0767 311422

 

Ninaandika barua hii nikiamini kwamba endapo utaitilia maanani na ukauelewa ujumbe wake, utaepusha janga na maafa kwa nchi.

Usipoona umuhimu wake, kwangu si muhali, ninachojali ni kuufikisha ujumbe kwako na kwa Watanzania unaowatawala.

Nimelitafakari kwa umakini onyo lako dhidi ya waliokusudia kuandamana Aprili 26, mwaka huu.

Maandamano hayo yanahamasishwa kupitia mitandao ya kijamii. Maandalizi ya kuwapinga waandamanaji yanaonekana wazi wazi.

Rais Magufuli, umeonya ukisema watakaoandamana watakuona, kauli hiyo inaashiria umekusudia kuwadhibiti ipasavyo, kupitia vyombo vya dola. Umejiapiza kuwa “watakwenda kuwaeleza baba zao.”

Hayo siyo maneno ya amani bali ya Jemedari aliyejiandaa kupigana vita dhidi ya raia wake wasiokuwa na silaha, kwa sababu tu raia hao wanataka kusema yale asiyopenda kusikia.

Wanaoiombea Tanzania na wanaokuombea 

Watu wanaoiombea Tanzania wanafanya vyema, pia wapo wanaokuombea wewe Rais, pasipo kukueleza ukweli kuhusu utawala wako na misimamo yako.

Kwa sababu Mungu huwasikia wanaomsikiliza na huwakubalia hao wanaoyakubali maneno yake na kuyatii.

Upo mfano hai wa Mfalme wa kwanza wa Israeli, Sauli mwana wa Kishi. Mungu alimchagua kuwa Mfalme na sherehe ya kumsimika ilifanyika hadharani.

Lakini Mfalme Sauli alipoanza kutawala, alifanya makosa yanayofanana na makosa ya Marais wengi wa nyakati zetu.

Mfalme Sauli hakuwa msikivu. Hakukubali kushauriwa, bali alifanya yale ambayo akili yake ilimwaminisha kwamba ndio yanastahili kufanywa.

Mwenyezi Mungu akamwambia Nabii Samweli (aliyemsimika na kumtawaza Sauli awe Mfalme) “najuta kumchagua Sauli” (1Samweli 15:10-12).

Imeandikwa Samweli akamlilia Mungu usiku kucha, alipoamka alikwenda kumwona Mfalme Sauli uso kwa uso, akampa ukweli wote.

Hata hivyo, Mfalme aliendeleza utamaduni wa kufanya mambo kama atakavyo, badala ya kama inavyotakiwa. Ilifikia hatua Mungu akaishiwa uvumilivu, akamuuliza Nabii Samweli hata lini wewe utamlilia Sauli?

Nani anayefaa kuwa Mwalimu wako?

Inaeleweka duniani pote kwamba urais ni kazi ambayo wanaoipata hawasomei darasani. Kwa hiyo hakuna yeyote anayeweza kukufundisha jinsi ya kutawala wala kukuelekeza namna nzuri ya

kufanya kazi zako kama Rais.

Hakuna atakayekufundisha jinsi ya kutimiza majukumu yako ya kiutawala, kuanzia marais wastaafu waliowahi kuitawala Tanzania kabla yako, hadi wananchi wa kawaida.

Hakuna Rais wa nchi katika dunia anayeweza kuwa mwalimu wako mzuri wa kukufundisha a, b, c, d za urais, wala hakuna Rais wa nchi anayestahili kuwa mwalimu wa kukufundisha jinsi unavyoweza kuwa Rais bora.

Lakini kuna mwalimu mmoja tu anayekufaa, anaitwa Yesu. Atakufundisha somo muhimu liitwalo unyenyekevu wa moyo.

Kwenye injili ya Mathayo 11:28-29, Yesu amesema “njooni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kuelemewa na mizigo nami nitawapumzisha, jivikeni nira yangu mjifunze kutoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo na nira yangu ni laini.”

Yeyote anayetaka Mungu wa kweli alisikie dua lake na aweze kumpigania, anapaswa kulielewa vilivyo somo la unyenyekevu wa moyo.

Yeye asiyekuwa na huo unyenyekevu wa moyo anajidanganya mwenyewe, anaweza kukazana kumwomba Mungu kwa bidii, akidhani hiyo bidii yake katika kuomba na kusali itachangia kumsukuma Mungu amsikie na kumtendea hayo ayaombayo.

