Bupe Mwaipopo:

 

Jina la Bupe limepata umaarufu sana katika Kituo cha Mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi cha Ubungo (UBT) jijini Dar es Salaam.

Umaarufu wa jina hili unatokana na mmiliki wa jina hili kufanya kazi ambayo wengi imewashtua na kuwafanya wakati mwingine wamshangae mwanamke huyu.

Lakini yeye anasema kuwa ulimwengu wa sasa si wa kuchagua kazi, bali ni wa kufanya kazi kwa kujituma zaidi ili kuboresha hali ya maisha tuliyonayo kwa sasa.

 

Kumekuwa na tabia ya baadhi ya watu kuchagua kazi za kufanya kutokana na jinsia zao. Kwa maana ya kwamba kuna watu wanaoamini kuwa kuna kazi ambazo ni maalum kwa wanaume na nyingine ni kwa wanawake. Mtizamo huu ni tofauti kabisa na ule alionao mwanadada Bupe, ambaye ameamua kufanya kazi ya kung’arisha viatu kama kazi yake ya kumwingizia kipato cha kila siku.

Bupe anafanya kazi hii katika eneo la Kituo cha Mabasi cha Ubungo jijini.

Akielezea historia yake, Bupe anasema kuwa alimaliza kidato cha nne mwaka 2002 katika Shule ya Sekondari ya Usongwe iliyoko mkoni Mbeya.

Baada ya hapo alipata kazi ya kufundisha katika Shule ya Msingi ya Nsoho, Mbeya, kama mwalimu wa shule ya awali, kazi aliyoifanya kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kuja Dar es Salaama kwa ndugu yake, ikiwa ni katika harakati za kutafuta maisha.

Akiwa kwa ndugu yake Dar es Salaam alianza kufanya kazi katika saluni, kazi ambayo anasema kuwa hakuifanya kwa muda mrefu kwa madai kuwa ilikuwa inamwingizia kipato kidogo. Baada ya hapo Bupe alianza kujishughulisha na kazi za kufuma kofia.

“Hii ni kazi ambayo kidogo ilianza kunipa mwanga, kwani baada ya hapo nilipata mtaji na nilifungua sehemu nikawa nauza vifaa vya baiskeli,” anasema Bupe.

Katika utaratibu wa kuuza vifaa vya baiskeli, Bupe anasema kwamba alikuwa na kijana aliyemwajiri kwa ajili ya kuhakikisha kuwa asilimia kubwa ya wateja wake wanaonunua vifaa vya baiskeli waweze kutengeneza baiskeli zao pale pale.

Katika eneo hilo hilo pia akamweka kijana mwingine maalum kwa ajili ya kutoa huduma ya kung’arisha na kushona viatu.

Kwa hiyo katika eneo hilo Bupe alikuwa na biashara za aina mbili — aliwaajiri vijana wawili. Ndani ya kipindi cha miaka miwili Bupe akiwa anasimamia biashara zake, alihakikisha anajifunza ufundi wa baiskeli, hali kadhalika akajifunza kushona na kung’arisha viatu.

Utaalamu huu aliupata kwa njia ya kuangalia wale vijana jinsi walivyokuwa wakiwahudumia wateja wake.

Bupe aliamua kuachana na biashara ya uuzaji wa vifaa vya basikeli baada ya eneo alilokuwa akifanyia biashara kuuzwa kwa mmiliki mwingine.

Hapo ndipo Bupe alipopata wazo la kuja kufanya biashara katika Kituo cha Mabasi cha Ubungo na kuanza kazi ya kung’arisha viatu.

“Nilikuja hapa kama vile wanavyokuja watu wengine, nikaomba nafasi, nikafuata taratibu zote nikapewa. Kazi hii naichukulia kama ilivyo kazi nyingine. Maisha ya sasa hivi siyo ya kuchagua kazi,” anasema Bupe.

Mafanikio

Bupe, mama mwenye mtoto mmoja wa kike mwenye umri wa miaka saba sasa, anasema kuwa kazi hiyo imemsaidia kufanya mambo mengi ya muhimu katika maisha yake.

“Kwa kweli nathubutu kusema kuwa kupitia hii kazi yangu ya kung’arisha viatu nimeweza kufanya mambo mengi na mazuri katika maisha yangu, vitu vingine nisingependa kuvitaja, ila ningependa kusisitiza kwamba niko mbali kidogo kimaisha,” anasisitiza.

Bupe anasema kuwa kazi yake imempa nafasi ya kufahamiana na watu wengi, tofauti na ilivyokuwa awali.

“Nikiangalia idadi ya watu ninaofahamiana nao kwa sasa na zamani ni tofauti, hii kwangu ni mojawapo ya mafanikio makubwa kwani dunia ya sasa ni kufahamiana na watu, huwezi kuishi kivyako vyako,” anasisitiza.

Kitu gani kinamfanya Bupe kuwa tofauti na wengine?

Ukiingia ndani ya Stendi ya Ubungo, kila mtu anataka kung’arisha kiatu chake kwa Bupe, kwanini? Bupe anasema kuwa siri ya mafanikio katika hilo ni kauli nzuri kwa wateja wake pamoja na kuonesha umahiri katika utendaji wa kazi yake.

“Biashara zote zinahitaji kauli nzuri na uvumilivu kwa sababu kuna ile hali ya kuhudumia watu tofauti, mbali na kauli nzuri pia suala la utoaji huduma bora bado ni muhimu ili mteja aliyekuja leo na kesho aweze kurudi tena,” anasema Bupe.

Pamoja na hayo, Bupe anasema kuwa kitu kingine kinachomfanya kuwa tofauti na wengine, ni ile hali ya kumshauri mteja jinsi ya kuhudumia kiatu chake.

“Mteja anapokuja kwangu huwa namshauri kabla sijaanza kuhudumia kiatu chake, hali hii pia inanifanya kuwa tofauti na wengine kwa sababu si kila fundi ana utaalamu kama nilionao mimi,” anasema Bupe.

Wito wake kwa wanawake wengine

“Wanawake wenzangu hawana budi kufanya kazi mbalimbali katika jamii yetu kuliko kukaa vijiweni na kujadili mambo ambayo hayana msingi. Kwa mfano, mimi hapa huwa sina muda wa kukaa kijiweni na kujadili habari za watu wengine,” anasema Bupe.


Matarajio ya baadaye

Bupe ana ndoto ya kumiliki kitegauchumi kitakachompa nafasi ya yeye kuwa msimamizi wa shughuli zake kuliko kuwa mtendaji kama ilivyo sasa.

“Nimekuwa mtendaji sana muda mrefu katika hizi shughuli zangu, nataka kuwa mtu wa kufuatilia mipango zaidi kuliko kuwa mtendaji, kwa mfano, kwa utaratibu wangu wa sasa hivi sina Jumapili wala Jumamosi,” anasema.

Bupe ana matarajio ya kuwa na kiwanda cha kutengeza viatu, ambacho kitatoa huduma bora kwa Watanzania kwa bei ambayo inaendana na mazingira ya Kitanzania.

 

Anasema kuwa si kila kiatu kinafaa katika mazingira yetu, bali Watanzania wanatakiwa kuwa na viatu ambavyo vitaendana na mazingira waliyonayo.


 

By Jamhuri