Ninajua kuwa hautanielewa nikisema umenisahau kwa sababu haujapata nafasi ya kuja kunitembelea hapa kwangu na kuona jinsi ambavyo fuko la alizeti lilivyogeuka kuwa mto wa kulazia kichwa changu huku nikiwaza rundo la mahindi nitaliuza wapi, najiuliza, mihogo niliyonayo niwakabidhi nguruwe au nigawe kwa wagonjwa?
Mheshimiwa Waziri, nimehemewa mawazo kwa sababu najua haujui ni kiasi gani sisi wakulima tunaumizwa na mzigo wa mashamba na mazao.
Hivyo nimeamua nitumie fursa hii kukukumbusha shida tuliyonayo wakulima. Kila siku huu ni wimbo wa taifa kwamba kilimo ndicho kila kitu na kwamba kilimo kinatoa fursa nyingi kwa vijana kujiajiri.
Katika hili lazima nikiri uongo mkubwa kwa vijana kulima, na hauwezi kuwashawishi kwa sababu wanatuona sisi wazee wakulima jinsi ambavyo tunahangaika kuhusu mahali pa kuuza na hata kuhifadhi mzigo mkubwa wa mazao baada ya kutoka mashambani.

Si kweli kwamba kila mtu anajua hali halisi ya kilimo, watu wengi wanazungumzia kilimo kwa kupitia mazungumzo lakini si kwa kushika jembe na kuona radha ya kuchimba ardhi na hatimaye kupata mazao.
Watu wengi wanayaona mazao yakiwa sokoni lakini si kweli kwamba kila mtu anaujua uchungu wa shamba kuanzia mnunuzi dalali hadi mlaji.
Mheshimiwa Tizeba, wakulima wako tunakuangalia kwa jicho la hasira, tunalima katika jua kali sana, tunalinda mazao kwa kuweka dawa na kuyahifadhi, na mazao yetu ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku, lakini kila siku inayosogea hali inazidi kuwa mbaya kwa wakulima.

Zamani kama unakumbuka nchi yetu ilitenga kabisa mikoa ambayo ilikuwa ikilima sana, na hatukupata kuwa na njaa katika taifa letu, ni mwaka 1974 na mwaka mmoja baada ya vita ndio nchi iliingia katika tatizo la njaa, mwaka 1974 ilikuwa ni kutokana na ukame, hatukupata mvua na baada ya vita ilitokana na kupambana na nduli Idd Amin.
Sasa hivi naiona hali ya taifa kukumbwa na baa la njaa na kusababisha uchumi kuyumba. Taifa linapoingia katika njaa ni suala la mwaka mzima kuwa na njaa, kwa sababu wakulima wanakuwa ama hawajalima kabisa au wameuza hadi akiba ya chakula chao.

Kuna msemo kuwa adui yako muombee njaa, hauna sababu ya kumpiga, hali ilivyo naona kama taifa letu linaombewa njaa na maadui zetu wengine kama si kwamba tumeamua kujiombea njaa wenyewe. Kwa hali ilivyo, naona jinsi ambavyo sisi wakulima tutakavyoamua kuacha kulima na taifa litakapoingia katika mtego wa njaa.
Mheshimiwa Tizeba, naona jinsi ambavyo umetusahau wakulima wako katika suala zima la bei ya mazao na sasa tumekuwa watumwa kwa walaji, bei wanatupangia wao na pengine kutukopa.
Sisi wakulima tuko mashambani hatujui nini kinachoendelea huko mliko wenye dhamana na sisi, lakini ukweli ni kwamba mmefungua soko kwa watu wa nje na kutufungia soko watu wa ndani.
Tuna mazao ghalani na tunataka kuyauza lakini nje kuna mazao kama yetu kutoka kwa watu wengine wa nje ya nchi yetu, mnatulindaje sisi wakulima wenu, mnataka kutuingiza katika soko huria ili tushindane na wenzetu ambao kwa namna moja ama nyingine wanachangiwa sana juhudi zao na serikali zao?

Kilimo ni kazi ngumu sana na inatakiwa iwe sehemu ya kuwekwa ruzuku ya kutosha, lakini wengi wetu ni kama yatima ambao tunapambana kivyetu ili tuuze na kufanya mambo mengine kwa biashara ya mazao.
Tunapaswa kulipa ada za watoto wetu, kupata matibabu na kununua mahitaji muhimu ya kila siku kama ambavyo wafanyakazi wanafanya kupitia mishahara yao.
Lakini kwa mwendo huu wa kuacha soko la mazao yetu likiwa linashindana na mataifa ya nje ni kutuonea, hatuna namna nyingine, tunanunua mbolea kwa bei ya juu sana, tunamwagilia kwa gharama kubwa, tunahifadhi na kulisha dawa kwa gharama kubwa, lakini cha ajabu tunauza kwa bei ya nusu ya gharama zetu.

Ni wakati sasa wa kuacha kuimba ngonjera, tunaomba tusaidiwe, tuangaliwe kwa jicho la pili na muhimu kama kilimo kilivyo kuwa uti wa mgongo, tulilima zamani na tulipata faida ya kilimo kwa kupitia vyama vya ushirika, serikali ilithamini na kuweka ruzuku katika zana za kilimo na pembejeo, hatukuwa yatima wa kujitegemea wakati serikali ipo.
Mheshimiwa Tizeba, nakukaribisha katika nyumba ya mkulima yeyote ili uone jinsi ambavyo amebaki na mazao ya mwaka jana akishindwa kuuza kutokana na kudorora kwa bei.
Hata akiuza hawezi tena kugharamia kilimo cha mwaka huu. Nakukaribisha katika masoko uone ambavyo mazao kutoka nje yanavyotuua wakulima wa ndani.
Karibu Kipatimo utuangalie tulivyo.

Wasalamu,
Mzee Zuzu,
Kipatimo.

Please follow and like us:
Pin Share