Sababu za kupungua nguvu za kiume

 

Tatizo la upungufu wa nguvu za kiume limekuwa kubwa sana hivi leo katika zama hizi za sayansi na teknolojia, ni tatizo linalowakabili wanaume wengi mno; wazee kwa vijana karibu kote duniani na hususan maeneo ya mijini zaidi.

Hapo zamani, tatizo hili lilikuwa la wazee zaidi, lakini jambo la ajabu na la kuhuzunisha leo limekuwa ni tatizo la vijana zaidi kuliko hata wazee!

 

Utamkuta mwanaume  ni kijana wa miaka 25 au 30 au 40, lakini jinsi anavyotenda tendo la ndoa ni sawa na mzee wa miaka 90 au 100.

Atakwambia; “Ninafika kileleni ndani ya dakika mbili,” au “Nikimaliza tendo la ndoa raundi ya kwanza, siwezi kurudia mpaka kesho yake!” au “Uume wangu unasimama kwa ulegevu sana, na nikiingia ukeni tu, unakufa (unalegea)!”

Habari kama hizo ni nyingi kwa namna tofauti tofauti na kwa watu wengi sana. Ni utitiri wa watu, vijana kwa wazee, na vijana ndiyo wakiwa wameshika usukani. Kwa bahati nzuri matatizo mengi ya nguvu za kiume yanatibika, lakini iwapo tu kama matibabu sahihi (yanayoanzia kwenye chanzo cha tatizo yatapatikana).

Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana waathirika wengi wa nguvu za kiume wamekuwa wakikurupuka tu kubugia dawa, na hii ndiyo sababu wamekuwa hawaponi licha ya kutumia dawa chungu nzima, na pia wamekuwa wakipoteza pesa nyingi bure tu kwa matibabu hayo ya kubahatisha.

Pia kutokana na tatizo hili kuwa kubwa, kila kuchapo huibuka watu wanaodai wanaweza kutibu na kumaliza tatizo kabisa. Kwenye magazeti, kwenye mabango mitaani, katika redio n.k, kuna utitiri wa matangazo juu ya tatizo hili.

Lakini, kinachokata maini zaidi ni kwamba wengi wa wataalamu hao hawajui sababu za kupungua nguvu za kiume, wala hawajui utendaji wa mwili wa binadamu. Wengi wanadhani kuishiwa au kupungua nguvu za kiume ndiyo ugonjwa wenyewe.

Kupungua nguvu za kiume siyo ugonjwa, ni dalili ya ugonjwa. Kuna sababu zake ndani ya mwili. Sababu hizo ni nyingi mno, ni zaidi ya 100! Anatakiwa daktari mtaalamu aliyebobea katika uzazi, mifumo ya mkojo, anayelijua vizuri figo ndani na nje, ini na mifumo mingine ya mwili, ikiwa ni pamoja na kemia ya mwili. Na inatakiwa dawa iende kutibu chanzo cha tatizo.

Kuna madhara makubwa kutumia dawa kwa kubahatisha, hata kama dawa hizo zitadaiwa au zitaelezwa kuwa hazina madhara, kwamba ni asilia aslimia mia, bado unaweza kudhurika!

Kwa nini upate madhara wakati dawa hazina madhara?

Naam! Unapata madhara kwa sababu utakuwa unaacha kutibu chanzo cha tatizo, na badala yake utakuwa unashughulika na kitu kingine, hali ambayo itafanya  tatizo liwe kubwa zaidi.

Katika makala haya tutatazama mambo yanayosababisha  mtu aishiwe nguvu za kiume.

Unapojua  sababu umejua matibabu. Watu wengi wanateseka  majumbani mwao kimya kimya hawajui wakimbilie wapi, waanzie wapi, nani wa kuwasaidia!

Makala haya yatamfungua msomaji aweze kuutambua mwili wake, tatizo lake na wapi pa kuanzia na nini cha kufanya kwa ajili ya matibabu. Hivyo, ndugu msomaji fuatilia makala haya upate faida kubwa sana ambayo hutaipata mahala popote.

Upungufu wa nguvu za kiume ni nini?

Kabla hatujaingia kujadili sababu za kupungua nguvu za kiume, ni muhimu kwanza tufahamu maana ya kupungua nguvu za kiume. Ni kwa nini lazima tufahamu? Ni kwa sababu watu wengi wamekuwa wakielewa kimakosa maana ya kupungua nguvu za kiume.

Mara nyingi, ninapokuwa ninafanya mahojiano na wagonjwa katika kliniki yangu, mgonjwa anaweza kusema, “Mimi sina upungufu wa nguvu za kiume, isipokuwa nawahi tu kufika kileleni mapema sana!” Au “Mimi sina upungufu wa nguvu za kiume isipokuwa nikimaliza tu ‘round’ ya kwanza siwezi kurudia tena.”  Au “Mimi sina upungufu wa nguvu za kiume isipokuwa tu nakosa hamu ya tendo la ndoa!” Orodha ni ndefu!

Hii inaonesha watu hawa hawafahamu maana ya kupungua nguvu za kiume na hii ni moja ya mambo  yanayowasababishia waendelee kuteseka zaidi. Kwa uelewa huo wa kimakosa, watakuwa wanaacha kushughulikia tatizo na hivyo kusababisha liwe kubwa zaidi.

Upungufu wa nguvu za kiume ni sentensi ya jumla yenye kujumuisha vipengele vingi ndani yake. Kuwahi kufika kileleni; kuwahi kufika kileleni ni upungufu wa nguvu za kiume. Hiki ndicho kilio cha wanaume wengi katika zama hizi za leo.

 

Hii ni hali ya kufika kileleni ambayo hutokea kabla hata ya kuingia ukeni au muda mfupi tu baada ya uume kuingia ukeni, na hivyo wote wawili — mume na mke — kubaki bila kuridhika huku mwanamke akibaki akiteseka zaidi.

 

Inaendelea wiki ijayo


 

1855 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!