DAR ES SALAAM

Na Alex Kazenga

Manispaa ya Kigamboni imewekwa mtegoni na wakazi 31 wa Mtaa wa Magede, Kisarawe II, baada ya kuitaka itatue mgogoro wa ardhi baina yao na Kampuni ya Oilcom.

Mgogoro huo unahusu eneo la ekari 34 lililopo Magede ambapo wakazi hao wanadai maofisa ardhi wa manispaa wameruhusu eneo hilo kufanyiwa upimaji ‘juu’ ya upimaji mwingine.

 “Watu wa Idara ya Ardhi wa manispaa ndio wenye jukumu la kutoa ufafanuzi kwa sababu ndio waliolipima eneo letu na kutoa hati kwa pande zote.

“Tunataka kujua kwa nini walifanya upimaji juu ya upimaji mwingine na wakati wa kupima tunataka tujue iwapo taratibu zilifuatwa,” anasema Steven Mbuyakulema ambaye kiwanja chake kipo ndani ya uzio baada ya Oilcom kujenga ukuta wa matofali kuzunguka ekari hizo.

Mbuyakulema anasema wamefikisha malalamiko Halmashauri ya Kigamboni ili iweke wazi ni nani wapo kihalali katika eneo hilo.

Tangu wamefikisha malalamiko hayo kwenye Ofisi za Manispaa ya Kigamboni wanasema kumekuwapo na ucheleweshwaji wa makusudi wa kutoa uamuzi.

“Wakati tukisuluhishwa katika ngazi ya Serikali ya Mtaa na kata, mwakilishi wa Oilcom, Ally Mwinyi, alikuwa anakuja na maofisa ardhi wa manispaa kusikiliza mgogoro wetu.

 “Tulijihoji, iwapo anayekuja kusikiliza kesi yetu analetwa kwa usafiri wa gari la mtuhumiwa; hapo kuna haki kweli?” anasema Mbuyakulema.

Akizungumzia mgogoro huo kwa kina, Dotto Mabullah, mwenye makazi katika eneo hilo anasema mzozo baina yao na Oilcom umeanza mwaka 2017.

Anasema ulianza baada ya watu waliojitambulisha kuwa wafanyakazi wa Oilcom kufika katika maeneo hayo na kudai kuwa wamekuja kufufua mipaka ya eneo lao la ekari 34.

“Wao walidai eneo hili wameuziwa mwaka 1988. Walidai kuwa aliyewauzia ni Mhindi anayeitwa Ikbal. Walilifanyia upimaji mwaka 2007,” anasema Mabullah.

Kutokana na kitendo hicho, Mabullah anasema iliwalazimu wananchi wote wenye maeneo katika eneo lililotajwa kukutana pamoja ili kujadili pamoja taarifa hiyo.

Desemba 2017 wakazi hao walifanya kikao ambapo mwakilishi wa Oilcom, Mwinyi, alifika katika kikao hicho na kudai kuwa eneo hilo lilikuwa limetelekezwa kwa muda mrefu.

“Alitueleza kwamba yuko tayari kutufidia ambao tumo ndani ya eneo lake. Tulikubaliana eneo liwekwe uzio wa nguzo ili tutambulike kirahisi,” anasema Mabullah.

Makubaliano hayo yalifuatiwa na kikao cha Januari 14, 2018 ambapo Oilcom kupitia kwa Ally Mwinyi walihiari kuzungumza na mwananchi mmoja mmoja kuhusu viwango na utaratibu wa kulipa fidia.

Suala la kulipa fidia lilishindikana baada ya Oilcom kushindwa kuelewana viwango vya fidia ambayo wananchi hao walitaka walipwe.

Hatua hiyo ilifuatiwa na Mwinyi kujitoa kwamba hahusiki tena na suala la ulipaji fidia na badala yake likakabidhiwa kwa mtu mwingine aliyemtaja kwa jina la Fahad.