Wanaojidanganya kwa kumwomba Mungu kwa bidii pasipo unyenyekevu wa moyo ni wengi, kwenye waraka huu nitatoa mfano hai wa unyenyekevu wa moyo.

Maandamano ndani ya Biblia

Kwenye kitabu cha 1Samweli 8: 4-7 imeandikwa, “ndipo wazee wote wakakusanyika pamoja na kumwendea Samweli huko Rama, wakamwambia tazama wewe umekuwa mzee na wanao (uliowaweka kutimiza majukumu ya kiutawala) hawaenendi katika njia zako, wanakula rushwa na kupotosha hukumu.

Wanatafuta faida kwenye nafasi za utawala. Tunataka utufanyizie Mfalme atakayeamua kama ilivyo kwa mataifa mengine.” maneno yaliyo kwenye mabano ni yangu.

Ujumbe huo ambao wananchi walimpelekea Nabii Samweli kwenye makao yake yaliyoitwa Rama, ulikuwa mbaya mbele yake Samweli na Mungu.

Lakini imeandikwa, Mungu akamwambia Samweli “isikilize tu sauti ya watu hao na kila neno watakalokuambia, kwa maana hawakukukataa wewe bali wamenikataa mimi nisiwe mfalme juu yao.”

Uhalisia wa tukio hili ni kwamba watu walikusanyika pamoja na kuandamana hadi kwenye makao ya Nabii ili wamjulishe hisia zao.

Tafsiri halisi ya maandamano ni watu kujikusanya pamoja na kutembea kwa pamoja hadi hapo walipokusudia kuishia kwa lengo la kuelezea hisia zao.

Haijalishi hisia hizo kuwa halali ama kutokuwa halali zikipimwa kwenye mizania na vigezo au vipimo vya kibinaadamu.

Mwenyezi Mungu alijua hisia za waandamanaji kwamba ni mbaya, hata hivyo hakuwazuia wasiandamane wala hakuwahujumu kwa namna yoyote, ingawaje alikuwa na uwezo wote juu yao.

Mwenyezi Mungu hakuwazuia wala hakuwaadhibu, badala yake alimwagiza nabii awasikilize katika yote watakayomwambia.

Ingawaje maandamano yao yalikosa uhalali mbele ya Samweli na machoni pa Mungu mwenyewe, bado waandamanaji walisikilizwa na ujumbe wao ndio ulioifanya Israeli ipate ufalme.

Siku aliposimikwa huyo Mfalme Sauli, Nabii Samweli aliwaambia Waisraeli, “tazama nimeyasikia madai yenu mmempata Mfalme…”

“Kabla sijaondoka mnishuhudie mbele ya Mungu na mbele ya Mfalme wenu (masihi wake), nilitwaa ng’ombe wa nani ama kwa mkono wangu huu nilipokea rushwa kutoka kwa nani nami nitamrudishia. Semeni ukweli ni nani niliyemuonea nikatoa hukumu isiyokuwa ya haki?”

Watu walijibu kwamba hukuwahi kupokea rushwa wala hukutuonea, ndipo Samweli akasema kwa sasa ni wakati wa kiangazi, lakini nitamwomba Mungu alete mvua ili mjue kwamba dhambi yenu mliyofanya ya kujitakia mfalme ni mbaya sana.

Nabii Samweli akaomba, Mungu akapeleka ngurumo na mvua hadi watu wakamsihi Samweli wakisema, utuombee kwa Mungu wako tusije tukafa, kwakuwa tumetenda uovu kujitakia mfalme (1Samweli: 12).

Maandamano katika historia ya Tanzania

Novemba 1966, wasomi wa Chuo Kikuu eneo la Mlimani, wakishirikiana na wanafunzi waliokuwa kidato cha sita kutoka sekondari ya Kibaha, waliandamana hadi Ikulu.

Lengo lilikuwa ni kuelezea hisia zao kwa Rais wa wakati huo, Mwalimu Julius Nyerere (hayati). Walimweleza mambo kadhaa kuhusu utawala wake.

Miongoni mwa masuala waliyomweleza kwa uwazi ni kuhusu udikteta wake binafsi na udikteta wa chama kilichotawala (TANU).

Wasomi hao waliona kitendo cha kupelekwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakalitumikie Taifa kwa miezi sita na kukatwa mishahara yao pasipo kushirikishwa,

ilikuwa sawa na kuwaburuza, wakauita udikteta usiokubalika.

