Tupande miti kukuza uchumi wetu (4)

Kuna umuhimu mkubwa sana kwa sekta binafsi kupitia kampuni mbalimbali au mtu mmoja mmoja, ikiwamo wananchi walio wengi vijijini kujiwekea mipango na malengo mazuri na kuweza kupanda miti kwa wingi. Kuna mahitaji makubwa ya mazao ya misitu — nguzo, mbao, kuni na mkaa. Endelea…

 

Napenda kuchukua fursa hii kuwafahamisha Watanzania walio vijijini na mijini kwamba misitu ya asili katika maeneo mbalimbali nchini imeharibiwa mno (highly degraded). Isitoshe, bado kasi ya uharibifu wa misitu ya asili ni kubwa kuliko unavyodhania maana matumizi ya mashine za moto (power or chain saws) yameongezeka sana.

Kinachosababisha misitu ya asili kuharibika sana ni kutokana na shughuli za kibinadamu. Kwa mfano, kufyekwa kwa shughuli za kilimo, ufugaji na kukata aina mbalimbali za miti kwa wingi kwa ajili ya mbao, nguzo, kuni na mkaa.

Usimamizi na udhibiti wa shughuli za binadamu katika misitu na mapori umekuwa mdogo sana kiasi cha kusababisha hali ya misitu kutoridhisha na kutoweka kwa kasi sana. Hali ilivyo kwa upande wa mazingira si nzuri maana maeneo mengi ya misitu ya asili yameharibiwa mno kiasi cha kuhatarisha uhai wa viumbehai wengine kama wanyama, ndege na wadudu mbalimbali. Ili kukabiliana na hali hiyo ya ongezeko kubwa la matumizi ya rasilimali misitu, na athari zake kubwa kwa mazingira ni muhimu kwa Watanzania wengi wakapanda miti kwa wingi.

Kuna umuhimu mkubwa sana kwa sekta binafsi kupitia kampuni mbalimbali au mtu mmoja mmoja, ikiwamo wananchi walio wengi vijijini kujiwekea mipango na malengo mazuri na kuweza kupanda miti kwa wingi. Kuna mahitaji makubwa ya mazao ya misitu — nguzo, mbao, kuni na mkaa.

Vilevile, misitu/miti ni muhimu mno katika kuboresha hali ya hewa kutokana na uwezo wake wa kunyonya na kuondoa gesiukaa (carbon dioxide-Co2) kutoka angani, na hivyo kusaidia kupunguza ongezeko la joto duniani.

Eneo lenye misitu ya kutosha au miti mingi linakuwa na mandhari nzuri mno ikiwamo hali ya hewa safi kuwa na gesi ya oksijeni (oxygen-O2) kwa wingi na mazingira yanayovutia (micro-climate) kwa binadamu kuishi vizuri.    Misitu na miti pia husaidia kupunguza kasi ya upepo, kuboresha upatikanaji wa mvua na kuhifadhi wanyamapori (makazi ya wanyama), hivyo kuweza kuvutia watalii.

Pamoja na masuala mengine, madhumuni ya makala haya ni kutaka kuwahamasisha na kuwatia moyo ili watu wengi Tanzania Bara wapande miti kwa wingi. Nimeona ni vema kufanya hivyo kwa sababu kuu nne:

(i) Kwanza, kasi ya kutoweka misitu ya asili ni kubwa.  Kila mwaka tunapoteza hekta takriban 500,000 za misitu ya asili kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zisizoendelevu, kama nilivyoainisha katika aya zilizotangulia katika makala haya.

Hii inadhihirisha kuwa kuna mahitaji makubwa ya mazao ya misitu kuliko uwezo uliopo. Takwimu zilizotolewa na mradi wa kupima misitu ya asili na mashamba ya miti pamoja na miti mingine nje ya misitu (trees outside the forests-ToF) katika Tanzania Bara (National Forest Resources Management & Assessment-NAFORMA) zinaonesha kuwa kuna upungufu wa meta za ujazo zipatazo 22 milioni.

Hiki ni kiasi kikubwa cha mahitaji ya bidhaa za misitu na kama juhudi za kufidia pengo hilo hazitafanyika kwa haraka, hali ya misitu yetu itaendelea kuwa mbaya. Matumizi makubwa ya bidhaa za misitu hasa kutoka kwenye misitu ya asili bila kupanda miti mingi kila mwaka, yanaifanya Tanzania Bara kuelekea kwenye hali ya kugeuka jangwa.

Je, tunakubaliana na hali hiyo kwamba sehemu kubwa ya Tanzania Bara igeuzwe jangwa kutokana na matumizi ya rasilimali misitu ya asili kwa njia zisizo endelevu? Niwaombe Watanzania wenzangu tusikubali hali hiyo itokee, na tuchuke hatua madhubuti kuzuia uharibifu wa misitu ya asili tuliyozawadiwa na Mwenyezi Mungu, (muumba wa mbingu na dunia)  ili zawadi hiyo iendelee kutunufaisha sisi wa kizazi cha sasa na vizazi vitakavyofuata.

