MVOMERO

Na Mwandishi Wetu

Tochi ya watu wasio na sauti imemulika na kubaini mfumuko wa bei katika bidhaa mbalimbali nchini na kuhoji iwapo umeachwa uendelee kwa makusudi ili uwe faida kwa wenye nacho na kilio kwa wasio nacho? 

Watu wanajiuliza ni nani anayejali ‘mfumuko huu’ unapoumiza wasio na kipato?

Septemba 10, 2021, wakati wa kuahirisha mkutano wa nne wa Bunge la 12 jijini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema serikali imeunda timu maalumu kuchunguza kupanda kwa bei ya mafuta kwa kuwa kitendo hicho kinawaumiza wananchi hususan wa hali ya chini.

Novemba 24, 2021 pia Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitilla Mkumbo, wakati akizungumzia hatua wanazochukua baada ya kupanda kwa bei ya vifaa vya ujenzi, aliiagiza Tume ya Ushindani wa Biashara (FCC) kufanya uchunguzi kuhusu kupanda kwa bei ya saruji.

Kauli hizo za viongozi waandamizi serikalini zinakupa picha kwamba tatizo la kupanda kwa bei ya bidhaa si la mzaha, na inaonyesha bila hatua kuchukuliwa, kupanda huko kutaendelea kutikisa maisha ya watu wa kipato cha chini ambao wanategemewa kuwa na mchango katika ujenzi na ukuzaji wa uchumi mdogo wa taifa.

Kama kuna kitu kinachowaliza Watanzania wengi hivi sasa, ni mfumko huo kuendelea kushamiri, licha ya kuwapo mamlaka zinazoweza kuukomesha.

Viongozi wenye dhamana na kauli ya kufanya watu wawe na maisha nafuu, ni kama hawasikii au kuona kwa kuwa maumivu hayo hayagusi maisha yao! 

Ni rahisi kwao kutoona adha hiyo ijapokuwa wana macho lakini hawaoni, wana masikio lakini hawasikii na hali hiyo imebaki kuwa shangwe na vigelegele kwa wenye nacho, na kuwa kilio kwa wasio nacho (walalahoi).

Msumari wa moto kwa wananchi

Katika siku za hivi karibuni, mfumuko wa bei za mafuta ya kupikia, petroli, dizeli na mafuta ya taa, zimekuwa msumari wa moto na kusababisha kila sekta ya huduma kwa maisha ya wananchi kuathiriwa, hivyo kudumaza uchumi na maendeleo yao kisiasa, kijamii na kiutamaduni, ingawa nauli ni donda ndugu jingine.

Kama kuna eneo ambalo linaathiriwa moja kwa moja ni usafirishwaji wa chakula kinachogusa wengi, maana ili binadamu aishi lazima ale; maendeleo huletwa na mtu mwenye afya njema. Ili kuujenga uchumi wa mtu binafsi na taifa, chakula ni muhimu. 

Watu wa mijini huathiriwa na bei za juu za chakula huku wakulima wakiumizwa na bei kubwa za usafirishaji mazao kutoka vijijini hadi mijini ambazo huwa maradufu.

Mkulima asipokuwa makini mazao huozea shambani au anaposafirisha, mbali ya kilimo chenyewe kuhujumiwa na kupanda kwa bei za pembejeo.

Msumari mwingine wa moto, ni bei ya vifaa vya ujenzi; yaani saruji, nondo na mabati. Msione huku vijijini wanakaa kwenye nyumba za tembe zilizowekwa mabati yenye kutu na kuegeshewa mawe, hii ni kutokana na kwamba bei ya mabati imepanda kutoka Sh 17,000 hadi Sh 34,500; tena ALAF kiwandani. 

Huyu aliyeshindwa kununua petroli akajifungue ataweza kuezeka nyumba?

