DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Hii ndiyo Yanga ninayoijua. Inaingia sokoni kibabe, inasajili kibabe, kisha mashabiki na wanachama wake nje wanaanza kupiga mikwara mtaani.

Simba si kama hawajasajili nyota, wamesajili nyota, lakini wako zao kimya katika ishu za mikwara na tambo kwenye vijiwe vyetu vya soka. Wako kimya mno. Ni kama vile hawajasajili!

Aliko shabiki au mwanachama wa Yanga ni rahisi kumjua kipindi hiki. Yanga si watu wa kujiweka nyuma nyuma. Tena siku hizi wamekuwa jeuri kweli.

Yanga ya Kaseke, Nchimbi na Metacha bado mashabiki wake waliisumbua Simba ya Chama, Miquessone na Bocco. Muda mwingine hadi mechi za watani, wao ndio walioibuka na ushindi! Unadhani Yanga hii ya sasa mashabiki wake watakuwa katika hali gani vijiweni?

Naelewa tambo zao nyakati hizi. Kuelekea msimu ujao timu yao imejiimarisha vya kutosha. Wamesajili katika kila eneo uwanjani.

Wamesajili langoni, wamesajili kulia, wamesajili kushoto, wamesajili ndani. Wamesajili kiungo wa ulinzi, wamesajili mawinga, wamesajili washambuliaji. Wamejiimarisha sana.

Mastaa wao wa msimu uliopita nafasi zao zimo shakani. Ni wachache wanaoweza kuingia kikosi cha kwanza cha sasa, wengi watakuwa benchi, wengine wengi tutakaa nao jukwaani.

Kwa haraka haraka wazawa Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Bakari Mwamnyeto ambao walikuwapo msimu uliopita huenda wakawa sehemu ya kikosi cha kwanza cha timu. Wazawa wengi nafasi zao wamejaziwa mafundi kutoka nje.

Rafiki yangu Makapu amefanya jambo jema kukimbilia Polisi Tanzania. Huko anaweza kupata dakika nyingi. Makapu amefanya jambo jema sana kuondoka.

Alishindwa kucheza Yanga ya kina Sarpong, Yanga hii ya kina Aucho anachezaje? Ni vigumu kucheza. Amefanya jambo sahihi kuondoka. Polisi Tanzania itampa dakika nyingi za kutosha katika kila inayoitwa wikiendi.

Simba walianza kuiunda timu yao katika mtindo huu. Wao hawakwenda mbali na nchi waliivamia Chamazi na kuchukua mastaa wa kutosha.

Mastaa hao ndio ukawa msingi wa kukiona tunachokiona sasa ndani ya kikosi chao. Yanga wao wameanzia nje ya nchi. Wao wamewavamia majirani zetu wa Congo. Huko wamechota mastaa wa kutosha.

536 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!