipeleka malalamiko kwa Mkurugenzi wa Halmashauri, Margareth Nakainga, aliyefika chuoni hapo siku iliyofuata akiambatana na daktari huyo na Bwana Afya wake.


Baada ya kufika kwenye chuo hicho, mkurugenzi alisikitishwa na hatua ya watumishi kufunga chuo hicho ilhali hawana mamlaka hivyo; akawaamuru kumuomba radhi Dk. Alphonce ambaye aliwasamehe.
  Wanafunzi wake wakapata nafasi ya mafunzo kwa vitendo lakini yalisitishwa tena na DNO Chagula kwa madai usajili unaotolewa na NACTE ni wa kitapeli na kwamba hautambuliki kisheria.


  “Nilisikitishwa sana na hatua hiyo ya kuita usajili wa NACTE ni wa kitapeli wakati ni halali na unatambulika kisheria na umefuata taratibu zote kama inavyoelekeza NACTE yenyewe,'' anasema.
  Taarifa zinasema kwamba kutokana na hali hiyo, Dk. Alphonce alimfuata DNO Chagula na katika mazungumzo yao, mambo yalimgeukia kwani muuguzi huyo inadaiwa alimtisha kufunga chuo chake iwapo hatakubali kumpa hisa.


  Dk. Alphonce anadai kuwa mbali ya kudai apewe hisa pia aliomba rushwa ili awaruhusu wanachuo hao kufanya mazoezi kwenye hospitali hiyo, lakini hata hivyo mkurugenzi huyo aligoma na badala yake akafunga safari hadi wizarani jijini Dar es Salaam kupata ufafanuzi wa hatua anazochukua DNO.
  “Nilionana na Katibu Mkuu na kunipatia barua inayoelekeza mafunzo kuendelea na katika barua hiyo wizara ilipongeza uongozi wa chuo chetu  kwa juhudi zetu na hatua tuliyofikia kuelekea kwenye malengo yetu,” anasema.


  Nakala ya barua hiyo aliikabidhi kwa Dk. Sijaona aliyewapongeza kwa mara nyingine, kisha wanachuo waliendelea na mazoezi yao yaliyokuwa yamezuiwa na muuguzi huyo.
  Hata hivyo, katika hali isiyo ya kawaida, ndani ya wiki moja wakati wanachuo hao wakiendelea na mazoezi hospitalini hapo, Januari 29, 2015 mkurugenzi wa chuo hicho alipokea wito kwenye Ofisi ya Patron wa hospitali aitwaye Mwita.


 “Nilipofika ofisini hapo, patron alionesha masikitiko yake na baadaye alinieleza amefokewa sana na muuguzi  huyo kuruhusu wanachuo wake kuendelea na mafunzo hospitalini hapo, ilhali alikwishawapiga marufuku,” anasema.
  Sababu alizoelezwa patron ni kwamba wanachuo hao hawana idhini ya Baraza Uuguzi Tanzania (TNMC) ambalo hata hivyo halihusiki na vyuo vyao isipokuwa NACTE ambayo ndiyo yenye jukumu la kusimamia wanachuo na wanafunzi.


 “Vituko hivi vimenichosha,” anasema Dk. Alphonce na kuongeza kuwa ndiyo maana kwa sasa ameamua kulipua ili umma uone namna wazalendo wanavyoweza kukandamizwa na akaongeza, “ingekuwa Mzungu amefungua chuo hiki angebebwa, hata kama hakukamilisha taratibu.”
  Anasema kwamba madhara aliyoyapata kutokana na kauli za muuguzi huyo ni pamoja na baadhi ya wazazi kuhofia kuleta watoto wao kujiunga na chuo hicho, wakidhani kimesajiliwa kitapeli kama ambavyo imekuwa ikienezwa na muuguzi huyo.


  Aliitaka Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwawajibisha viongozi mfano wa muuguzi huyo, wanaotumia vyeo vyao kugandamiza wanyonge, hali inayoonesha kudidimiza uchumi wa nchi.
  “Kauli kama hii ni mbaya sana kutamkwa na mtumishi wa umma kama huyu muuguzi,” anasema Dk. Alphonce.


