MWENYEKITI wa Serikali ya Kijiji cha Mwikatsi wilayani Babati mkoani Manyara, Simon Lala (CHADEMA) ameshambuliwa na kujeruhiwa kwa mishale na mapanga na watu wasiojulikana kwa kile kilichodaiwa kuwa ni mgogoro wa ardhi.

 

 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Agustino Senga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa shambulio hilo limetokea jana Juni 18, 2018 katika Kitongoji cha Waloa wakati mwenyekiti huyo akiwa kazini pamoja na wajumbe wa Serikali ya Kijiji.

 

Kamanda Senga amesema kuwa Lala ameshambuliwa akitekeleza majukumu yake ambapo alikuwa akisimamia kesi ya ndugu wakigombea ardhi na ndipo upande wa walioshindwa hawakuridhishwa na matokeo ya Baraza la Kata.

“Tukio lilitokea mida ya saa 5:00 asubuhi wakati Mwenyekiti akiwa shambani akimuonesha mipaka ndugu wa watuhumiwa hao waliokimbia baada ya kutekeleza shambulio hilo, ambao walishindwa katika kesi ya kugombea ardhi lakini hawakuridhishwa na matokeo na kudai mwenyekiti amefanya upendeleo”, amesema Kamanda.

 

Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema amesema mwenyekiti huyo atahamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa matibabu zaidi baada ya kupewa rufaa katika Hospital ya Mkoa wa Manyara.

By Jamhuri