DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Rais Samia Suluhu Hassan, nakuomba unisaidie kupata haki yangu. Mimi naitwa Frida Kyesi, ni mama mjane wa Mzee Lutengano Mwakabuta ambaye alikuwa mstaafu.

Kwa sasa naishi Pugu Kajiungeni, Ilala jijini Dar es Salaam tangu mwaka 1982. Mwaka 1986 nilibahatika kununua eneo jingine lenye ukubwa wa ekari 12 kutoka kwa jirani yangu aliyeniuzia kihalali na bado yupo hai.

Eneo hili nalimiliki kwa miaka yote bila kuwa na shida hadi ikafikia hatua ya kuanza kuuza vipande – kuwauzia watu wengine na mwishowe nilitoa eneo kwa ajili ya kujenga kanisa.

Ilipofika Januari, mwaka juzi ndipo alipotokea kijana mmoja (jina lake linahifadhiwa) na timu yake walivamia kiwanja changu namba 458, chenye ukubwa wa mita za mraba 42,054 kilichopo Kata ya Pugu Mwakanga, Kitalu B.

Eneo hilo nilinunua kwa Rashid Mmbonde mwaka 1986 na amenisaidia kutoa ushirikiano katika hili tatizo kwa maana alipoitwa na OCD wa Polisi Chanika alikwenda akatoa maelezo yake na hata Takukuru walipomuita alishirikiana nao vizuri. 

Wakati uvamizi huu unatokea, mimi tayari nilikuwa nimeshawauzia watu viwanja kwenye eneo langu kama nilivyoeleza awali. Pia nilishagawa ekari moja kama sadaka kwa matumizi ya Kanisa la Shekemu Ministry mwaka 2012.

Awali, kijana huyo alidai katika Baraza la Kata kuwa eneo la ekari moja na robo tatu ni eneo lake.

Kwa kifupi uvamizi huo ulipotokea kwa sehemu kubwa uliathiri shughuli za kanisa na watu niliowauzia viwanja. 

Tuliitwa katika Baraza la Ardhi la Kata ya Pugu Kajiungeni baada ya mlalamikiwa huyo kufungua kesi huko, lakini kabla ya kwenda huko tulikwenda kwa Kamishna wa Ardhi wa Mkoa wa Dar es Salaam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuomba ushauri na kutoa malalamiko ya uvamizi wa eneo langu.

Kamishna alitushauri tuombe Baraza la Kata litupe barua inayotuhamisha kwenda katika Baraza la Wilaya ya Ilala kwa kuwa ndio wenye mamlaka ya kusikiliza kesi yetu kisheria.

Tulipopeleka maombi katika baraza na maelekezo ya kamishna, tuliambiwa tusubiri tutapewa barua.

Lakini kilichokuja kutokea si barua tena, bali hukumu iliyompa kijana huyo eneo nililokuwa nimewapa kanisa mwaka 2012 na robo tatu ya ekari moja ambayo tayari nilishauza kama viwanja kwa watu wengine kabla hawajavamia.

Nilimjulisha kamishna wa ardhi kilichotokea na akanishauri nikate rufaa katika Baraza la Wilaya ya Ilala. Nilifanya hivyo kupitia wakili wangu na Septemba 22, mwaka juzi uamuzi wa Baraza la Kata ulifutwa rasmi.

Kipindi tulipokuwa tunaendelea na taratibu za uendeshaji wa kesi ya rufaa, katika hali isiyokuwa ya kawaida, kijana huyo akaanza kukata viwanja katika eneo langu na kuanza kuviuza.

Uvamizi huo umesababisha baadhi ya waumini wa kanisa hili kuanza kupigwa na kijana huyo na kikundi chake hasa pale anapoleta wateja na waumini wanakwenda kuwaambia wateja kwamba eneo ni la kanisa haliuzwi.

Mchungaji wa kanisa hili amewahi kukimbizwa na mapanga na mshirika mmoja kupigwa na jembe tumboni na baada ya kipigo hicho amekuwa akilalamika kuhusu maumivu tumboni.

