Kama hamfahamu, Mpita Njia, maarufu kama MN ni mtumiaji mzuri wa usafiri uendao haraka (mwendokasi) mara kwa mara anapokuwa katika Jiji la Dar es Salaam.

Kwa takriban miaka miwili ambayo amekuwa mtumiaji mzuri wa huduma ya usafiri huo amezishuhudia tabia nyingi za watumiaji wa usafiri husika.

Kama ukifanyika utafiti wa mabadiliko ya kitabia kwa watu wanaotumia usafiri huo, hakika kwa wakazi wa maeneo ya Mbezi na Kimara na wale wanaotumia usafiri huo kuanzia kituo cha Kivukoni na kituo cha Halmashauri ya Jiji, hakika utafiti huo utabaini mabadiliko makubwa ya kitabia kwa watumiaji wa usafiri huo.

MN awapo kituo cha mwendokasi cha Kimara Mwisho au kituo cha Kivukoni huwashuhudia watu ambao wamepoteza kujiamini na wasio na ustaarabu wowote wanapoona magari hayo yakifika vituoni.

Magari ya mwendokasi kwa kifupi ni machache, hayatoshi kukidhi idadi ya wasafiri wanaotaka kutumia usafiri huo kwa siku.

Kinachomshangaza MN ni tabia za wasafiri kuonekana wakihaha kugombania kuingia kwenye magari hayo yanapowasili vituoni hasa magari ambayo yameandikwa ‘Express’.

Magari hayo yanagombaniwa kweli kweli lakini jambo la kushangaza wanaoingia kwenye magari hayo hugeuka watemi na kuchukia kusikia wengine wakiwaomba wasogee ili na wao waingie.

MN huwashangaa abiria kujazana milangoni mwa magari hayo huku upande wa mbele ukionekana kuwa na wasafiri ambao wamesimama kwa raha mustarehe bila kubanwa.

Kinachomsikitisha MN ni pale anapojaribu kuwa muungwana na kuwaomba wasogee mbele ili nafasi ipatikane, wasafiri wengine waingie kwenye usafiri huo.

Kama si kuambulia matusi kutoka kwa wasafiri wenzake, basi ‘atakatwa’ jicho la dharau likimaanisha, “mbona huyu hajielewi.”

Tabia hii kwa kweli inaonyesha namna baadhi ya Watanzania walivyojaa chuki.

Kupendana ndiyo nguzo ya amani na maendeleo, tubebane kwa vichache tulivyonavyo, kama usafiri wa mwendokasi ni usafiri wa umma, wasafiri walio ndani ya usafiri huo acheni chuki kati yenu.

Sogezaneni ili wenzenu pia waingie kwenye usafiri huo, kutaka starehe katika usafiri huo wakati si magari yenu huo si uungwana.

By Jamhuri