Pamoja na wananchi kuhiari kushiriki hatua hizo, Mabullah anasema baadhi yao hawakuwa wameafiki kuhusu suala hilo kwani ushahidi unadhihirisha uhalali wa Oilcom kulimiliki haukuwa wazi.

“Oilcom wanadai kuwa wafanyakazi waliopewa kukilinda kiwanja hiki ndio wameuza baadhi ya maeneo kwa watu.

“Ukimhoji Mwinyi aonyeshe watu waliouziwa na vielelezo vyake anakuja juu, anasema sisi tunamiliki vikaratasi vya mauziano vilivyoandikwa na mwenyekiti wa serikali ya mtaa ilhali yeye anamiliki nyaraka iliyoandikwa na Kamishna wa Ardhi na hati ambayo anailipia kila mwaka,” anasema Mabullah.

Mabullah anasema walidai kupatiwa ushahidi wa nyaraka hizo ili wajiridhishe lakini akashindwa na badala yake alitengeneza mazingira ya kampuni hiyo kushitakiwa mahakamani na Kamishna wa Ardhi kwa kutokulipa kodi ya eneo hilo.

Baada ya Oilcom kushitakiwa kwa kutokulipa kodi ya ardhi takriban Sh milioni 50, Mabullah anasema walikwenda mahakamani na kueleza kuwa wanashindwa kuilipa kodi hiyo kwa sababu eneo limemilikishwa kwa watu wengine.

Hatua hiyo ilifuatiwa na maofisa ardhi wa manispaa kufika katika maeneo hayo ambapo walikiri uwepo wa upimaji juu ya upimaji mwingine.

Baada ya ushahidi huo mahakama iliendelea na kesi na baadaye ikatoa uamuzi kama Oilcom atashindwa kulipa kodi kiwanja hicho kiuzwe kwa mnada kwa watu wengine ili kodi ya serikali ipatikane.

Hukumu hiyo ilipotoka Oilcom walikwenda Wizara ya Ardhi na kulipia kodi waliyokuwa wakidaiwa kisha manispaa ikaridhia kuwa Oilcom ndiye mmiliki halali wa kiwanja hicho.

Octapy Banga ambaye mashamba yake pia yamo kwenye mgogoro huo anasema eneo hilo halina tatizo bali watendaji wachache serikalini wanashirikiana na Oilcom kuukuza kwa masilahi binafsi.

Anasema ofisi ya mkurugenzi inapaswa kuwa makini katika kutoa uamuzi juu ya mgogoro huo kwani wenyeviti wa Madege waliotakiwa kutoa ushahidi wamekana hadharani kutomtambua Oilcom katika eneo hilo.

“Tunavyochelewa kufikia uamuzi sijui mkurugenzi wa manispaa anataka tumpe ushahidi gani,” anasema Banga huku akisema kumekuwa na tabia ya madalali kupora maeneo ya watu na kwenda kwa mmiliki wa Oilcom kumueleza kuwa wamepata eneo awape fedha wakalinunue.

Banga anasema wanamtaka mmiliki wa Oilcom ajitokeze ili waweze kumhoji na ajibu kweli kama eneo hilo ni mali yake.

“Awali, Mwinyi alikuwa akidanganya kwamba eneo hilo Oilcom ameuziwa na Ikbal lakini baadaye akakiri kwamba alidanganya kwani ameuziwa na watu wanne,” anasema Banga.

Hata hivyo, Banga anasema hadi leo ushahidi wa watu wanne anaowataja Mwinyi kwamba ndio waliouza eneo hilo hawajawahi kujitokeza wala kufika Manispaa ya Kigamboni kuonyesha ushahidi wa kuuza eneo hilo kwa Oilcom.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Madege, Selemani Koba, amelieleza JAMHURI kuwa mgogoro upo ngazi ya manispaa, hivyo hawezi kuutolea ufafanuzi, lakini yuko tayari kushirikiana na wananchi kutoa ushahidi kuhusu eneo hilo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kisarawe II, Issa Hemed, amelieleza JAMHURI kuwa alifanya jitihada kuwaunganisha wananchi hao na Oilcom ili waweze kufikia mwafaka lakini ilishindikana.

