Endelea na uchambuzi wa hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa kwa mwalimu mmoja mjini Bukoba baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kumuua mwanafunzi wake kwa kumchapa fimbo.

Dereva hulaumiwa kwa mwendo kasi baada ya ajali kutokea na huenda angelaumiwa kwa mwendo wa pole kama angeendesha hivyo na kuchelewa kufika. Aidha, huenda ni kawaida yake kuendesha kwa kasi na huwa akisifiwa kwa mwendo huo kabla ya kusababisha ajali.

Vyombo vya majini vinapopata ajali kinachosemekana zaidi ni vyombo hivyo kubeba kuliko uwezo wake. Mamlaka zinazosimamia vyombo hivyo hulaumiwa lakini lawama hizo hutolewa baada ya ajali kutokea. Binadamu hawajazwi kama magunia bila hiari yao. Ni dhahiri kabla ya kupanda chomboni, hata abiria mwenyewe huona ujazo wa chombo hicho lakini akaamua kukipanda. 

Akizuiwa kukipanda, huwalaumu wanaomzuia na huenda lawama hizo zisifutike moyoni mwake. Akiwa mwalimu wa nidhamu, mwalimu wa Kibeta aliyehukumiwa kwa kuua huenda angelaumiwa kutotoa adhabu inayotosha kurekebisha nidhamu za wanafunzi wake endapo kifo kisingetokea na huenda ameshawahi kulaumiwa.

MV Bukoba, meli iliyozama katika Ziwa Victoria mwaka 1996, ilipoondoka Bukoba kwenda Mwanza ilikuwa imejaza kuliko uwezo wake. Pamoja na ukweli huo, abiria waling’ang’ania kuipanda hata baada ya kuzuiwa kufanya hivyo. Baadhi yao walikodi magari kwenda kuiwahi katika Bandari ya Kemondo ilipokuwa ikipitia kabla ya kwenda Mwanza ambapo hapakuwa na vizuizi vikubwa vya kutosha kuwazuia kupanda meli hiyo kama vilivyokuwa Bukoba.

Walioachwa Bukoba baada ya kuzuiwa kupanda waliendelea kulalamika na kuwalaumu waliowazuia huku wakiwaombea dua mbaya hadi walipopata taarifa za kuzama kwa meli hiyo. Meli hiyo isingezama, huenda uhasama kati ya aliyezuiwa kupanda na aliyemzuia ungedumu hadi leo. Aliyeonekana shetani kabla ya meli kuzama alionekana malaika baada ya meli hiyo kuzama, na aliyeonekana malaika kabla akaonekana shetani.

Mama mmoja aliwahi kueleza jinsi alivyonusurika kwenye ajali ya moto wa petroli kama uliotokea hivi karibuni mkoani Morogoro. Gari la kusafirisha mafuta lilipopata ajali na watu kukimbilia kuchota mafuta yaliyokuwa yakimwagika, mama huyo naye alitaka kufanya hivyo lakini mtoto wake mkubwa alimzuia.

Wakiwa wanaendelea kuvutana, mtoto akimzuia mama na mama akitaka kwenda kuchota mafuta, moto ulilipuka na kusababisha vifo na majeruhi. Mwerevu kabla ya ajali akaonekana mjinga na mjinga kabla ya ajali akaonekana mwerevu.  Shetani akaonekana malaika na malaika akaonekana shetani. Ajali isingetokea mama angemlaumu mtoto na pengine lawama hizo zingedumu.

Mara kwa mara kinachoonekana kizuri kabla ya tukio huonekana kibaya baada ya tukio, na kinachoonekana kibaya kabla ya tukio huonekana kizuri baada ya tukio. Si haki kumlaumu mtu kwa kitendo kinachohusishwa na ubaya baada ya ubaya huo kutokea ambacho hakikuonekana kusababisha ubaya huo kabla ya kutokea, na kisingeonekana endapo ubaya huo usingetokea.

Ingawa nahodha na wahusika wengine wa usafiri wa majini katika Ziwa Victoria walihusishwa na vifo vilivyotokea baada ya MV Bukoba kuzama, ni vigumu kusema waliua hasa ikizingatiwa kuwa miongoni mwao wapo waliokufa pia na walionusurika kufa katika ajali hiyo hiyo waliyotuhumiwa kuisababisha.

Kilichotokea kabla na baada ya mwalimu huyo kumwadhibu mwanafunzi wake huenda kikahusishwa na kifo cha mwanafunzi huyo lakini ni vigumu kusema aliua, mbali ya kuua kwa makusudi kama alivyohukumiwa. Kabla ya kifo hakuna kilichoonyesha kuwa adhabu aliyopewa mwanafunzi ingesababisha kifo chake.

Ingawa kujaza kupita kiasi ndiyo sababu inayotajwa ya kuzama kwa MV Bukoba, ni dhahiri haikuwa sababu pekee. Kama ingekuwa sababu pekee, meli hiyo ingezama hapo hapo Bukoba au muda mfupi baada ya kuondoka Bukoba au Kemondo. Lazima kulikuwa na sababu nyingine ndiyo maana meli hiyo iliweza kusafiri hadi dakika chache kabla ya kufika Mwanza ndipo ikazama ikiwa imeshakaa na kusafiri majini zaidi ya saa tisa bila kuzama ikiwa na mzigo huo huo unaosemekana umezidi uwezo wake wa kubeba. Ingefika salama nani angelaumu kujazwa kwake kupita kiasi?

