Ukombozi na mapinduzi kwa wanawake

Napenda kusema kwa mama zangu kuwa suala la ukombozi daima huambana na mapinduzi. Hayo ni mapambano yanayohitaji dhamira, busara, ujasiri na utashi wa kujikomboa kifikra na kiutamaduni.
 Kabla sijazungumzia ukombozi na mapinduzi ya mwanamke wa Kitanzania, nimeamua kwanza kuwafahamisha imani yangu na mtazamo wangu kwenu kutokana na shughuli zenu za kila siku.


  Sina tatizo katika kujitambua kwenu na kudai haki zenu mlizopewa na Mwenyezi Mungu, tangu mama Hawa alipoletwa duniani. Sina gere kwenu kwa heshima na utukufu mliojaaliwa na Mola wetu.
  Sina mashaka katika harakati zenu za kutafuta elimu kwa sababu mama ni mwalimu, tabibu na mlezi wa familia. Kuelimika kwa mama ni kuelimika kwa familia. Kutoelimika kwa mama ni kutoelimika kwa familia. Huo ndiyo ukweli uliopo duniani kote.


  Sichukii kusikia wala kuona wanawake wanapofunga vibwebwe katika kudai  usawa wa kijinsia na katika masuala ya kupata elimu, ajira, madaraka katika uongozi wa kitaaluma na kisiasa kwa sababu ni tunu mlizopewa na Mwenyezi Mungu tangu awali.
  Sina sababu kwa vipi nisiwasifu kwa maumbile yenu, tabasamu zenu,  unyenyekevu wenu na huduma zenu mbele ya watoto wenu na waume zenu. Achilia mbali utii wenu mbele ya wazazi na viongozi wenu.


  Sasa naweza kuzungumzia ukombozi na mapinduzi ya mwanamke wa Tanzania. Sizungumzii ukombozi na mapinduzi ya kisiasa la hasha. Nazungumzia hali duni na mabadiliko ya fikra na mbinu za kujiwezesha kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.
  Idadi kubwa ya walimu nchini ni wanawake. Walimu hawana budi kujitokeza kwa wingi kuanzisha vikundi vya kutoa elimu ya msingi hadi sekondari kuanzia huko majumbani hadi ngazi ya kijiji, mtaa na kata.


  Kushawishi na kuhamasisha wasichana na wanawake kujenga tabia ya kupenda elimu badala ya mipasho na misuto, itasaidia sana kupunguza au kuondoa ombwe lililopo la elimu kati ya wasichana na wavulana na kati ya wanawake na wanaume.
  Kama mnaweza kuanzisha vikundi vya kwaya, ngoma, misuto, Vikoba au Saccos vipi mshindwe kuitafuta elimu kwa udi na uvumba? Kama mnathubutu kuhamasishana kaulimbiu ‘Mwanamke ni suna kusutwa’, vipi mshindwe kuhamasishana kaulimbiu ‘Mwanamke elimu kwanza?’ Tafakari.


 Nimewasifu jinsi mnavyoweza kutunza vibubu vya kuweka fedha, kuanzisha upatu wa Vikoba, Saccos na kuwa wajasiriamali katika kuanzisha viduka vya bidhaa mbalimbali na kuanzisha migahawa ya vinywaji na vyakula. Achilia mbali uchuuzi wa matunda, mboga, nguo na urembo. Haya mnayaweza sana.
 Inakuaje mshindwe kujiunga pamoja na kuanzisha umoja wa kutoa elimu ya biashara na utunzaji fedha kujenga mitaji ya kuanzisha asasi za awali za uchumi badala ya kuanzisha vijiasasi vya kujenga chuki na wivu?


 Ukweli mkithubutu mnaweza mkafanya majambo. Hivi karibuni mmeweza kuanzisha na kumiliki benki yenu ya wanawake. Hii ni hatua nzuri. Lengo hapa ni kuwaendeleza na kuwainua wanawake kiuchumi. Kwa hili sina ubishi, nakupeni kongole zenu.
 Hata hivyo, ni busara pia kuanzisha au kuendeleza vikundi vya kiuchumi badala ya kuacha mtu mmoja mmoja kufanya shughuli zake. Utaratibu ukifanywa na vikundi kitaifa utawakomboa sana akina mama.


 Binafsi nakerwa na desturi ya kukeketa na kutia mimba ya utotoni wasichana. Wanawake kuvaa nguo fupi kwa kusingizio cha “mitindo ya kisasa na kwenda na wakati”. Mwanamke kufanywa bidhaa huo ni utumwa wa waziwazi.
 Ndugu yangu Ramadhani Fomu wa Polisi Morogoro amenieleza kuwa mshahiri mmoja wa Kiarabu amewasifu na kuwapa heshima wanawake kwa kuwatungia mashahiri yafuatayo.


“Katika malezi ya mwanamke, ndipo kunapopatikana amani. Na katika kifua cha mwanamke ndiyo kuna mapenzi. Kwa mwanamke ndiyo kuna utulivu, na katika viganja vyake kuna usalama, na maneno yake ni utajiri na upole wake ni dawa.”
 Sifa zote hizo amepewa mwanamke. Vipi mwanamke ushindwe kujiheshimu na kujithamini? Heshima yako na thamani yako itatokana na fikra zako za kujikomboa na mapinduzi ya vitendo vyako. Nani kama mama?