Tujiulize, je, nini sababu za kupanda kwa bei za bidhaa kwa kiwango kikubwa kiasi hiki? Wawakilishi na watendaji wa wananchi waliowachagua na kuwapa nafasi hizo wawasemee wawe bubu na wasioona maumivu ya wananchi?

Tochi ya wasio na sauti inamulika tena gizani na kuona! Je, shida ni viongozi au wawakilishi kutojua wajibu wao kwa wananchi? Je, ni nguvu iliyojificha ya wanaopandisha bei? 

Je, bidhaa zinazopandishwa zina uhusiano na wawakilishi hao nyuma yake? Je, wanaogopa kusema wasije wakakosa uteuzi? Tochi inaendelea kumulika gizani na kujiuliza: Ni kiongozi gani asiyeelewa kuwa mgawo na kukosekana kwa umeme, hata bei ya maji yanayouzwa mitaani gharama zake huwa zinapanda na kuna uwezekano wa kuuziwa maji yasiyo safi na kuibua gharama kubwa ya matibabu na kuhatarisha maisha ya wananchi? 

Je, wawakilisha hao ni wa wenye nacho na si wa wasionacho, ndiyo maana wako kimya?

Tochi inamulika na mwanga unaonyesha! Ni mwakilishi na mwajiriwa gani wa wananchi asiyejua umeme ukikosekana, na wanaotumia jenereta au umeme wa jua kutoa huduma wanapandisha bei? 

Gharama za uzalishaji huongezeka hata kinyozi tu naye anapandisha bei, na hata kudurufu karatasi, na pipi za watoto wadogo zinaongezeka bei bila woga kwa malaika hawa!

Hivi majuzi tochi ilipokuwa kijijini kwenye familia ya Athanas Mwalongo, iliyokuwa na msiba wa mjamzito (Handeni) ambapo umbali kutoka hapo hadi ilipo zahanati ni mwendo wa nusu siku, alifariki dunia kwa kukosa Sh 5,000 za kununua lita moja ya petroli ampe bodaboda amfikishe hospitalini!

Ieleweke kwamba; huko mashambani tunakokaa na wananchi, wakati Sh 1,000 kwa wenye nacho ni fedha ya kununulia sindano au kiberiti, kwa wasio nacho hiyo ni sawa na Sh 1,000,000 hata kama wana mazao mengi, na ndiyo maana mmeshuhudia mtoto akichukua Sh 100 akanunua biskuti au pipi, hupigwa kwelikweli!

Katika hili ifahamike pia, kwa safari hii kumekuwa na kinachodaiwa ni mabadiliko ya tabia nchi.

Chakula kitakuwa na bei kubwa na wakulima watakapotaka kupandisha bei kubwa kama wafanyabiashara wanavyofanya, watadhibitiwa kwa nguvu kubwa! Lakini wafanyabiashara hakuna anayewadhibiti. Tunaumia na bei!

Semeni Mfwimi, aliyekuwa akimuuguza mama aliyefariki dunia kwa kukosa lita moja ya petroli, anasema: “Kama chanjo ya Covid-19 na elimu vinaweza kuwa bure kwa sababu ‘vimeruzukiwa’, inashindikanaje kwa huduma ya afya ambayo imekuwa kama msumari wa moto kwa wananchi wasio na kipato?”

Mtalaamu wa uzalishaji wa Kiwanda cha Mabati ya Dragon, Dodoma aliyekuwa mkoani Morogoro na aliyeomba asitajwe jina, anasema: “Suala la umeme kukatikakatika limekuwa msalaba hata kwa wazalishaji wa vifaa vya ujenzi, gharama za uzalishaji zinaongezeka, huku ndiko kunaongeza pia bei ya vifaa hivi.

“Viongozi wenye dhamana ya kutetea wananchi, wanaoweza kuondoa kadhia hii wanapokaa kimya hadi maangamizi ya kibiashara na kiuchumi yatokee, ni hatari. 

“Sasa hivi wateja wanaokuja kununua vifaa vya ujenzi kiwandani ni wale wenye uwezo tu. Wasio na kipato ni mmoja kwa watu 50.”