Mwandamanaji mmoja aliyeitwa Mkate, alibeba bango lililoandikwa “better were the colonial days” akimaanisha ni heri enzi za ukoloni, mambo yalikuwa mazuri.

Lingine ambalo mhutubiaji aliliweka wazi ni suala la utabaka na tofauti ya mapato kati ya wakubwa na wadogo, mhutubiaji amesema mbele ya Mwalimu Nyerere, “mishahara yenu (akimaanisha mishara ya watawala na wanasiasa) ni mikubwa mno punguzeni.”

Hayo yalikuwa maandamano ya kwanza dhidi ya utawala katika Tanzania huru, ikiwa ni miaka mitano tu tangu uondoke utawala wa kikoloni.

Matunda ya maandamano hayo yakaandika historia mpya katika nchi yetu, kwani ni hayo maandamano ya Novemba 1966 ndiyo yaliyozaa Azimio la Arusha mwaka 1967.

Mwalimu Nyerere hakuyazuia maandamano wala hakupuuza ujumbe wa waandamanaji, ingawa maneno “afadhali ya ukoloni” yalimuuma, yalimuudhi na kumuumiza moyo, akahoji mnasema afadhali ya mkoloni!

Mwalimu Nyerere alizikubali baadhi ya hoja za waandamanaji aliopoona zina mantiki, aliahidi kupunguza mshahara wake kwa asilimia 20 na akawahakikishia hangewapeleka JKT watu walioiona kama kambi ya mateso.

Akamwagiza Waziri Mkuu wa wakati huo, Rashid Kawawa ahakikishe wanafunzi hao hawarudi chuoni bali wanarudi makwao.

Mheshimiwa Rais umenukuliwa ukiwaonya watu wanaotaka kuchezea amani ya nchi ambayo unathibitisha kuwa ilijengwa katika misingi imara, tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza, umesisitiza “msione vyaelea vimeundwa.”

Kupitia waraka huu, nakusihi uuone ukweli kwamba huko nyuma tulikotoka amani yetu ilijengwa katika misingi ya udugu, siyo uadui, uhasama wala ubabe.

Mwalimu Nyerere hakupambana na waandamanaji wa 1966 kwa nguvu za dola, hakuthubutu kutumia askari wenye risasi na mabomu kuwapinga waandamanaji wasio na silaha bali wenye hoja bali alikabiliana nao kihoja.

Watanzania tumejengwa katika msingi huo wa kujadiliana na kutofautiana bila kupigana.

Mwalimu Nyerere akawathibitishia uhalali wa JKT, wanafunzi waliompinga kwa kumwagiza Kawawa aende JKT, aonyeshe mfano kwamba haukuwa mpango wa kuwakomoa waliosoma, bali mpango wa kujenga Taifa.

Mwalimu Nyerere hakuwaepusha na JKT hata wanawe wa kuzaa, akina Anna Nyerere, Andrew (sasa hayati), Makongoro na Rose (wachache ninaowafahamu).

Waliokwenda JKT miaka ya sabini wangali wanakumbuka simulizi zilizohusu kisa cha Afande Vero, jinsi alivyomzaba kofi Rashid Kawawa.

Ndani ya mwezi mmoja wa Desemba 1966, Mwalimu Nyerere aliutafakari ujumbe wa waandamanaji uliohusu tatizo la utabaka kati ya wachache wenye nacho waliotumia nafasi zao na madaraka yao

 kujitajirisha na tabaka la wavuja jasho.

Mwalimu  Nyerere akaona hayo hayafai kuwako ndani ya nchi huru, akahisi yatampunguzia uhalali wa kutawala.

Kwahiyo ilipofika Januari 26, 1967 akaitisha kikao cha NEC mjini Arusha kilichoibuka na Azimio la Arusha ambalo lilipiga vita utabaka, unyonyaji, dhuluma na watu kutumia madaraka yao kujitajirisha.

Maandamano ya Aprili 26 hayana madhara

Mheshimiwa Rais, hakuna sababu ya halali inayokulazimisha kutumia nguvu kupambana na waandamanaji ifikapo Aprili 26, mwaka huu.

Mosi, kwa sababu watakaoandamana hawatabeba silaha ya kuwadhuru watawala ama wananchi wengine. Hali hiyo ya watu kuandamana bila silaha ndiyo inayofanya Watanzania makini wahoji inakuwaje Serikali ijiandae kutumia silaha kupambana na raia wasiokuwa na silaha?