Mwenye kifafa akikutwa amekufa ndani ya mtaro huku akinuka pombe ni rahisi kuamini kuwa sababu ya kuanguka kwake na kufa ni ulevi. Ni dhahiri kilichomuangusha kinaweza kuwa kifafa na hata kusukumwa na mtu. Katika mazingira kama haya ni muhimu kuzingatia ukweli kwamba hata kinachoonekana wazi kuwa ni sababu huenda kisiwe sababu.

Kuna uwezekano mkubwa kinachosemekana kuwa ni sababu ya kifo cha mwanafunzi wa Kibeta aliyeadhibiwa na mwalimu wake kikawa si sababu licha ya kutokuwa sababu pekee. Hata taarifa ya daktari haikuonyesha wazi kuwa mwalimu huyo ndiye aliyesababisha kifo cha mwanafunzi wake. 

Alama za fimbo zinazosemekana mwanafunzi huyo alipigwa zilionekana kuwa si za siku hiyo aliyoadhibiwa na mwalimu wake. Kilichoitwa ukuni hakikuelezwa ukubwa wake. Inavyoelekea kiliitwa ukuni kutokana tu na matumizi yaliyokusudiwa wakati wa upatikanaji wake na hakina uhusiano wowote na hatari yake kikitumika kama fimbo, kama inavyoweza kudhaniwa na baadhi ya watu.

Kama ni vigumu kuthibitisha kuwa aliua, ni vigumu zaidi kuthibitisha kuwa aliua kwa makusudi. Kukusudia ni kuamua kufanya jambo kabla ya kulifanya, kujiandaa kulifanya na kuchukua hatua za kutosha za kuhakikisha kuwa linafanyika na kukamilika. Aidha, aliyekusudia hutarajia masilahi au kuepuka hasara baada ya kitendo anachokusudia kukamilika ingawa matarajio hayo yanaweza kuwa ya kweli au ya kufikirika.

Kabla ya kuamua, anayeamua huwa na sababu za kufanya hivyo. Kuhusu mwalimu aliyehukumiwa kwa kuua kwa makusudi, hakuna kiashiria chochote kinachoonyesha kuwa alikuwa na sababu za kumuua mwanafunzi wake. Kabla ya kifo cha mwanafunzi huyo, hakuna kisa kinachoonyesha mgogoro binafsi kati ya mwalimu huyo na marehemu wala wazazi au jamaa zake wa karibu.

Akiwa na umri wa miaka zaidi ya 50, alikuwa amekwisha kufundisha kwa muda mrefu na katika kipindi chote hicho hakuna kinachoashiria kuwa kwa tabia yake ni mtu mshari wa kuhatarisha maisha ya wengine. Aidha, aliaminiwa na kupewa dhamana ya kusimamia nidhamu ikiwa ni kiashiria cha yeye mwenyewe kuwa na nidhamu. Tukio la kumwadhibu marehemu liliingilia ratiba ya kawaida baada ya kutuhumiwa kuiba pochi. Aidha, aliadhibiwa mbele ya mwalimu mwingine na wanafunzi. 

Haiyumkiniki kuua kwa makusudi mbele ya watu wanaoweza kuingilia au kusababisha kuingilia  mchakato wa kuua usikamilike. Pamoja na ukweli huo, alikamilisha adhabu na kumwachia marehemu kabla hajafa bila mtu yeyote kuingilia kati. 

Katika hali hiyo ni dhahiri hakuchukua hatua za kukamilisha kitendo cha kuua, na kwa sababu hiyo hakukusudia kuua. Pamoja na ukweli huo, hakuna kinachoashiria masilahi halisi au ya kufikirika ambayo mwalimu huyo angepata au hasara halisi au ya kufikirika ambayo angeiepuka kwa kifo cha mwanafunzi wake huyo.

Kabla marehemu hajaadhibiwa, wakati wa kuadhibiwa na baada ya kuadhibiwa hadi kifo chake, hakuna hatua zilizochukuliwa za kumzuia mwalimu wake asitekeleze adhabu. Hakukamatwa wakati wa kutekeleza kitendo cha kumwadhibu au mara tu baada ya kukamilisha adhabu. Hali hii inaonyesha kuwa kifo ndicho kilichobadilisha mtazamo wa watu kuhusu adhabu iliyotolewa.  Katika mazingira haya, ni vigumu kusema mwalimu huyo aliyehukumiwa kunyongwa hadi kufa alisababisha kifo licha ya kuua. Ni dhahiri hakuua kwa makusudi.

Akiwa mwalimu wa nidhamu, kitendo cha kumwadhibu mwanafunzi ni kitendo cha kutekeleza majukumu yake. Matokeo tu ya kutekeleza majukumu hayapaswi kumtia mtu hatiani. Katika kutekeleza majukumu yake, daktari anaweza kusababisha kifo cha mgonjwa lakini hatuwezi kusema ameua. 

Katika kutekeleza majukumu yake, jaji anaweza kumhukumu mtu kwa makosa kunyongwa hadi kufa na mtu huyo akanyongwa. Hatuwezi kusema jaji aliua hata kama itathibitika baadaye kuwa marehemu aliyekufa kwa kutekelezwa kwa hukumu ya jaji huyo hakuwa na hatia.

HALIFA SHABANI

[email protected]

0783 705566

By Jamhuri