DHAMANA NININI?
Dhamana ni hatua ambayo mtuhumiwa wa kosa fulani huachiwa huru kwa muda, ili kusubiri hatua za kufikishwa mahakamani, au kama tayari amefikishwa mahakamani husubiri kuendelea na kesi kwa siku zijazo.
 Kwa hiyo, ili lije suala la dhamana ni lazima uwe umetuhumiwa polisi au tayari umefikishwa mahakamani. Ieleweke kuwa kuna aina kuu mbili za dhamana. Kwanza dhamana ya polisi na pili dhamana ya mahakamani. Hapa tunazungumzia dhamana ya polisi.

UKIOMBWA FEDHA KWA AJILI YA DHAMANA KATAA
Dhamana hutolewa bure. Ieleweke wazi kuwa hakuna malipo yoyote yanayotakiwa kutolewa ili mtuhumiwa au mshtakiwa akubaliwe dhamana. Mchezo huu wa kuomba fedha ili mtu apate dhamana umetamalaki zaidi vituo vya polisi.   
 Wewe kama raia, unalotakiwa kujua ni moja tu kuwa hakuna sheria inayomtaka raia kutoa fedha ili apate dhamana. Serikalini hakuna risiti ya malipo ya dhamana. Kama wewe utaamua kutoa fedha hiyo ujue umetoa kwa sababu zako lakini sheria iko hivyo. Ifikie hatua raia wajisimamie kwa kukataa kutoa fedha kununua dhamana.


  Hakuna kitu ambacho askari anaweza kukufanya ikiwa utakataa kutoa fedha kwa ajili ya dhamana. Hakipo kabisa kinachohitajika ni ujasiri wako tu kwa kumwambia askari kwamba ‘sikupi fedha kwa kuwa dhamana hainunuliwi.
 Usikubali kutoa fedha kwa ajili ya dhamana, ni kosa na fedha hizo ni rushwa. Na hiyo ni kwa dhamana zote — ya polisi pia ya mahakamani. Katika taratibu za kupata dhamana hamna kulipa fedha.

POLISI WANALAZIMIKA KUKUPA DHAMANA
Hapo juu nimesema kuwa ili upate dhamana hutakiwi kutoa chochote kitu isipokuwa kuna mambo yanazingatiwa ili upate dhamana. Baadhi ya mambo hayo ni haya.
(a) Kisheria ikiwa makazi yako au anuani yako ya makazi inajulikana vyema au haijulikani, lakini umewafanya polisi kuijua na wakajiridhisha kwamba kweli fulani haya ndiyo makazi yake, basi ni sababu ya kupatiwa dhamana. Hii ni kwa sababu lengo kuu la dhamana ni ili utakapohitajika upatikane kwa urahisi.
(b) Ikiwa kosa alilotenda mtu ni la kudhaminika, hakuna haja ya kuendelea kumshikilia. Sheria imeshaweka wazi makosa yapi dhamana ya mtu itolewe na makosa yapi isitolewe. Baadhi ya makosa ambayo mtu hatakiwi kupata dhamana ni kama kuua kwa kukusudia (murder), uhaini (treason), wizi wa kutumia silaha na kadhalika. Ajabu ni kuwa kwenye vituo vyetu vya polisi unakuta hata mwenye kosa la kutukana naye ananyimwa dhamana. Hii ni kinyume cha sheria na muda umefika wa raia wenyewe kuyakataa haya.


(c) Pia kama mtuhumiwa hana kumbukumbu (criminal records) zozote za uhalifu, nayo ni sababu au kigezo cha kumfanya apewe dhamana haraka. Hakuna sababu ya kuendelea kumshikilia mtu ambaye kwa kumbukumbu hakuwahi kutenda kosa lolote la jinai hapo kabla. Kisheria kutokuwa na kumbukumbu za uhalifu hapo awali ni dalili za uaminifu na ukweli. Hii nayo ni sababu ya kisheria na yafaa izingatiwe sana huko vituo vya polisi.
(d) Pia ikiwa polisi itajiridhisha kwamba mtuhumiwa atatimiza masharti ya dhamana atakayopewa kama kufika siku na saa atakayoamriwa, basi hakuna haja ya kumng’ang’ania. Hii nayo ni kati ya sababu za kisheria ambazo huwa hazipewi nafasi kwenye vituo vya polisi na hivyo kuendelea kulifanya suala la dhamana kuwa gumu.

NAMNA YA KUJIANDAA NA DHAMANA
Ni vema sana unapopata taarifa za ndugu yako kushikiliwa kituo cha polisi kujiandaa na dhamana. Usitoke nyumbani kwenda kituoni bila kujiandaa na dhamana. Na hii ni iwe una uhakika amefanya kosa fulani au huna uhakika. Zaidi kama unajua kosa lake ni la kudhaminika basi umuhimu wa kujiandaa na dhamana huongezeka.


 La kuzingatia sana; hakikisha unapotoka nyumbani una barua inayokutambulisha kwa suala la dhamana kutoka Serikali za Mitaa. Ukienda Serikali za Mitaa wanazijua hizi barua. Pia kama ni mwajiriwa usisahau kwenda na kitambulisho chako cha kazi.
 Hii husaidia kutopoteza muda kwa kurudishwarudishwa huku ndugu yako akiendelea kusota polisi. Kwa kujiandaa utamwokoa ndugu yako na zahma ya kulala au kukaa selo. Usiende polisi ukiwa hujajiandaa kwa kuwa kufanya hivyo ni kupoteza muda tu.
 
OMBA KUJIDHAMINI MWENYEWE, INARUHUSIWA
Kuna watu wamekuwa wakikosa dhamana kwa kukosa wadhamini. Lakini polisi wamekuwa hawawaelezi watu hawa haki hii ya kujidhamini wenyewe. Mtu akikosa mdhamini na polisi nao wanakaa kimya mtu anaendelea kusota. Hili si sawa kwa kuwa moja ya majukumu waliyonayo polisi ni kuwaelimisha watuhumiwa haki zao za msingi.


Aidha, kama ulikuwa hujui ndiyo ujue kuanzia leo kuwa inaruhusiwa kujidhamini mwenyewe na ukaondoka kituo cha polisi bila kuhitaji ndugu yeyote kukudhamini. Unachotakiwa kufanya kama uko mikononi mwa polisi ni kusema tu kwamba ‘nahitaji kujidhamini’ ili upewe fomu maalum uijaze na uondoke. Usisahau kuliomba hili ni haki yako.
 
Kuhusu Sheria za Ardhi, Mirathi, Ndoa, Kampuni nk tembelea: sheriayakub.blogspot.com

By Jamhuri