Huenda huu ukawa ndiyo mwisho wa Tanzania kuibwa rasilimali zake hususani madini, kutokana na Bunge kuingilia kati na kutaka kufahamu ni kwa namna gani nchi inanufaika na biashara ya madini.

Mwisho huu unatokana na Spika wa Bunge, Job Ndugai, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedith Kakoko, kuonesha wasiwasi juu ya makasha ya mchanga wa dhahabu yanayosafirishwa nje ya nchi kama kweli yanakuwa hayana dhahabu ya kutosha ndani yake.

Spika Ndugai alionesha wasiwasi wake huo Jumapili iliyopita, alipotembelea Bandari ya Dar es Salaam, kwa ziara maalumu akiwa na wajumbe wa kamati mbili za Bunge ambazo ni Kamati ya Bajeti na Kamati ya Nishati na Madini, ili kujionea makasha hayo yanayoshikiliwa na Bandari.

“Haiingii akilini kwamba kontena lenye mchanga wa uzito wa tani ishirini kutoa dhahabu kwa asilimia 0.02. Hivi kweli 0.02 ndiyo inayosababisha makasha haya kusafirishwa kutoka mgodini hadi hapa bandarini na hatimaye kusafirishwa kupelekwa nje ya nchi?Hata kwa mimi ambaye sikusomea mambo ya madini, hili siwezi kulielewa kabisa,” amesema Ndugai.

“Mmi pia nimeamua kuja ili kujionea badala ya kuziachia kamati peke yake ili tuweze kujua namna ya kuishauri Serikali. Kama mnavyofahamu kuwa sisi tunatunga sheria zikiwamo za madini. Tunaenda kuunda kamati itakayotupatia majibu namna biashara hii inavyoendeshwa. Tunataka kujua biashara ya madini kwa ujumla wake nani ananufaika hasa!” amesema Ndugai.

Wakati Spika wa Bunge akionesha wasiwasi huo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Kakoko, ametofautiana na takwimu za kiwango cha dhahabu inayosadikiwa kuwamo katika makasha yanayosafirishwa nje ya nchi kwa ajili ya kupembuliwa upya.

“Mheshimiwa Spika, kwenye huu mchanga hakuwezi kuwa na dhahabu ya kiwango kidogo kiasi hicho. Humu kuna dhahabu ambayo inaweza kuwa ya asilimia kubwa. Kuna ulazima wa kujiridhisha zaidi na mimi kwa uzoefu wa utaalamu wangu hili haliingii akilini,” amesema Kakoko.

Kakoko amemweleza Spika kuwa hadi sasa makasha yanayoshikiliwa bandarini hapo kwa ajili ya uchunguzi zaidi ni 282.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA), Gilay Shamika, amesema kuwa kazi ya uchenjuaji imekuwa ikihusisha pande tatu ambazo ni mgodi, TMAA na kule makasha yanakopelekwa baada ya uchenjuaji wa ndani.

“Pande zote hizi zimekuwa zikitoa matokeo ya uchenjuaji ambayo mara nyingi yamekuwa yakishabihiana. Katika makasha haya dhahabu imekuwa ikionekana kwa asilimia ya 0.02, fedha kwa asilimia 0.02 na shaba kwa asilimia kati ya 17 na 20. Hata hivyo, sisi tumekuwa tukiweka ‘serial number’ kule kule mgodini ili kuepuka udanganyifu,” amesema Shamika.

Ameeleza kuwa makasha yamekuwa yakisafirishwa kwenda nje ya nchi tangu mwaka 1998 na kwamba kila mwaka yamekuwa yakisafirishwa makasha kati ya 55,000 na 60,000. Hata hivyo, ameeleza kuwa Tanzania haina mwakilishi wa kuhakiki kiasi cha dhahabu kinachopatikana katika makasha hayo huko yanakosafirishwa.

Hata hivyo, alipoulizwa na Spika Ndugai kuwa TMAA ina uhakika gani iwapo takwimu hizo za viwango vya madini katika mchanga huo hutumwa kutoka kwa kampuni hizo na si watu hukaa na kubuni tu, Shamika alijibu kuwa Mamlaka haina uhakika kwa kuwa haina mwakilishi huko.

Shamika alimueleza Spika kuwa makasha hayo yamekuwa yakisafirishwa kwenda nchi za Japan na China kwa ajili ya kuchanjuliwa.

Itakumbukwa kuwa Machi 23, mwaka huu, Rais John Magufuli, alifanya ziara ya kujionea utekelezaji wa maagizo yake kwa Mamlaka hiyo juu ya mfumo wake wa utendaji kazi.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli alishuhudia makasha 20 yenye mchanga wa madini kutoka katika migodi ya uchimbaji wa madini ya dhahabu hapa nchini. Hata hivyo, Machi 2 mwaka huu, Rais Magufuli alipiga marufuku usafirishwaji wa mchanga wa madini nje ya nchi na kutaka ufanyiwe uchenjuaji hapa hapa nchini.

Baada ya kuyaona makasha hayo, Rais Magufuli alimuagiza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga wa madini unashikiliwa popote ulipo hadi uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini aina na asilimia ya madini inayopatikana katika mchanga huo.

By Jamhuri