Watanzania hivi sasa wamo katika mawazo na mazungumzo ya ajenda moja tu ya Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika hivi Oktoba 25, 2015 wa kuwachagua viongozi bora ambao ni madiwani, wabunge na rais wa nchi.

Mazungumzo hayo yanaendeshwa mchana na usiku katika sehemu mbalimbali zikiwamo za nyumbani, shambani, ofisini, chuoni na kijiweni ilimradi penye mkusanyiko wa watu wakiwamo wake kwa waume kuanzia rika la ujana hadi uzeeni.

Uchaguzi Mkuu hutoa nafasi kwa Watanzania kila baada ya miaka mitano kuchagua na kubadili baadhi ya viongozi na kuweka wenye uwezo wa kushika madaraka na kuwaongoza Watanzania kwa kipindi hicho, katika hali ya usalama salimini na kuboresha maslahi ya watu.

Mamlaka inayohusika kushughulika na kusimamia kazi ya Uchaguzi Mkuu –  Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) – imesharuhusu vyama vya siasa na wagombea uongozi kufanya kampeni za kunadi ilani za vyama vyao kwa kumwaga sera na ahadi, wakitilia mkazo vipaumbele vyao watakapopata ridhaa ya kushika dola.

Kila chama na kila mgombea anajitapa na kujigamba yeye na chama chake watakavyoweza kutimiza mahitaji na matakwa ya Watanzania katika mustakabali wa kupata elinu bora, afya nzuri, kazi na ajira pamoja na kukuza pato la kila mtu na kuinua uchumi wa nchi.

Kabla na baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza rasmi kuanza kwa kampeni wiki iliyopita, vyama na wagombea wao wamejichimbia chini ya msamiati wa kisiasa ‘Mabadiliko’. Hata vyombo wa mawasiliano na umma baadhi yao navyo vimejitumbukiza humo.

Linapotamkwa neno ‘mabadiliko’, mimi huzingirwa na maswali makuu matano. Nini maana halisi ya mabadiliko? Ni mabadiliko yepi Watanzania wanayotaka? Mabadiliko hayo ni kwa manufaa ya nani? Nani ni mwendeshaji na msimamizi mkuu wa mabadiliko yatakiwayo? Na la mwisho, je, ni wakati mwafaka wa kutaka mabadiliko?

Ni vema wananchi na Watanzania wakatambua wanahitaji ‘mabadiliko’ au wanataka ‘bora mabadiliko?’ Ni faida ipi watakayopata katika mabadiliko na ni zahama ipi watakayovuna katika ‘bora mabadiliko’!

Ni busara kwanza kuangalia nchi barani Afrika, Asia na Ulaya zilizofanya ‘mabadiliko’ na ‘bora mabadiliko’ zipo katika hali gani hivi sasa kiuchumi na kiusalama.

Mimi ni muumini wa mabadiliko. Lakini kuna baadhi ya Watanzania wanaotaka ‘bora mabadiliko’ ilimradi yawepo tu mabadiliko. Hii inatokana na kauli zao za kejeli, mzaha, kuficha au kutosema ukweli juu ya jambo fulani na badala yake kuleta ushabiki mwingi mbele ya wahitaji mabadiliko, jambo ambalo ni hatari.

Mgombea au kiongozi wa siasa anaposimama jukwaani na kutoa porojo, uwongo au kusita kusema ukweli na badala yake kutetea na kushabikia vitendo vibaya vilivyowahi kutendwa ndani ya jamii hii, ni hatari mno.

Baadhi ya Watanzania na viongozi nchini wanapojinasibu kurejea na kukariri nusunusu au kinyume na kauli ya Baba waTaifa, Mwalimu Nyerere, kwa maelezo kuwa wanamuenzi ilhali sivyo, ni sawa na kumdhihaki na kuwaona Watanzania wengine kama majuha! Hii ni hatari.

Siandiki kwa hisia bali naandika kwa uhalisia. Sipendi kutoa mifano halisi kwa sababu unafahamu fika ninachokisema. Mifano iko mingi kuhusu hayo niliyoyaeleza.

Nachelea kufungulia uchochezi usije kutamalaki ndani ya jamii yetu. Itoshe tu na wewe kuangalia na kupima yasemwayo ukemee na kuepuka ushabiki.

Sioni haya kutamka katika msimu wa uchaguzi wa mwaka huu ‘ushabiki’ unanuka na kuranda kama rushwa inavyobembea nchini. Huu ni msimu wa tano wa uchaguzi wa vyama vingi vya siasa (1995-2015) uliotanguliwa na misimu minne iliyopita ya kutokuwa na ushabiki mpana na hatari kama huu wa leo. Kulikoni? 

Ushabiki wa msimu wa mwaka huu, umewakumba hata baadhi ya wagombea, viongozi wa siasa na hata waandishi wa habari kama si vyombo vya habari.

Kwa desturi, ushabiki hufanywa na wenye vyama vyao vya siasa. Waandishi au vyombo vya habari vinapomshabikia mgombea maana yake ni nini? Ni vema mkanielewesha.

Ushabiki unapopandwa na kupaliliwa kwenye vikundi au vyama vya ngoma, kwaya, klabu za mpira au hata vijiweni na maskani ukweli vinasisimua ushindani uliopo wa kimchezo na kutia hamasa na burudani ndani ya mioyo ya wanamichezo. Mashindano yakimalizika na ushabiki unaisha wala hakuna madhara.

Ushabiki unapoletwa ndani ya vyama vya siasa vyenye dhima ya kubeba maslahi na maisha ya watu na hasa katika msimu kama huu ukaachiwa kuchanua kama mtende; wakati Watanzania wanatafuta viongozi bora wa kuwaweka madarakani kwa maslahi ya Taifa, ni sawa na kuchezea shilingi kwenye tundu la choo.

Hivi ni kweli Watanzania mpo tayari kupoteza maisha yenu, usalama wenu kwa thamani ya ushabiki? Ushabiki una maana gani mbele ya ukweli na hoja? Ukweli na nguvu ya hoja ndizo zana ya kuleta mabadiliko nchini Tanzania. Ushabiki ni zana ya kuvuruga mabadiliko.

Ni busara na hekima kwa wanaounda na kuusambaza ushabiki huo kuacha kuusanifu kwani matokeo yake ni kuleta ghasia. Ushabiki huo unaweza kuleta sintofahamu wakati wa kupiga kura na kutangaza matokeo ya kupiga kura kwani kila shabiki atajihesabu ni mshindi ilhali si mshindi.

1450 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!