Ghafla juzi juzi wakati Waziri Mkuu keshatoa hotuba yake kuomba fedha kwa ofisi yake, nikashtuka kusikia kuwa Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, badala ya kutoa hotuba mbadala wa ile ya Waziri Mkuu, eti ameongea kwa dakika chache tu na kususia kikao. Nilipigwa butwaa.

Mapema mwezi huu Kiongozi huyo wa Upinzani alitamka hadharani kuunga mkono Rais Magufuli kwa hatua zake za kubana matumizi huku akielekeza fedha namna ile kutumika kwenye maendeleo ya wananchi – yaani shughuli za jamii.

Sasa ghafla nasikia Kiongozi yule yule- Freeman Mbowe – anang’aka na kuigeuka Serikali kwa maneno namna hii “bajeti inaongozwa na sheria, lakini kumekuwa na matumizi ya ziada ambayo wameambiwa yanafanyika kwa maagizo ya Rais badala ya Serikali kuwasilisha maombi bungeni ili yapitishwe (Soma Mwananchi Jumapili Na. 5749 la Aprili 24, 2016 uk. 4) “What a contradiction”.

Katika gazeti la Jambo Leo Toleo Na. 2404 la Aprili 07, 2016, Mbowe huyu huyu amenukuliwa akimpongeza Rais kwa uamuzi wake juu ya zile fedha za sherehe za Muungano. Leo hii bungeni anang’aka eti mbona hazikuombwa bungeni! Hapo we msomaji unamwelewaje kiongozi mkuu mwenye kigeugeu kama kinyonga? 

Mimi nashangaa sana. Hali hiyo peke yake inathibitisha upinzani hawakujiandaa kwa hatua nzuri na elekezo kwa kutetea wananchi wanyonge, ndiyo maana hawana hoja mbadala na wamepitwa na matukio ya Serikali ya Awamu ya Tano. Kutoka nje ya Bunge au kususia vikao si suluhisho mbadala. Kilichotarajiwa hapa ni upinzani kutoa bajeti mbadala kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na si kutoka bungeni.

Mtazamo sahihi kwa upinzani ni kushiriki vikao maana wanapokea posho ya aina mbili. Kuna ile posho ya malazi (mtu kuwa nje ya kituo chako cha kazi) inayojulikana kama “per diem” na iko posho ya kushiriki kikao ambayo inaitwa “sitting allowance”. Kama waheshimiwa siku ile wamepokea posho hii ya kikao huku hawakushiriki kikao huo ni ukwapuaji wa fedha za umma wa mchana kweupee! (Kiingereza tunasema “Day Light Robbery”). Walichangiaje kikao hiki huku walitoka nje na kususia kikao? Maadam hawakuchangia kimawazo, basi hawakustahili posho ya kikao.

Kule Afrika Magharibi kwa Wafaransa, Profesa Rènè Dumont katika Kitabu chake cha The FALSE START IN AFRICA, kwenye utangulizi aliandika maneno haya, “…. so we are not yet at the stage, at least locally, where independence is a means of effective evolution of the masses. Rather the masses have the impression that national sovereignty has created a privileged class which has cut itself off from them” (Tazama Rènè Dumont: Falls start in Africa, Author’s Introduction – page 20).

Hapa ni dhahiri, wenzetu hawa ni kikundi au niseme “tabaka” maalum Lenye kutafuta sifa na utambulisho wa kipekee badala ya kutumikia waliowachagua – wale wananchi wanaowaita “people” ambao Dumont anawaita “masses”. Hawa “masses” hawahitaji kuwaona viongozi wao mwenye runinga, bali waliwachagua kuwakilisha mawazo na mahitaji yao bungeni ili yasikike kwa Serikali.

Hapa, waheshimiwa wabunge wote wakubali maneno ya Rènè Dumont, kuwa ninyi wenzetu mko kikundi maalum “privileged class” na mnaitwa “WAHESHIMIWA” nyie si miongoni mwetu sisi “masses” tuliowapigia kura. Laiti mngekuwa miongoni mwetu, kamwe msingejiona kuwa ni tabaka maalum.

Uhuru, anaosema Dumont ni ule wa kuwaletea mabadiliko wananchi (masses) ameita “effective evolution of the masses”. Kumbe kwa kususia vikao vya bunge ndipo Dumont alisema “rather the masses have the impression that national sovereignty has created a privileged class (tabaka) which has cut off from them” maana yake nyie wenzetu waheshimiwa wabunge mnajitenga na sisi kabwela. Hii ndiyo picha sisi “masses” au CHADEMA wanawaita“people” tunavyowaona sasa.

Uchambuzi ule wa Rènè Dumont mie naukubali kwa maana, bungeni tunaona mnaongelea mishahara yenu, marupurupu yenu na namna ya kujipatia mikopo kiulaini kudai fedha za magari ya kifahari, kumbe Rais Magufuli ametuambia anataka maboresho ya wananchi wote wa Taifa hili hasa wanyonge wa hali ya chini.

Huu utumbuaji wa majipu anaoufanya ni katika kukusanya fedha kwa maendeleo ya elimu, afya, miundombinu na uchumi kwa wananchi wote. Sasa hata zile fedha Sh milioni 600 au Sh bilioni 6 (sijui sawasawa) zilizookolewa na Bunge kwa kuminya safari za nje, Naibu Spika alipozirudisha Hazina na kuomba zitengeneze madawati tunasikia waheshimiwa mmeziulizia eti idhini alitoa nani? Huo kama si ubinafsi wa kujiona, tutatafsirije ulizo lenu hilo?

Hapa matendo yenu na matamshi yanathibitisha nyie waheshimiwa mko TABAKA la pekee (privileged class), wakati sisi tu masses.

