Na Deodatus Balile

Ndugu msomaji ninakushukuru kwa mrejesho mkubwa ulionipa wiki iliyopita. Sitairejea makala ya wiki iliyopita, ila leo nitazungumzia kwa uchache kilichomtokea aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi. Mwakabibi na mwenzake wamepandishwa kizimbani kwa kesi ya uhujumu uchumi na matumizi mabaya ya madaraka.

Sitanii, nilipata kuandika hapa kuwa “Ya Sabaya, tuandike majina yetu vizuri.” Mwakabibi ni mmoja wa wakurugenzi waliosumbua mno wananchi na waandishi wa habari. Temeke wakati wa uongozi wa Mwakabibi iligeuka gereza lisilo rasmi. Alinunua kontena akaliweka mbele ya ofisi zake, ambako alikuwa anakamata watu na kuwaweka chini ya ulinzi siku nzima kisha jioni anawakabidhi polisi Temeke.

Kontena hilo halikuwa na choo wala maji ya kunywa kwa watuhumiwa. Mbaya zaidi hakuwa na mamlaka ya kisheria kufanya hicho alichokuwa anafanya. Kwa Temeke ilifika mahala hata kama nyumba yako inavuja, ukikutwa unabadilisha bati bila kibali cha manispaa “vijana wa Mwakabibi” wanakukamata unakwenda unaswekwa ndani hadi atakapojisikia kukuachia.

Katika hili sisemi labda makosa hayo ndiyo ameshitakiwa nayo, ila kama nayo ni sehemu ya hayo makosa mashahidi wapo wengi wa kushuhudia hayo alivyowatesa. Napigiwa simu na watu kadhaa wanasema bado yupo bosi wao akina Mwakabibi na Sabaya, aliyewafundisha ‘ujangili’ huu. Wangependa naye kumwona anakamatwa kwani alitesa watu wengi ndani ya Dar es Salaam na nje ya Jiji la Dar es Salaam. Nadhani bado wanamvutia pumzi, ila ipo siku mbuyu utaanguka.

Sitanii, viongozi mnaoshikilia nyadhifa mbalimbali naomba niwasihi. Hizo nafasi mlizonazo mfahamu kuwa cheo ni dhamana. Msinyanyase wananchi kwa sababu mnayo nafasi ya kufanya hivyo. Dunia hii imejaa maajabu. Sina uhakika kama mlikwisha kuisikia hadithi ya mende kuangusha kabati au sisimizi kumuua tembo. Siku nikiwa na muda nitawasimulia hii, ila hakuna kisichowezekana chini ya jua. Naomba Mwakabibi na Sabaya watendewe haki kwa mujibu wa sheria.

Nikiachana na hilo la Mwakabibi, kuna hili tunaloliandika la mtandao unaosaka urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Naomba niweke wazi hapa kuwa kugombea urais ni haki ya kila Mtanzania. Kisichokubalika ni mbinu chafu kufikia lengo hili. Zinapoanza hujuma za kumfanya aliyeko madarakani aonekane hafai, tena ukaharibu mambo kwa ujanjaujanja hilo halikubaliki.

Unapopata hamu ya kufanya mbinu za kupandisha bei ya mafuta, vinywaji au kusababisha upungufu wa dawa hospitalini kwa hesabu ndefu kuwa wananchi watamchukia aliyeko madarakani, hilo halikubaliki. Jambo moja niliseme hapa. Unapofanya mbinu kama hizi, ni wazi kuna watu unaoshirikiana nao. Ufahamu kuwa siku na wewe ukiwa madarakani, watatumia mbinu sawa na hizo kukuangusha.

Ukiacha hilo, katika makala ya wiki iliyopita nilisema tuepuke Tanzania kugeuka taifa la uchaguzi. Nafahamu mwaka 1992 tuliingia mfumo wa vyama vingi. Inawezekana hatukuandaa vema kanuni za mchezo. Inawezekana pia hapa kwetu demokrasia haijakomaa kwa kiwango cha nchi za wenzetu. 

Kwa nchi nyingi zilizoendelea siasa za wazi hufanyika wakati wa kampeni na muda uliosalia wanasiasa hutumia vyombo vya habari, mikutano ya ndani, mabaraza ya halmashauri, bunge na makongamano kukosoana.

Sitanii, kwa hapa kwetu inaonekana kama tunafanya kampeni miaka mitano na zaidi. Tukimaliza uchaguzi, ndani ya chama tawala watu wanaanza kujipanga kwa ajili ya uchaguzi ujao. Kwa wapinzani, nao hawabaki nyuma. Rais aliyeko madarakani anajikuta anapambana na mishale kutoka ndani ya chama chake na kwa wapinzani. Binafsi hili naliwaza mno na naomba mwenye jibu sahihi anisaidie kunipa jibu hilo. Tufanyeje? Tufanye siasa muda wote au tutekeleze sera baada ya uchaguzi? Mungu ibariki Tanzania.

By Jamhuri