Pili, maandamano hayo siyo ya kudumu, hayafanani na yaliyotokea Tunisia na

Misri ambako wananchi walipiga kambi kuonyesha nia ya kuzikataa Serikali zao.

Tatu, maandamano hayo ni ya siku moja kati ya siku 365 za mwaka, hayaizuii Serikali isitimize majukumu yake, wala waandamanaji hawakuzuii (Rais) kuendelea kuifanyia mema nchi yako.

Maandamano yao hayakuzuii usiwatendee mema Watanzania wanaokukubali, isipokuwa waandamanaji wanataka kuonyesha tu hisia zao kuhusiana na yale yanayogusa maisha yao ndani ya Tanzania yao chini ya utawala wako.

Kitendo cha watu kuonyesha hisia zao siyo dhambi wala siyo kosa la kuwafanya wapigwe na askari, wavunjwe viungo vyao, waumizwe ama wauawe.

Nne, waandamanaji bado ni raia wako, hawana Tanzania nyingine isipokuwa Tanzania moja tu inayowahifadhi Watanzania wote, wala waandamanaji hawana Rais wao mwingine zaidi ya

John Pombe Magufuli.

Isipokuwa tofauti ndogo tu kwamba waandamanaji wana hisia zao tofauti ambazo wamekusudia kuziweka wazi.

Hao watakaondamana hawatofautiani na Waisraeli walioandamana kumwendea Nabii Samweli kumwelezea hisia zao, maandamano ya Aprili 26 hayatofautiani na maandamano ya kihistoria ya wanafunzi ya Novemba 1966 yaliyozaa Azimio la Arusha.

Ikiwa maandamano ya Waisraeli yalizaa ufalme na maandamano ya wanafunzi ya mjini Dar es salaam yalizaa Azimio la Arusha, yaache maandamano hayo ya Aprili 26 yaandike historia tuone yatazaa nini. Usiyazuie!

Tano, kuyazuia maandamano hayo ni kuanzisha mapambano yatakayozaa vurugu na kuondosha amani iliyopo. Nakusihi Rais wangu, usiwe chanzo cha vurugu za kuikomesha amani ndani ya nchi unayotawala, hekima ya kawaida inashauri

kwamba “yeye anayeishi kwenye nyumba ya vioo asiwe wa kwanza kuwarushia wengine mawe.”

Nakusihi waache watu waandamane kwa amani ili wapumue yanayowauma, kwani hata hayati Mwalimu Nyerere aliumizwa na kejeli za “better were the colonial days”, lakini ustahimilivu wake ulimwepusha kuandika historia mbaya ya kumwaga damu za raia anaowatawala.

Ukistahimili utaingia kwenye orodha ya viongozi makini wasioogopa hoja za wanaowapinga, bali husikiliza hoja na kuufanyia kazi ukweli unaowasilishwa kwao, wakiyaacha maneno yasiyofaa ya waandamanaji yaishie hewani.

Sita, kwenye mikutano yako ya hadhara kuna Watanzania wengi wanaokukusanyikia ili kukueleza hisia zao, wapo waliodhulumiwa viwanja na wamerudishiwa, wapo

walioonelewa kwa namna moja ama nyingine nawe umewasaidia kupata haki zao baada ya kuwasikiliza vilio vyao.

Nakusihi uuone ukweli huu kwamba hata hao waliodhamiria kuandamana Aprili 26, bado ni Watanzania na wanayo haki ya kusikilizwa na Rais wao. Inabidi Serikali yako ijiweke kwenye mkao wa kupokea, ijue wanalilia nini?

Yawezekana wanaililia Tanzania mpya na iliyo bora ambayo ukiwasikiliza utapata kilicho chema.

Saba, nakusihi uuone ukweli huu kwamba thamani ya Mtanzania anayesema “ndiyo kwa Magufuli” ni sawa na thamani ya yule anayesema “hapana kwa Magufuli.”

Thamani yao ni moja, Mtanzania hawezi kupungua thamani yake kwa sababu tu ya kumwambia Rais hapana.

Nane, unapojiandaa kukabiliana na waandamanaji kwa kutumia nguvu kubwa inabidi ujiulize unalinda nini? Je, unailinda haki ya mwananchi na uhuru wake wa kujieleza ama unalinda kiburi cha kiutawala kinachowasukuma  kutokuwa tayari kusikia msiyoyapenda?