  “Kumbuka hii ni mara ya pili wanachuo wanatimuliwa hospitalini hapo wasifanye mazoezi na sababu ya NACTE kutoa usajili wa kitapeli wakati siyo kweli, na hata wanapofukuzwa chokochoko zinaendelea, je, hii ni haki kweli?” anahoji.
  “Serikali lazima immulike huyu muuguzi maana kauli yake kuhusu chuo changu inaweza kuleta madhara makubwa kwa jamii na kwa Serikali yenyewe,” anasema.


  “Nimekuwa nikijiuliza iweje hospitali za rufaa za wilaya na mikoa zipokee wanachuo wangu na hii ya Geita iwafukuze kama mbwa kuna nini nyuma ya pazia yaani siku hizi watu wanalazimisha rushwa kwa nguvu wakati kunachombo cha kukamata wala rushwa, je, kipindi cha nyuma wakati chombo hicho hakuna hali ilikuwaje?” anahoji.
Hata hivyo, uchunguzi wa JAMHURI umebaini kuwa muuguzi huyu ana mtandao mkubwa kati yake na baadhi ya vigogo wa Baraza la Uuguzi Tanzania ambao wamekuwa wakimtumia kutisha wamiliki wa vyuo binafsi vya uuguzi kwa maslahi binafsi.


  Imebainika kwamba uchunguzi huo umebaini kuwa Novemba, 2014 kigogo mmoja wa TNMC (jina tunalihifadhi kwa sasa kwa kuwa hatukumpata kuzungumza naye), akiongozana na Chagula walifunga Chuo cha Saint Bernard kilichopo katika mji mdogo wa Katoro kinachomilikiwa na Padre wa Kanisa Katoliki.
  Mbali na chuo hicho kuwa na usajili, inaelezwa kilifungwa baada ya mmiliki wa chuo hicho kukosa fungu la kuwapa vigogo hao, hali iliyosababisha baadhi ya wanachuo kurudi majumbani na wengine kukimbilia katika vyuo vingine kikiwamo cha GMLTC kinachomilikiwa na Dk. Alphonce.


  Mbali na Chagula kuita chuo hicho cha kitapeli, JAMHURI imejiridhisha kwamba kina usajili halali kutokana na kuona nyaraka za usajili wa Chuo cha GMLTC zilizoandikwa na Mkurugenzi wa NACTE, ambapo nakala zake zimenakilishwa kwa Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Msajili Baraza la Maabara Tanzania pamoja na TNMC.
 
Dk. Sijaona aruka kimanga

Akizungumzia hali hiyo, Dk. Sijaona, mbali na kukiri muuguzi huyo kuwatimua wanafunzi wa Chuo cha Uuguzi cha GMLTC aliomba mwandishi amfuate muuguzi mwenyewe kuelezea sababu za uamuzi wake.
  “Mimi niliwaruhusu kufanya mafunzo kwa vitendo sababu walikuja na barua kutoka wizarani, lakini huyu muuguzi mfawidhi wa hospitali hakuwapo na aliporudi aliwafukuza kwa madai hawana barua kutoka TNMC, sasa sijui kama wana ugomvi wao, ila sijapata muda kuona kama Baraza la Uuguzi lina mamlaka au la kwenye vyuo hivi ila nitafuatilia kubaini ukweli,” anasema na kuongeza: “Lakini yawezekana anafanya hivyo kwa kuwa hajapata ruhusa kutoka TNMC, labda uje hapa nikupe muuguzi mwenyewe akueleze kwa nini aliwazuia wanafunzi hao kufanya mafunzo kwa vitendo.”
 
Alichosema DNO Chagula

Machi 18, mwaka huu, kati ya saa 6 hadi 7 mchana, gazeti hili lilipomtafuta Chagula kwa njia ya simu na gazeti hili kutoa ufafanuzi wa tuhuma zinazomkabili, ikiwa ni pamoja na kueleza mipaka waliyonayo kati ya TNMC na NACTE, alidai kuwa atafutwe baadaye saa 8 kwa kuwa wakati huo alikuwa kwenye kikao.
  “Samahani nipo kwenye kikao ila nilitoka nje kidogo kukusikiliza; naomba unipigie saa 8 mchana nitajibu maswali yako," alisema na kukata simu, lakini alipotafutwa saa 8 mchana kama alivyoomba hakupokea simu na badala yake aliikata.


