Home Kitaifa Kukosa umoja chanzo miradi mibovu ya maji

Kukosa umoja chanzo miradi mibovu ya maji

by Jamhuri

Hali ya miradi ya maji inayozinduliwa nchini mingi kutotoa maji ipasavyo inaelezwa kuchangiwa na mipango mibovu pamoja na ushirikiano hafifu baina ya wataalamu, hasa wahandisi wakati wa utekelezaji.

Hayo yamebainishwa na Msajili wa Bodi ya Wahandisi nchini (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, wakati wa uzinduzi wa kongamano la kujengea uwezo wahandisi lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema tatizo hilo linawajumuisha wataalamu wenye taaluma mbalimbali, hivyo lawama haziwezi kuelekezwa kwa mtu mmoja mmoja.

“Hatuwezi kusema kuwa mhandisi ndiye ameharibu mradi, kwani mipango inaweza kuharibika kuanzia kwenye bajeti yenyewe ya kutekeleza mradi,” amesema Mhandisi Barozi.

Amesisitiza kuwa wahandisi wana jukumu la kuhakikisha taaluma yao inaheshimika kwa kufanya kazi kwa weledi ili wajitofautishe na watu wasio wahandisi. Amebainisha kuwa kwa bahati mbaya wapo baadhi yao ambao wanatumia cheo hicho kwa masilahi binafsi.

Akifungua kongamano, Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, amesema kuanzia sasa wahandisi ambao watatambulika na kupata kazi kutoka serikalini ni wale watakaokuwa wameajiriwa rasmi na bodi na kupewa leseni za uhandisi.

Amesema hilo ni kwa mujibu wa sheria Na. 15 ya mwaka 1997, ambayo inafafanua kuwa mhandisi lazima awe amepitia masomo ya kihandisi katika chuo kinachotambuliwa na serikali.

“Si kila mtu anaweza kuwa mhandisi. Haiwezekani mtu anasoma miaka mitatu hadi minne halafu mtu mwingine anabeba cheo cha uhandisi kirahisi wakati hajasomea,” amesema Mhandisi Nditiye.

Wakati akizindua kongamano hilo aliwataka wahandisi wote kujiamini, kwani serikali kwa sasa inawaamini wazawa kuliko wageni lakini ili waendelee kuaminika wanatakiwa kuonyesha ujuzi na taaluma zao kwa vitendo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wahandisi nchini, Mhandisi Ninatubu Lema, amesema umefika muda kwa wahandisi wazawa kutumiwa kwenye miradi inayoanzishwa nchini badala ya kutumia wageni.

“Tunaiomba serikali kupitia wizara zake na taasisi zake kuwa na utaratibu wa kisheria wa kuwachukua vijana (wahandisi) kuendelezwa katika miradi inayotekelezwa kwa sasa hapa nchini.

“Miradi iliyopo itumike kama miradi darasa kwa vijana wahandisi tulio nao kwa sasa,” amesema Mhandisi Lema.

You may also like