Mtaalamu huyo anadai kuwa kutokana na maisha magumu na bidhaa kupanda bei, hivi karibuni kijana mmoja wa Mpwayungu, Dodoma, alipigwa hadi kufa kwa sababu alichukua mabaki ya vipande vya bati vilivyokatwa kwenye nyumba iliyokuwa inajengwa ili akaweke juu ya nyumba yake ya majani iliyokuwa inavuja, akidhaniwa ni mwizi.

Lakini kiukweli aliponzwa na kudhani kwake kuwa vipande vile havikuwa na kazi.

Mwandishi wa Majira mjini Morogoro, Severini Myelu, akielezea mfumuko wa bei unavyowatesa wananchi wasio na kipato, anasema:

“Maumivu ya wasio nacho ni sawa na kumnenepesha mtoto wa jirani ilhali watoto wako wanalala njaa.”

Anasema Severini akiongeza: “Wakristo wanapofurahia ujio wa Krisimasi na Mwaka Mpya, wanachukizwa na mfumuko wa bei!”

Wananchi walioathiriwa na mfumuko huo waliozungumza na mwandishi wa makala hii kwa nyakati tofauti wamedai: “Yawezekana wenye mamlaka hawauoni mfumuko wa bei za bidhaa unavyotuumiza huko nje kutokana na nafasi zao (vyeo) kuwapa ahueni ya kipato. Hawaendi sokoni, wanapelekewa mahitaji.

“Laiti kama tungebadilishana! Wao wawe hawana kipato na tuchukue vipato vyao, vyeo na nafasi zao, kusingekucha, maana kwa saa chache, mfumuko huo wa bei ungekomeshwa haraka kama ambavyo mwanamume angebebeshwa ulezi wa mimba asingekaa nayo hata nusu saa. Angeomba mabadiliko.”

Helena Jackson, wa kijiwe cha Msanvu, Morogoro, anasema Januari 2021 aliwekeza kwa mwenye duka mabati 10 ya kuezekea nyumba yake kwa Sh 17,000.

“Lengo ni niezeke kibanda niwe na maendeleo ya makazi mazuri. Lakini baada ya kifo cha Rais John Magufuli, bati hizo zimepanda mara mbili na sasa ni Sh 34,500. Kwa hiyo kwa sasa siwezi tena kununua, ninahangaikia mlo wa kila siku, kwa sababu mwenye duka anataka niongeze fedha japo nililipa Sh 800,000.”

Serikali ifanye nini?

Serikali iwaonee huruma wasio nacho, itazame upya punguzo la kodi ya ongezeko la thamani, ipitie Sheria ya VAT na kutazama  ili iwapunguzie wananchi maumivu ya kupanda kwa gharama za maisha.

Asilimia ya VAT iliyopo hivi sasa ya 18% ukiweka na tozo hizi zilizoongezwa kwenye bajeti, mwananchi anakuwa na mzigo mkubwa sana na ni kwa vile serikali haiingi majumbani mwa watu ikaona kuna amani au ugomvi. 

Ni rai yangu serikali iwafutie wananchi tozo ya kadi za simu angalau inaweza kuwapa nafuu kidogo ya kimaisha, na kama serikali ina madini, gesi na rasilimali zingine, itafute namna ya kuweza kupata mapato bila ya kuathiri sana shughuli za wananchi kwani hiyo itasaidia wananchi kujijenga vizuri kiuchumi.

Hili linaweza kufanyika kwa ufanisi kwa kufanya tafiti yakinifu juu ya namna ya kuweza kupata vyanzo vipya vya mapato kuliko kuendelea kutegemea vyanzo vilevile vya Adamu na Hawa kila wakati, jambo ambalo litasababisha kudumaa kwa uchumi wa nchi wakati huu wa mdororo wa uchumi duniani.

0715 933 308

By Jamhuri