Naomba Mhandisi Mjungi akumbukwe

Na Angalieni Mpendu

Rais Dk. John Pombe Magufuli nimekusikiliza kwa utulivu, nimekusoma kwa umakini na nimekuelewa kwa undani katika hotuba yako ya uzinduzi wa Daraja la Mfugale (Mfugale Flyover), eneo la TAZARA, katika makutano ya Barabara ya Mandela na Barabara ya Nyerere wiki iliyopita jijini Dar es Salaam.
Kati ya mambo niliyoyaelewa moja wapo ni ‘gharama ya kuwa mwaminifu katika kazi.’ Jambo hili umelieleza katika hisia za huzuni jinsi tabia ya uaminifu inavyopewa majuto na toba. Hakika malipo ya aina hii hutia simanzi moyoni na ganzi mwilini.
Samahani. Sehemu hii ya hotuba imenichoma moyo na kutia maumivu mwilini mwangu. Hata kama macho yanacheka kwa furaha ya kupata maendeleo ya miundombinu ya barabara na madaraja, lakini moyo unalia kwa sababu tu ya kupuuzwa tabia njema na taaluma ya mtu. Si kitendo chema ni choyo.

Ukisema ukweli, ukitetea haki yako au haki ya mtu mwingine, ukakataa dhuluma na uonevu, ukazingatia maadili ya kazi au taaluma yako au ukapenda na ukatumikia nchi yako, hautapata shukrani wala faraja. Asante utakayopewa ni kebehi na dharau. Utapuuzwa au kutupwa kama vile hauna utu.
Utazikwa ungali hai au utakufa kwa kufikwa na kihoro. Na hiyo ndiyo eti gharama ya kuwa mwaminifu katika kazi na mtiifu katika nchi yako. Watu wengi nchini petu na hata duniani, hawamo katika simulizi fasihi na andishi kutokana na baadhi ya watu wakubwa kuziba sura za matendo mema ya watu.
Si semi watu wote watendao mazuri au wateteao mema hawapewi heshima, utukufu au tuzo zikiwa ni faraja. La hasha!  Wanapewa tuzo. Ninachosema, baadhi ya watu hufikwa na madhila haya. Angalia maelezo yafuatayo ya Rais Dk. Magufuli, namnukuu:

“Na walikuwa wakurugenzi wakuu wa barabara kwenye mwaka 2007, 2008. Hawa walikuwa wasimamizi wakuu wa barabara na madaraja katika Wizara ya Ujenzi, baada ya kupewa maagizo fulani na wakubwa wao wakayakataa, wakaamuliwa kufukuzwa. Wamshukuru katibu mkuu aliyekuwepo ambaye alizuia kufukuzwa kwao kwa sababu palikuwa kinyume cha sheria na wao walikuwa wameamua kusimamia maadili ya kihandisi.
“Nilitegemea wakati huo kwa sababu Wahehe huwa wana tabia ya kujinyonga, Mfugale angejiua, lakini yule mwenzake ambaye alikuwa si Mhehe, marehemu Mjungi, alikwenda kuchukua pistol akajipiga risasi. Na leo ni marehemu kwa sababu ya kusimamia maadili ya kazi yake ya uhandisi. Hiyo ndiyo gharama ya kuwa mwaminifu katika kazi.”  Mwisho wa kunukuu.
Ukiangalia nukuu hii kwa undani ni dhahiri shahiri, Mhandisi Patrick Mfugale na marehemu Mhandisi Leopord Mjungi ni wabobezi katika taaluma yao. Waadilifu na wazalendo. Waliheshimu kazi yao, walithamini utu wao, wamejali haki za Watanzania na wameipenda nchi yao.

Sababu hizo ziliwafanya kuwa aghali katika kuuza utu na taaluma yao. Mhandisi Mfugale alihimili vishindo, lakini Mhandisi Mjungi hakumudu vishindo, pamoja na katibu mkuu wao kuzuia vishindo hivyo, Mhandisi Leopord Mjungi alijidhulumu nafsi yake. Kifo kilimfika, Mungu amsamehe makosa yake na azidi kumuweka mahali pema peponi. Amina!
Marehemu Mhandisi Leopord Mjungi alisimamia maadili ya kazi yake ya uhandisi. Hii ni sifa bora na aghali kwa mtu kujisimamia. Je, katika muktadha huu hatuguswi au hatuwashwi na tendo hili?
Serikali, chama, Bodi ya Wahandisi, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu (TUGHE), taasisi za haki za binadamu na Watanzania tunaguswa au hatuguswi? Tutafakari.