Unapodhamiria kutumia nguvu kubwa kuzuia maandamano, Je, thamani ya Mtanzania asemaye hapana itazingatiwa wakati wa operesheni na kuchukuliwa kuwa sawa na thamani ya Mtanzania asemaye ndiyo?

Maana haiwezekani ukailinda amani ya Tanzania pasipo kuitambua thamani ya Mtanzania, kwani “thamani” na “amani” ni pacha lazima viende pamoja.

Tisa, endapo itatokea Watanzania kadhaa wakapoteza uhai wao kwenye maandamano hayo, je, wewe binafsi utawaeleza nini Watanzania watakaobaki hai?

Utawaeleza nini wazazi wao na ndugu wengine wa marehemu? Je, utatamba kwamba umefanikiwa kuwazimisha waandamanaji na kwahiyo waliouawa wachukuliwe kirahisi kwamba uhai wao hauna thamani, wameuliwa kama wanavyouliwa kunguni, mbu na virobota wanaostahili kuangamizwa kuzuia magonjwa?

Nakufahamisha mapema kwamba damu ikimwagika itawasha moto usiozimika nchi nzima na utakuwa mwanzo wa wewe kujiumbia upinzani wenye nguvu, lakini ulio mbaya kwakuwa upinzani huo utachanganyikana na mbegu za chuki, uhasama na uadui.

Mapambano yatakayotokana na kuzuia maandamano yatazalisha makundi ya watu waovu kila mkoa, kila wilaya na kila pahala ambapo Watanzania watakuwa wameuawa.

Ukiwa Rais wetu wa tano hutatembea kifua mbele ndani ya Tanzania huru, badala yake utaifanya kazi ya urais huku ukijificha.

Kwasababu hasira ya Watanzania wasiokubaliana nawe itaongezeka na kuwa kali zaidi, pia itaenea kwa kasi kwenye maeneo yote muhimu kuanzia ndani ya chama chako (CCM) hadi serikalini.

Kumi na moja, nakusihi tafadhali ukumbuke siku za nyuma, Watanzania walipowapokea wageni wa Rais, huku Rais wao na mgeni wake wakitumia gari ya wazi iliyotembea taratibu kama imebeba maharusi.

Rais na mgeni wake wakiwa kwenye gari ya wazi waliwapungia mikono Watanzania waliokwenda kuwapokea. Leo ninyi watawala wetu mnalazimika kusafirishwa kwenye gari za vioo vyenye giza, huku gari zilizowabeba zikienda kasi mkiwahofia wananchi waliokuchagueni na kukuwekeni madarakani.

Hapo ni lazima kuna jambo lisilo la kawaida limetokea, hamuitendei haki historia ya nchi yetu, mnatakiwa kuwaongoza Watanzania kuurudia utanzania wao.

Hatua unayokusudia kuichukua ya kupambana na waandamanaji ni hatua ya hatari yenye hasara nyingi kuliko faida, kwa kuwa itakuongezea maadui ndani ya nchi unayotawala.

Hatua hiyo italeta chuki penye upendo, itakomesha uvumilivu penye subira na kuleta vilio penye kicheko, itawafanya vijana wapoteze tumaini lililoanza kuchipua baada ya ujio wako.

Nayaandika haya kwa nia njema nikiamini kwamba hasara hizo zinaweza kuepukwa, ukitaka kujenga Tanzania ya Magufuli yaani Tanzania ya viwanda, ziepuke hatua mbaya zinazokufarakanisha wewe na umma, usijiongezee maadui.

Msome kwa makini Mtume Paulo, anavyowashauri wamwaminio Mungu akisema “tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote na huo utakatifu ambao hakuna atakayemwona Mungu asipokuwa nao, mkiangalia sana mtu wa kwenu asiipungukie neema ya Mungu hadi shina la uchungu likaibuka ndani yake likamsumbua na kusababisha wengine watiwe unajisi kwa hilo” (Waebrania 12: 14 -15).

Katika kuijenga Tanzania upya unahitaji mchango wa kila Mtanzania wakiwemo wale wanaokwambia hapana, kwa ajili hiyo achana kabisa na dhamira ya kuzuia maandamano.

Badala yake Serikali yako ijipange kuyadhibiti ili maandamano hayo yasichukue mwelekeo hasi wa uporaji na fujo.

Mwisho

By Jamhuri