USHINDI iliyoupata Simba,Jana Jumapili wa mabao 4-0 dhidi ya Majimaji, umeifanya timu hiyo kujikita zaidi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kufikisha pointi 35.

Simba imepata ushindi huo kwa mabao mawili ya John Bocco aliyefunga dakika ya 16 na 26 pamoja na yale mawili ya Emmanuel Okwi dakika ya 53 na 68 na kuifanya timu hiyo kuwa pekee ambayo mpaka sasa haijafungwa hata mchezo mmoja msimu huu.

Awali ilikuwa ni Simba na Azam, lakini kipigo ilichopata Azam juzi Jumamosi dhidi ya Yanga, kimeifanya Simba kuwa pekee ikishikilia rekodi hiyo baada ya kucheza mechi 15, imeshinda kumi na sare tano.

Huu ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Mfaransa, Pierre Lechantre, kukaa katika benchi la Simba ikiwa ni siku chache tangu asaini mkataba wa kuwa kocha mkuu akichukua mikoba ya Mcameroon, Joseph Omog.

Kwa ushindi huo, Simba inaendelea kukaa kileleni, huku Azam ikishika nafasi ya pili ikiwa na pointi 30, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 28.

3067 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!