Wabunge wote, tunawaomba mkafanye kazi ya kuwatumikia “masses” waliowapigia kura. Mjaribu sana kushiriki na kuchangia mawazo mbadala bungeni. Mtafanya vikao kuwa hai kwa michango yenu chanya. Kususia vikao ni kupora haki za waliowachagua na ni aina ya ufisadi – kama hamkujua hivyo, basi sasa mjue. “Active participation is required not passive nor absenteeism”- katika Bunge huo ni aina ya unyonyaji. Kazi kubwa ya upinzani bungeni ni kutoa mawazo mbadala ya kujenga Taifa na kuibana Serikali inapokiuka sheria na taratibu.

Sisi wananchi (masses au people) tuliamini kuwa humo bungeni ninyi waheshimiwa wote mu WAZALENDO. Lakini sasa kwa tendo hili la kususia vikao tunaona inajitokeza hali kama ile katika kile kitabu cha “THE ANIMAL FARM”. Hadithi ile ya baadhi ya wanyama kujibagua na kujiona wao ni bora zaidi kuliko wale wanyama wengine mle shambani. Ndipo walipotoa tamko lile maarufu kwamba; “THAT ALL ANIMALS ARE EQUAL BUT SOME ANIMALS ARE MORE EQUAL THAN OTHERS (soma Animal Farm by George Orwell uk. 92).

Mawazo namna hii ni ya kibepari na ni ya hatari katika nchi inayojivunia umoja na usawa miongoni mwa watu wake. Wazo la u-tabaka, “sisi wa aina hii na “wao” wa aina ile katika nchi inayojenga ujamaa halikubariki. Eti kuna watu bora zaidi ya wengine ndio Dumont ameita “privileged class” na “masses”. Hapo ni mwelekeo ule ule wa kwenye ubepari.

Sisi sote hapa Tanzania tu raia sawa wa Taifa huru – “all are citizens of a sovereign independent state” tangu Desemba 9, 1961. Maneno hayo ya Baba wa Taifa yalikaziwa (cemented with) kwa maneno yake mengine haya, “forget the past. It is true that in education and wealth, many of the Europeans and Asians are still better off than you are – BUT, political control is in your hands. The Europeans and Asians, even if they wished to do so cannot use their property or their education to harm you. And to ALL OUR CITIZENS as a whole, I say this; my friends, let everyone of us put all he has into the work of building a Tanganyika in which there will be no more distinctions and divisions …” (Nyerere: Hotuba ya Ufunguzi wa Bunge la Jamhuri ya Tanganyika tarehe 10 Desemba, 1962: Soma hayo toka sura ile ya 40 uk. 181).

Ningeweza kutafsiri hivi: “Tusahau yaliyopita. Ni kweli Wazungu na Waasia wako mbele sana kielimu na kiuchumi kuliko ninyi. Lakini kisiasa wananchi sasa tunathibitisha. Basi, Wazungu na Waasia hawawezi kutudhuru hata wangetamanije. Kwa kutumia hiyo elimu yao au utajiri wao. Kwa hiyo basi, kwenu RAIA WOTE wa nchi hii, nawaambieni sasa kila mmoja wetu, ajizatiti kwa kila namna, kuijenga Tanganyika hii ili tuwe wamoja pasi na matabaka yoyote miongoni mwetu”. Tafsiri isiyo rasmi.

Hapo, Mwalimu alituhimiza tangu mwanzo tuwe na UTU, tujitambue heshima na thamani ya huo UTU wetu. Binadamu wote ni SAWA, kwa maana ya uraia wetu, mahitaji yetu, uwajibikaji wetu na kwa mantiki hiyo tujenge nchi huru na yenye amani.

Katika mwaka wa 55 wa huo Uhuru wetu kuna dalili za Watanzania kugawanyika katika matabaka. Rais wa Awamu ya Tano ameapa kuleta mabadiliko katika nchi hii. Anataka rasilimali za nchi hii ziwanufaishe wananchi wote. Pasiwepo matabaka miongoni mwa wananchi wenye kuwa nacho (matajiri) na wasiokuwa nacho (makabwela). Kwa hili, Rais anachukua hatua za makusudi kabisa kusafisha wanyonyaji. Ndipo anapotumbua majipu ya hao waliojinufaisha kwa jasho la wanyonge yaani “masses” au “people”.

Angependa viongozi wote katika ngazi zote hapa nchini wamuunge mkono kwa kumwombea na kwa kumsaidia. Wabunge WOTE ni viongozi katika Taifa hili. Inapotokea, kikundi cha wabunge badala ya kuchangia mawazo bungeni kuboresha hali ya nchi kwa ujumla wanajikita katika KUSUSIA vikao vya Bunge, hiyo ni DOSARI. Wanalialia wanakosa hili au hawatendewi inavyopasikana. Hapo ndipo Mfaransa anaona Waafrika tena viongozi waheshimiwa namna hii wanalingana na watoto wadogo – anawaita “matoto hayo – Le grande enfante.

Kwa nini tusiwathibitishie Wazungu wote kuwa viongozi wa Afrika tumepevuka na kamwe tusilinganishwe na matoto makubwa ya Wafaransa – Le grande enfante”. Ni sisi Waafrika tubadilike! Tupevuke tusidai kuonekana katika runinga. Hilo si la muhimu kwa maendeleo ya watu. La muhimu ni kutoa mawazo na maoni endelevu mbadala wa yale ya Serikali – Tuwe wenyewe na tusikubali kuwa manokoa na vivuli wa nchi za nje. Tudumishe demokrasia ya Kiafrika na hasa ya KITANZANIA. Mapambano bado yanaendelea. Aluta Continua. 

 

>>TAMATI

By Jamhuri