(ii) Hali ya mazingira Tanzania Bara inazidi kuwa mbaya kwa sababu wapo Watanzania wachache ambao hawajali maslahi ya wengi ila kuziangalia tu nafsi zao kwa nia ya kutajirika haraka. Watu wenye mwelekeo kama huo hawaoni aibu hata kama nchi ikigeuka jangwa kwao si tatizo, ilimradi wamefanikisha azma yao.

Watu wenye fikra kama hizo ni hatari sana kwa uhai na maendeleo endelevu ya Taifa letu. Wakati mwingine inawezekana likawa kundi dogo lakini lenye nguvu sana kifedha (economically powerful elite group).

Pamoja na kuwa na nguvu kiuchumi, bado wanataka wajaze zaidi mifuko yao na kujirundikia mali hata kama mazingira yanaharibika kiasi cha kugeuza nchi kuwa jangwa; hilo kwao si hoja bali suala la msingi kwa mtazamo wao ni jinsi ya kupata fedha zaidi. Inabidi kupambana na kundi kama hilo bila kukata tamaa mpaka ushindi upatikane;

(iii) Watanzania walio wengi hawafahamu kuwa misitu au miti inaweza kuwa chanzo kizuri kwa mapato ya familia na kampuni binafsi na hata Serikali. Mfano mzuri ni miti ambayo inavumwa kutoka kwenye mashamba ya miti kuwa ni chanzo kizuri kwa mapato serikalini.

Hebu tuangalie hali ilivyo kwa shamba la miti la Sao Hill, lililopo katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa. Je, Serikali inanufaika vipi? Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii ilianza kuotesha miti miaka ya 1950 na kuanzia wakati huo hadi mwanzoni mwa miaka 1970 upandaji ulikuwa ukifanyika kwa kiwango kidogo sana.

Upandaji ulifanyika kwa kiwango kizuri kati ya 1974 na 1985 na kuweza kufikia hekta 30,000 kwa kipindi hicho. Hii ni sawa na kupanda karibu hekta 2,000 za miti kwa mwaka. Kiasi hicho kilifikiwa kwa kutumia mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni tano kutoka Benki ya Dunia. Hii ni karibu dola za Marekani 170 kwa hekta moja au karibu shilingi laki tatu kwa hekta moja.

(iv) Hadi kufikia mwishoni mwa 2012, karibu hekta 45,000 za miti zilikuwa zimepandwa: ikiwa ni karibu nusu ya eneo la mashamba yote ya miti nchini.  Miti iliyopandwa Sao Hill iko katika uwiano ufuatao: Miti laini (softwoods) ni Pinus patula (60%); P. elliotii (10%); P. caribbea (5%); P. oocarpa (2) na Cupressus lusitanica (2%).

Miti migumu (hardwoods) ni aina ya mikalatusi hasa Eucalyptus gradis na E. saligna ambayo kwa pamoja inachangia asilimia ishirini (20%). Asilimia moja (1%) ni aina mbalimbali za miti kwa ajili ya utafiti (majaribio) unaofanywa na Shirika la Utafiti wa Misitu (Tanzania Forestry Research Institute (TAFORI).

Kwa kipindi cha miaka 4-5 iliyopita, uvunaji umekuwa ukifanyika katika hekta 2,000 kwa mwaka na sasa Serikali inapata si chini ya shilingi 20 bilioni. Wakati huo huo watu binafsi wanaovuna miti wananufaika wanapouza mbao na TRA kuweza kupata VAT isiyopungua shillingi bilioni moja na nusu.

Miti inavunwa baada ya kufikia umri wa miaka 25 (uvunaji wa mwisho-final crop). Hata hivyo, kuanzia miaka 10 miti huwa inapunguzwa kutoka wastani wa miti 1,600 kwa hekta moja (inapopandwa) hadi kufikia wastani wa miti kati ya 300 mpaka 600 kwa hekta moja wakati wa kuvunwa (final crop) kulingana na aina ya miti kama ni ya “mi-pine”, “mi-cyprus” au mikalatusi.

Upunguzaji hufanyika kila baada ya miaka minne na huanza miti inapofikisha miaka kumi tangu kupandwa. Kitaaluma tunapunguza idadi ya miti ili kuwezesha miti mizuri kukua ipasavyo. Vilevile, ili miti iweze kuwa na thamani nzuri, hupogolewa matawi na upogoaji hufanyika kuanzia miaka minne hadi sita kulingana na jinsi ukuaji wa miti ulivyo.

Upogoaji wa kwanza ni muhimu sana ili kuwezesha mtu kupita katika miti kirahisi (access pruning) ili kuweza kuihudumia kirahisi, mfano, kukitokea moto kuweza kuuzima haraka kabla haujaleta madhara makubwa.

Miti inayopunguzwa kuanzia miaka kumi huweza kuuzwa na inaweza kuwa mwanzo wa mkulima kuanza kunufaika kama itakavyoelezwa baadaye katika makala zijazo.

Hapa utaona kuwa kupanda miti si gharama za kutisha, na ni kujihakikishia kipato kizuri kwa miaka ya usoni. Pata eneo, panda miti sasa kwa faida ya baadaye — kwako binafsi na Taifa kwa jumla.

Itaendelea

Dk. Felician Kilahama ni Mwenyekiti wa Kamati ya Misitu, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO).


 

2111 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!