Home Kitaifa Ofisa Afya alia na Tume ya Utumishi

Ofisa Afya alia na Tume ya Utumishi

by Jamhuri

Ofisa Afya mstaafu, Joseph Ndimugwanko, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Buhororo wilayani Ngara anailalamikia Tume ya Utumishi wa Umma kwa madai ya kutomtendea haki katika rufaa yake ya Agosti 20, 2014 ya kupinga kufukuzwa kazi.

Ndimugwanko alifukuzwa kazi Julai 30, 2014 na Mkurugenzi wa Wilaya ya Ngara kwa madai ya utovu wa nidhamu.

Hata hivyo, akizungumza na JAMHURI, Ndimugwanko anadai kuwa mchakato wa kumfukuza kazi haukuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 ya mwaka 2002, pamoja na Kanuni ya 60 (2) ya Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2003, pamoja na tangazo la Serikali Na. 42 la Februari 16, 2007.

Katika rufani yake, Ndimugwanko aliieleza tume kuwa ofisi ya mkurugenzi ilimfukuza kazi pasipo kuzingatia Kifungu Na. 13 cha tangazo la Serikali la mwaka 2007, kitendo kilichomnyima haki ya kuhoji na kuhojiwa kwa njia ya mdomo kwenye kikao cha kumfukuza kazi, ikiwa ni pamoja na kukosa haki ya kujieleza na kujitetea mbele ya kikao hicho.

Ameeleza kuwa asili ya kufukuzwa kazi kwake ni tuhuma za kupokea rushwa ya Sh 20,000 iliyomfikisha Mahakama ya Wilaya  ambako alikutwa na hatia na kulipa faini.

Hata hivyo, Ndimugwanko anadai kuwa tuhuma hizo zilitengenezwa na askari wa TAKUKURU wakimshirikisha kijana aliyemtaja kwa jina la Imani Karisa, mkazi wa Nyamiaga wilayani humo, ambaye alitumiwa kumpatia fedha za rushwa.

Akifafanua, amesema siku ya tukio alikuwa anarejea nyumbani kutoka kazini na njiani alisimamishwa na kijana huyo ambaye alitoa noti mbili za Sh 10,000 kila moja na kumtaka azipokee kama shukrani kwake.

“Nilikataa lakini ghafla wakatokea askari wa TAKUKURU na kunikamata kwa tuhuma za kupokea rushwa,” anasimulia.

Amesema kabla ya hapo, aliingia kwenye mgogoro na aliyekuwa Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Mathias Mwangu, baada ya yeye kufunga klabu ya pombe kwa kutokuwa na choo lakini mkurugenzi huyo akamuamuru akifungulie.

“Badala ya kukifungulia klabu hicho kama mkurugenzi alivyotaka, mimi nilimpeleka mahakamani mmiliki wake, Imani Milenzo, mkazi wa Nyamiaga, kwa sababu alikuwa amevunja sheria. Hapa ndipo mgogoro na mkurugenzi ulipoanza,” amesema.

Ndimugwanko amesema mkurugenzi alipomtaka kukifungulia klabu hicho, alimtaka mkurugenzi amuandikie barua ili atengue uamuzi wake kimaandishi.

“Mimi ni mtu wa msimamo, niligoma kutekeleza agizo la mkurugenzi. Nilimueleza kuwa nimetekeleza hatua za kufunga klabu hicho kwa kuzingatia Sheria ya Afya, hivyo sifanyi kazi kwa vitisho,” amesema.

Amesema baada ya mfanyabiashara huyo kutiwa hatiani na vitisho vya mkurugenzi kuendelea, aliandika barua na nakala akazisambaza kwa viongozi ngazi ya wilaya, mkoa hadi kwa Waziri Mkuu wa kipindi hicho, Mizengo Pinda.

“Baada ya kupokea barua yangu ya malalamiko Ofisi ya Waziri Mkuu ilimwandikia barua Mkuu wa Mkoa wa Kagera ikimuelekeza kushughulikia suala langu. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ilimtaka mkurugenzi kujieleza kwa nini ananitishia maisha na kunizuia kutekeleza majukumu ya kazi yangu,” amesema Ndimungwanko.

Amesema baada ya muda mfupi mkurugenzi huyo alihamishwa na kuletwa mkurugenzi mpya aliyefahamika kwa jina la Coronel Ngudungi, ambaye aliendeleza mgogoro huo.

Amedai kuwa kwa kushirikiana na TAKUKURU, mkurugenzi huyo mpya ndio waliandaa mpango wa kumshikisha rushwa, tukio ambalo lilitokea Oktoba, 2013.

Amedai ilifanywa njama na TAKUKURU kwa kutoa ushahidi wa uongo mahakamani kwa kuleta maelezo ambayo hayakuwa yake, hivyo yeye kutiwa hatiani na kulipa faini ya Sh 500,000.

Amesema baada ya kesi hiyo alirudi kuripoti kazini lakini alishangaa kupatiwa barua ya tuhuma za utovu wa nidhamu ikimtaka kujieleza ndani ya siku 14.

Aliijibu barua hiyo ndani ya siku tatu na kwamba baada ya wiki moja alipokea barua yenye kumb. Na. NGR.HW/C/S.16/41 ikieleza kuwa amefukuzwa kazi.

Amesema barua hiyo ilinukuu Kanuni Na. 48(6) chini ya Tangazo la Serikali Na. 168 ya Utumishi wa Umma ambayo haihusiki kabisa na kumfukuza kazi mtumishi.

“Mkurugenzi hakuzingatia kifungu hicho Na. 48(6) wakati anatekeleza azima ya kunifukuza, alisahau kuwa Kanuni Na. 48(9) inaeleza kuwa endapo kanuni Na. 48(6) haikutekelezwa mtuhumiwa mtumishi wa umma anakuwa hana hatia,” amesema Ndimugwanko.

Baada ya kubaini upungufu huo, aliamua kukata rufani wizarani lakini maombi yake hayakushughulikiwa ipasavyo, kwani mkurugenzi alipeleka nyaraka tofauti na zile zilizotumika kumfukuza kazi.

Hivi sasa Ndimugwanko anafanya jitihada za kuonana na Rais John Magufuli ili amfikishie kilio chake baada ya kukwama katika maeleo yote ambako amekwenda.

Msemaji wa Wizara ya Utumishi wa Umma, Richard Cheyo, amelitaka JAMHURI kumpelekea nyaraka za Ndimugwanko ili aweze kuzitolea ufafanuzi.

You may also like