Home Kitaifa Msafara wa Magufuli una mambo mengi

Msafara wa Magufuli una mambo mengi

by Jamhuri

Usidhani kuwa Rais John Magufuli anapopanga kutembelea eneo fulani katika ziara zake wanaohusika katika misafara yake ni viongozi wa serikali pekee. 

Wakati maofisa wakiandaa safari hizo, wapo watu wengine kwa mamia ambao nao hujiandaa kwenda katika ziara hizo kwa malengo tofauti.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, watu wengi nao hujiandaa kusafiri pindi wanaposikia taarifa kuwa Rais Magufuli amepanga kutembelea eneo fulani. 

Hawa ni watu wenye shida mbalimbali walizoshindwa kuzipatia ufumbuzi katika mifumo ya kawaida na kubakiza tumaini lao pekee kwa Rais Magufuli.

“Ni kweli, nimepanga safari kuelekea kwenye ziara za Rais Magufuli mara tatu, moja nilikwenda alipotembelea machinjo ya Vingunguti jijini Dar es Salaam, kisha nikafunga safari alipokwenda mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, pia nilikuwepo Lindi hadi Ruangwa alipotembelea mikoa ya Lindi na Mtwara. Lengo langu kubwa lilikuwa ni kwenda kufikisha kilio changu kwa rais kutokana na viongozi katika ngazi nyingine kushindwa kunisaidia,” ameeleza Thomas Njama, kachero mstaafu ambaye tangu mwaka 2015 amekuwa akihangaika kudai mafao yake ya kustaafu bila mafanikio.

Akifafanua, amesema aliamua kumfuata rais kwenye ziara zake kwa sababu kuna ugumu mkubwa kumfikia kiongozi huyo mkuu wa nchi kwa kufuata mchakato maalumu uliopo.

“Inakuwa rahisi kumfikia rais na kutoa kilio katika mikutano yake ya hadhara,” amesema.

Njama amesema alianza kuzifuata ziara za Rais Magufuli wakati alipofanya ziara kwenye mradi wa machinjio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam mwezi Agosti mwaka huu, lakini hakufanikiwa kumuona ili amueleze anavyohangaika kupata mafao yake ya kustaafu.

Hata hivyo, amesema Septemba 4, alipata taarifa kuwa rais anakwenda ziarani mkoani Songwe, napo aliamua kusafiri kuifuata ziara hiyo hadi Songwe.

Akiwa Songwe kwenye mkutano wa hadhara wa Rais Magufuli na wananchi wa mkoa huo, amesema kuna mama alipewa nafasi ya kueleza kero zake naye akataka kutumia mwanya huo kujipenyeza ili aeleze shida yake mbele ya rais lakini kwa bahati mbaya alidhibitiwa na walinzi na kushindwa kufikisha kilio.

“Wakati walinzi wananizuia nisipite kwenda mbele kumuona rais, nilipoteza nyaraka nilizokuwa nazo, hata pesa niliyokuwa nayo kwa ajili ya nauli na kujikimu ilidondoka, ilibidi niuze viatu nilivyovivaa ili nipate pesa ya kula na nauli ya kurudi Dar es Salaam,” amesema Njama.

Hata hivyo, amesema hakukata tama, alianza safari tena kuelekea Tunduma ambako alielezwa kuwa Rais Magufuli atakuwa na ziara lakini katika ziara hiyo hakufanikiwa kumuona wala kupewa nafasi ya kueleza kero zake.

Lakini hilo halikumkatisha tama, kwani aliposikia rais ataelekea Lindi kwenye sherehe za kilele cha Mwenge wa Uhuru, naye akafunga virago kuelekea huko akiwa na imani kuwa atafanikiwa kumuona rais na kufikisha kilio chake.

“Nilipofika Lindi, kutokana na protocol (itifaki) katika sherehe za Mwenge nilishindwa kumuona rais lakini siku ya pili nilisafiri hadi Ruangwa ambako alikuwa na mikutano ya hadhara,” amesema na kuongeza:

“Lakini nako nikakosa nafasi ya kumuona. Baada ya kukosa nafasi ya kumuona rais akiwa Ruangwa nilijiandaa kwenda Nachingwea alikokuwa anaelekea siku iliyofuata, lakini niliishiwa nauli nikashindwa kumfuata rais kwenye mkutano wa Nachingwea.” 

Naye, Ramadhani Hussein, mkazi wa Katavi ambaye amewahi kusafiri kutoka Katavi kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kumuona Rais John Magufuli, anasimulia kuwa baada ya kusingiziwa kesi ya ubakaji mwaka 2007 alihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela lakini alikaa jela kwa miaka 11 na kwamba baada ya kuachiwa alijikuta amepoteza mali zake zote.

Katika kuhangaikia haki yake iliyopotea, amesema aliwahi kupata mtu aliyejitambulisha kuwa karibu na familia ya rais aliyempa tumaini kwamba atamsaidia kufikisha kilio chake mbele ya rais.

“Mwezi Agosti mwaka huu, huyu mtu alinipigia simu nije Dar es Salaam kumuona rais, kwamba amekubali nionane naye, nilisafiri hadi Ikulu lakini nilizuiliwa na walinzi,” amesema Hussein.

Hata hivyo, baada ya kuhojiwa na walinzi wa Ikulu ilibainika kuwa Hussein alikuwa amedanganywa na matapeli wa mtandaoni, kwa sababu tukio hilo limefunguliwa jalada la uchunguzi Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam. 

Pia kuna kundi la wakazi wa Kijiji cha Butiama, mkoani Mara ambao nao walifunga safari hadi Dar es Salaam kwa lengo la kumuona Rais Magufuli awasaidie baada ya kudhulumiwa ardhi yao.

Wakizungumza katika ofisi za JAMHURI hivi karibuni, kina mama hao wa Butiama wamesema kuwa wanaamini kuwa wakimuona rais atawasaidia kupata ufumbuzi wa suala lao.

You may also like