Novemba 26, mwaka juzi mshirika huyo aliyezuiliwa na kijana huyo na kundi lake alifariki dunia.

Kwa sasa sina raha kwa sababu niliowauzia wameshambuliwa kwa kukatwa mapanga na katika

kanisa walipoweka uzio wa nguzo kwenye eneo lao, kijana wao alikuja usiku akazing’oa zote na kuondoka nazo.

Kutokana na hofu ya usalama, waumini wengi wamekimbia kanisa hilo kwa sababu wamekuwa hawapati msaada wa mamlaka husika kwa kumwogopa mvamizi huyo.

Pia Mwinyimvua ambaye ni kijana wangu wa kazi naye amewahi kupigwa na kundi la mvamizi huyo na kuambiwa asionekane katika eneo langu watamuua. Siku ya tukio hili mwanangu Flenan pia alifanyiwa fujo na kutishiwa maisha.

Lakini cha ajabu zaidi ni kwamba kijana huyo aliendelea kumtolea vitisho vya mauaji mwanangu hata mbele ya polisi mpelelezi Tumaini. 

Hata baada ya zuio nililoomba liwekwe wakati wa uendeshaji wa kesi kuondolewa na Baraza la Wilaya lakini bado amekuwa akizuia watu kuendelea na shughuli zao na hata kudiriki kuwavunjia wanaojenga walionunua kihalali kutoka kwangu na wamepitia mamlaka husika katika mauzo hayo.

Kwa sasa watu waliomo katika eneo langu wamekuwa wakikutana na vurugu isiyo ya kawaida, inayosababisha kutishiana mapanga.

Kijana huyo amekuwa na kawaida kuuza maeneo ya watu na kuwavunjia na sasa anafanya hivyo katika eneo langu lote la mraba mita 42,054 ninalolimiliki kihalali tofauti na kanisa.

Eneo la awali alilodai kijana huyo ni la kwake amewatishia maisha na waliovunjiwa na waliopata usumbufu wameripoti matatizo haya Kituo cha Polisi Chanika lakini hawajapata msaada.

Tuliwahi kupeleka malalamiko yetu kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala kupitia kwa Diwani wetu, Imelda Samjela na maelekezo yake tuliitwa ofisi za Takukuru na kutoa maelezo yetu kuhusu kadhia hii.

Lakini pamoja na hayo kufanyika, hatuoni hatua zikichukuliwa, kwa sababu usumbufu ndiyo umezidi maradufu.

Yafuatayo ni baadhi ya malalamiko tuliyowahi kupeleka Polisi Chanika kuhusu kijana huyo na watu wake lakini hayajawahi kushughulikiwa.

Baadhi ya kesi ni CNK/RB/ 2021 kujipatia mali kwa udanganyifu – Frida Kyesi, CNK/RB/2021 kupigwa na kutishiwa maisha – Mwinyivua Zungo, CNK/RB/2021 kupigwa na kujeruhiwa – Dina Mrisho, CNK/RB/3165/2021 kutishia kuua kwa maneno – Flenan Kilasara.

Nyingine ni CNK/RB/ 2021 kuharibu mali kanisani -Anthony Walter, CNK/RB/ 2021 kupigwa kofi – Mzee wa Kanisa Eric, NK/RB/347/2021 kuharibu mali – Halifa Ally – Mpare.

Kesi namba CNK/RB/ 7246/2021 kupigwa na kujeruhiwa –  Betheli, CNK/RB/ 7199/2021 kuharibu mali – jirani na nesi, CNK/RB/2021 kuharibu mali – Dawa wa CCM.

Kwa kweli inauma kuona watu niliowauzia viwanja katika eneo langu halali wanasumbuliwa, wanavunjiwa na kupata hasara wanapojenga na hata kutishiwa maisha na wengine maeneo yao kuuzwa. Wamekuwa hawana amani.

Ni mimi Frida Kyesi.

Nimetuma nakala hii pia kwa OCD Polisi Wilaya ya Ilala, Polisi Chanika, Mkuu wa Wilaya Ilala na kwa Diwani wa Pugu Kajiungeni.

By Jamhuri