  Alipotumiwa ujumbe wa maandishi kuhusu tuhuma zake huku akisisitiziwa kuzijibu kutokana na kutokuwa kinga ya kutoandika tuhuma zake kwa kuacha kujibu, aliamua kupiga simu.
  Akizungumza, Muuguzi Chagula, mbali na kudaiwa kufika mara kwa mara kwenye vyuo hivyo hususani GMLTC alijitetea kuwa hakitambui kilipo na wala mmiliki wake.


  Alipobanwa kwa maswali alidai kuwa mmiliki wa chuo hicho anamfahamu na alikiri kuwatimua wanafunzi wake kwenye Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa kile alichodai hakuwa amekidhi matakwa ya TNMC.
  “Chuo cha Saint Bernard kilifungwa na uongozi wa Baraza Taifa ambao walikuja Geita tukaambatana nao na tuliongea nao vizuri tukawaelewesha na sasa wameanza mchakato wa kutimiza masharti ya Baraza, hivyo hawawezi kunilalamikia,” anasema.


  “Hiki cha Geita mjini wahusika ni Geita Town Council (Halmashauri ya Mji) mimi sina mamlaka nacho na wala hatuingiliani nao sisi wilayani, maana kiko kwenye halmashauri nyingine, wala sijui kilipo,” anajitetea kabla ya kudai mmiliki wake anamfahamu.
  Alipotakiwa kujibu tuhuma za kuomba rushwa kwa mmiliki wa chuo cha GMLTC, aliyedai kumfahamu baada ya kubanwa maswali mazito, muuguzi huyo hakukiri wala kuzikana tuhuma hizo na badala yake alikata simu na kuizima kabisa.
 
Mtendaji TNMC anena

Akizungumza kwa kujiamini, mmoja wa watendaji wakuu wa TNMC, Andrew Kapaya, pamoja na kukiri baraza hilo kuwatumia wauguzi wafawidhi wa hospitali za wilaya na mikoa kukagua vyuo ambavyo havijakidhi matakwa ya kitaaluma, alikana kuwaagiza kuomba rushwa kama tuhuma zinazoelekezwa kwa Chagula.
  Anasema kwamba NACTE na TNMC wote wana mamlaka kwa mujibu wa sheria za nchi zilizopitishwa na Bunge kusajili vyuo.


  “Sisi tunaruhusiwa kufunga chuo chochote ambacho tunaona kwa mujibu wa sheria zetu hakijakidhi, lakini suala si kufunga ovyo tu,” anasema.
  “Kwa hiyo lazima tuhakikishe masuala ya taaluma yanafanyiwa kazi; suala hapa ni kushirikiana tu na hili suala la kufunga tunalibadilisha utaratibu kama NACTE ndiyo waliompa na sisi tunaona hajakidhi vigezo sisi tutamwandikia barua NACTE na yeye ndiye mwenye wajibu wa kumfungia yule,” anasema.


  “Kwa sababu yeye alimpa na kwa kuwa sisi tutakuwa tunajenga hoja wanayoitambua NACTE na iko kimsingi namna ya kusaidia nchi na watu, wala hakutakuwa na ubishi hapo sababu nia tupate wauguzi wazuri, kesho na kesho kutwa matatizo yanapokuwa mengi  hawataulizwa NACTE tutaulizwa sisi wauguzi gani hao, baraza gani hilo mbona mnafanya nini, mbona wauguzi wako hivi, hawataulizwa tena NACTE,” anafafanua.


  Anasema, “Ni makosa wanayoyafanya kusajili vyuo hivyo, moja ya sifa za chuo ni kuainisha wapi watafanyia mazoezi ya vitendo, kwa hiyo hata katika usajili wa NACTE lazima aoneshe sehemu ya mafunzo,   masharti ambayo yalitekelezwa na walalamikaji."

By Jamhuri