Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imesisitiza kuwa mwisho wa zoezi la kusajili laini za simu kwa kutumia alama za vidole ni Desemba 31, mwaka huu.

Msisitizo huo unatokana na kuwepo kwa taarifa kwamba serikali kupitia Waziri wa Mambo ya Ndani amewataka  wananchi wasiwe na hofu ya kuzimiwa simu baada ya Desemba 31.

Akizungumza na JAMHURI, Ofisa Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Semu Mwakyanjala, amesema wananchi wanapaswa kuelewa kuwa tarehe ya mwisho ya usajili wa laini za simu haijabadilika.

Amewataka wananchi kuendelea kusajili laini zao za simu kwa haraka ili kuepuka usumbufu zoezi litakapofikia mwisho wake.

“Mwanzo wa zoezi hili mwitikio wa watu ulikuwa unasuasua lakini kwa sasa idadi ya watu wanaokuja kusajili inaongezeka,” amesema.

Amebainisha kuwa hadi Oktoba mwaka huu idadi ya watu waliokuwa wamesajili laini zao kwa kutumia alama za vidole ilikuwa imefikia watu milioni 13 na mwezi Novemba idadi hiyo iliongezeka kwa watu takriban milioni 3.9.

Amesema idadi ya watu ambao wamekwisha kujisajili mpaka sasa imefikia 16,904,421, hali inayoonyesha kuwa zoezi limekuwa endelevu na mwitikio wa watu kuzidi kuwa mkubwa.

Aidha, amedokeza kuwa kuanzia wiki hii maofisa wa TCRA, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kampuni za simu za mikononi watafanya ziara vijijini ili kuwahamasisha watu kusajili laini zao za simu kwa kutumia alama za vidole.

Alibainisha kuwa kusajili laini kwa alama za vidole kunalenga kudhibiti na kubaini wizi katika mitandao, pia kutaka kurahisisha kazi katika suala la malipo mbalimbali na miamala ya fedha kupitia simu za viganjani.

Mwakyanjala ametoa angalizo kuwa usajili wa laini za simu ni bure na yeyote atakayetozwa gharama kwenye usajili wa laini atoe taarifa TCRA, NIDA na kampuni za simu ili sheria ichukue mkondo wake. 

By Jamhuri