Home Kitaifa Serikali yatahadharishwa kuhusu gesi

Serikali yatahadharishwa kuhusu gesi

by Jamhuri

Serikali imetahadharishwa kuwa kucheleweshwa kwa makubaliano na wawekezaji katika mradi wa kiwanda cha kuchakata gesi asilia (LNG) kunaweza kuiingiza nchi kwenye hasara ya kutonufaika ipasavyo na rasilimali ya gesi asilia.

Hayo yamebainishwa na wataalamu wa masuala mbalimbali yanayohusiana na gesi na mafuta kupitia kitabu kilichochapishwa hivi karibuni.

Wataalamu hao walioandika kitabu hicho kinachoitwa ‘Governing Petroleum Resources: Prospects and Challenges for Tanzania’ (Uendeshaji wa Rasilimali za mafuta: Matarajio na Changamoto kwa Tanzania) wanabainisha kuwa ucheleweshaji wa makubaliano hayo unaweza kuisababisha Tanzania kutonufaika ipasavyo, kwani bei ya gesi asilia duniani imekuwa ikishuka tangu mwaka 2014.

“Upo uwezekano wa bei kupanda kwa sababu inabadilikabadilika lakini kama tukichukulia trend (mwenendo) ambayo imekuwepo tangu mwaka 2014, kuna uwezekano mkubwa bei ikazidi kushuka kwa sababu kuna sababu kadhaa zinazoonyesha hilo,” amesema Donald Mmari, Mkrugenzi Mtendaji wa REPOA na mtafiti wa masuala ya uchumi ambaye naye ameshiriki kuandika kitabu hicho.

Akizungumza na JAMHURI kutokea Dodoma ambako yuko kikazi, Mmari anaongeza: “Mathalani, kwa miaka mingi Marekani ilijizuia kuchimba mafuta na gesi kwa sababu za kimazingira lakini kiongozi wao wa sasa hajali sana masuala ya mazingira na Marekani imeanza kuwa msafirishaji nje wa gesi. Hapa jirani Msumbiji tayari wameshafikia makubaliano ya kuanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi kuwa kimiminika. Hatua hizo zote zinasababisha mbinyo kwenye soko, kwani bidhaa zitaongezeka, hivyo kuwepo uwezekano mkubwa wa bei kushuka.”

Kwa mujibu wa Mmari, ni vema serikali ikahakikisha inaharakisha mchakato wa kufikia makubaliano na wawekezaji hao wakati huu ambapo bei haijashuka sana ili faida ambayo nchi itaipata kutokana na mradi huo isiwe ya chini sana.

Hata hivyo amesisitiza kuwa hilo halimaanishi kuwa serikali iharakishe mchakato bila kuwa makini na kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika na rasilimali yake.

Wakizungumzia hali ya sasa katika kitabu hicho, watalaamu hao wamesema ipo haja ya kufanya marekebisho ya mfumo wa sheria kwa sababu yapo baadhi ya mambo yanayokwaza uendelezaji wa sekta ya mafuta na gesi nchini na kusababisha nchi kutonufaika ipasavyo.

Katika andiko ndani ya kitabu hcho lililoandikwa na Mmari, James Andilile, Odd-Helge Fjeldstad na  Aslak Orre, wanabainisha kuwa mfumo wa kisheria ni nguzo kuu ya kuhakikisha kuwa pande zote zinazohusika katika miradi ya gesi na mafuta zinanufaika.

Wanabainisha kuwa Tanzania, kama zilizvyo nchi nyingine zinazoendelea haina uwezo wa kuendeleza rasilimali yake ya gesi asilia kwa kuwa haina fedha, utaalamu na teknolojia ya kufanya hivyo wakati kampuni za kimataifa zina hivyo vyote lakini hazina rasilimali hiyo.

“Kwa maana hiyo mfumo wa kisheria unaofaa ni ule ambao utahakikisha kuwa pande hizi mbili zinanufaika na mifumo ya kisheria itakayoongoza sekta ya gesi na mafuta,” wanabainisha wataalamu hao.

Wanaonya kuwa mfumo wowote wa sheria ambao unalenga kuinufaisha serikali pekee utaleta matatizo kwa sababu utaifanya Tanzania isiwe shindani katika sekta hiyo, hivyo kuwalazimisha wawekezaji kuhamia sehemu nyingine ambako wanaamini watapata faida.

Wakitoa mfano, wataalamu hao wanabainisha mathalani kuwa chini ya sheria za sasa, waziri ndiye ana uhuru wa kupanga kiwango cha mrabaha na ana mamlaka ya kubadilisha kiwango hicho wakati wowote atakapoona inafaa.

“Hii inaweza kusababisha kutokuwepo uhakika kuhusiana na kaisi cha faida ambacho mwekezaji atapata katika mradi,” wanatahadharisha.

Pia wataalamu hao wanakosoa utaratibu mwingine uliowekwa na sheria kuipa Bunge mamlaka ya kuitisha mikataba na kuagiza yafanyike majadiliano upya baada ya mikataba hiyo kusainiwa.

Kwa upande mwingine, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, ni mmoja wa watu waliong’ara barani Afrika baada ya kutajwa miongoni mwa Waafrika 25 ambao wametikisa katika sekta ya mafuta na gesi kwa mwaka 2019 barani humo.

Dk. Kalemani kutokana na ahadi yake kwa niaba ya serikali kuwa itahakikisha kuwa makubaliano na wawekezaji katika mradi wa LNG yanafikiwa mwakani ili mchakato wa ujenzi wa kiwanda uanze mwaka 2022.

Mradi huo ambao gharama zake zinatajwa kuwa dola bilioni 30 utatekelezwa na kampuni kadhaa zikiwamo Equinor, Shell, ExxonMobil, Ophir Energy na Pavilion Energy.

Hata hivyo, mchakato wa ujenzi wa kiwanda hicho cha kuchakata gesi asilia katika Kijiji cha Likong’o mkoani Lindi umesimama kwa muda mrefu kutokana na serikali kushindwa kufikia makubaliano ya wawezekzaji hao kuhusiana na namna ya kugawana faida itakayotokana na mradi huo.

You may also like