“Nilifanya kadiri ninavyoweza wananchi walipwe fidia wampishe mwekezaji lakini makubaliano yakawa mabovu. Nikaamua kujiondoa,” anasema Hemed.

Akiuzungumzia mgogoro huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kigamboni, Erasto Kiwale, anasema umefikia hatua nzuri ya kupata ufumbuzi.

Anasema amekwisha kukaa vikao mara tatu na wakazi wa Madege wenye mgogoro pamoja na mwakilishi wa Oilcom ofisini kwake ili kujadiliana suala hilo lakini hawakufikia uamuzi baada ya wakazi hao kumkataa mwakilishi huyo na badala yake wanadai wanataka kukutana na mmiliki wa Oilcom mwenyewe.

Awali ilidaiwa kuwa mkurugenzi wa Oilcom alikuwa akimtuma Ally Mwinyi kumwakilisha lakini kutokana na wakazi hao kuhisi suala hilo kuwa na utapeli ndani yake wanamtaka Oilcom mwenyewe ndiye aje wajadiliane.

“Kiongozi mkuu wa Oilcom tuliwasiliana, akadai yupo nje ya nchi, sasa hivi amerudi, tuko kwenye hatua za kuwakutanisha tupate ufumbuzi wa suala lao,” anasema Kiwale.

Anasema kwa sababu ndani ya mgogoro huo kuna masuala mengi ya kisheria, wanalenga kuutatua kwa kuzingatia vipengele ambavyo havitaathiri pande zote.

Anasema wamefikia hatua ya kutafuta suluhu kwa njia za kiutawala kwa sababu kuna masuala mengi ambayo yanaleta mkanganyiko, likiwamo suala la eneo hilo kuwa na hati mbili za umiliki, zote zikiwa halali.

“Kuna hati ndogo ndogo za wananchi wa Madege ndani ya hati kubwa ya Oilcom.

“Nia ya kuutatua iko palepale. Kwa sasa hivi tunauchambua vizuri mgogoro huo ili kuona namna nzuri ya kuumaliza kisheria,” anasema Kiwale.

Kwa upande wake, Mwinyi, anasema kwa sababu suala liko ofisi za manispaa hawezi kulizungumzia bali anawaachia maofisa wanaohusika kulishughulikia kwa kuzingatia taratibu za serikali.

“Manispaa ni ya serikali, hivyo naiamini itatenda haki na imewekwa kwa ajili ya kutatua kero za wananchi likiwamo suala la mgogoro unaousema.

“Sina maelezo mengine zaidi ya yale ambayo manispaa wanayafanyia kazi,” anasema Mwinyi.

Kuhusu uhalali wa leseni ya Oilcom katika eneo hilo, Mwinyi anasema malalamiko ya wananchi yawe halali au yasiwe halali vyombo vinavyohusika na upimaji wa ardhi vitathibitisha suala hilo kisheria.

“Vyombo vya kutatua malalamiko ya wananchi kisheria vipo, hao wanaolalamika wapeleke malalamiko yao kwenye ofisi husika wapate haki yao,” anasema Mwinyi.

Kuhusu Oilcom kutokuwa na ushahidi wala nyaraka zinazothibitisha umiliki wa eneo hilo anasema halina ukweli bali ni maneno ya kutunga.

“Hao wananchi wanavyotaka wao suala lao liendeshwe manispaa haitaki, ndiyo maana hakuna maelewano.

“Wao wanataka waiendeshe manispaa wakati wao si waendeshaji wa manispaa,” anasema Mwinyi huku akisisitiza kuwa kuleta suala la mgogoro huo kwenye vyombo vya habari si suluhisho la wao kupata haki yao.

461 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!