Tutaanza kumshangaa Sure Boy 

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu 

Huko nyuma tuliwahi kuvishangaa viwango vya wanasoka kadhaa wa ndani kama akina John Bocco, Aishi Manula, Erasto Nyoni na Shomari Kapombe.

Hawa walitushangaza au waliushangaza ulimwengu wa soka mara tu baada ya kuhamia Simba SC wakitokea Azam FC zote za Dar es Salaam. Tuliwashangaa sana na kwa hakika tulikuwa na haki ya kushangaa.

Yaani ghafla tu tukawaona ni kama wamekuwa wachezaji wapya kabisa ambao hatukuwa tukiwafahamu kabla. Lakini kumbe ni walewale waliokuwapo maeneo ya Mbagala kuelekea Mbande kwenye Uwanja wa Chamazi na ni hawa hawa ambao kila wiki walikuwa wanacheza kwenye viwanja mbalimbali vya soka nchini. 

Lakini mara tu walipofikia uamuzi wa kuondoka Azam; kile kitendo tu cha kuhamia Simba, kikawafanya mashabiki tuanze kuwafuatilia kwa umakini zaidi. 

Yaani tukaanza kuwatazama kwa jicho la tatu. Ni hapo ndipo tulipoanza kuwaona kina Manula, Bocco na Kapombe kama wachezaji wapya kabisa katika soka la Tanzania! Kwa nini? Kwa kuwa sasa wamesogea zaidi akilini na kwenye mboni za macho yetu. Hawapo Chamazi, wamehamia mjini. Wapo Msimbazi.

Kuna shida mahala kwa mashabiki wa Tanzania. Hii ni kwa kuwa wengi wetu tunakwenda viwanjani kutazama timu zetu na mastaa tunaowapenda tu. Tunaishia hapo.

Huwa hatuna muda wa kutupa jicho upande wa pili na kutazama ni nini kinachoendelea katika timu nyingine na nyota wao. Tunachukulia kama vile timu hizo hazipo.

Aina hii ya kutazama mpira ndiyo iliyofanya tuwashangae sana akina Manula.

Kwa kusema ukweli ni kwamba, tofauti ya Manula wa Azam FC na Manula wa Simba SC iko nje ya uwanja tu, lakini ndani ya uwanja bado Manula ni yule yule. 

Akiwa nje ya uwanja Manula wa sasa ana mashabiki wengi kuliko aliokuwa nao Azam FC. Ana kundi kubwa la watu linalomfuatilia tena kwa furaha na mshawasha mkubwa tofauti na alipokuwa Azam FC. Hii ni tofauti kubwa sana.

Uwanjani kwa tunaofuatilia soka bila kibanzi jichoni, Manula ni bora tangu alipokuwa Azam FC hata sasa. Shida moja tu ni kwamba, kule Azam wengi hawakuwa wakimtazama mara kwa mara kama ilivyo sasa akiwa na Simba SC. 

Kuna ambao hata wala hawataki kukumbuka au kufahamu kuwa tangu alipokuwa ndani ya kikosi cha Azam FC tayari Manula alishakuwa kipa namba moja wa Taifa Stars; yaani Tanzania One.

Amehamia Simba akiwa na ‘status’ hiyo na hadi leo ndivyo ilivyo au ndivyo alivyo.  

Sasa kwa hakika ni zamu ya Abubakar Salum ‘Sure Boy. Naye ninamuona akiwa katika njia ile ya kina Manula na Bocco. Ghafla naye sasa ataonekana ni mchezaji mpya ambaye ni kama hatukuwa tunamjua.

Sure Boy ni fundi wa mpira. Tena fundi kweli kweli. Alivyokuwa Azam FC, hakuna aliyekuwa anamtazama kila mara kama itakavyokuwa sasa.

Tulimtazama zaidi Sure Boy siku Azam FC walipokuwa wanacheza na Simba, Yanga; Azam FC ikicheza na Namungo FC hatukujipa muda wa kuitazama Azam wala Sure Boy mwenyewe na kuupima au kuutathmini uwezo wake wa kusakata soka.

Kinachokwenda kutokea Yanga, Sure Boy ataimbwa kuliko ilivyokuwa alipokuwa akichezea Azam FC ambako aliimbwa na kikundi cha mashabiki wachache walioongozwa na rafiki yangu Hassan Manyanya, tena wanaoishia pale pale Azam Complex, Chamazi. 

Huko Yanga kila atakapokanyaga na timu au matembezi yake binafsi atashangiliwa, ni kama anavyoshangiliwa Aucho ambaye baadhi ya Watanzania hawakuwa wanamjua kumbe aliwahi kucheza hapo Kenya – Gor Mahia.