NA MWANDISHI WETU

Alexis Sanchez anaweza kuwa ameokoa kibarua cha Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho, kufukuzwa mapema wiki hii baada ya kuwafunga Newcastle United 3-2 mwishoni mwa wiki.
Endapo Jose Mourinho ‘The Special One’ atafungashiwa virago, Meneja wa Tottenham, raia wa Argentina, Mauricio Pochettino, anatajwa kurithi mikoba yake.
Mourinho amekalia kuti kavu kutokana na timu yake ya Man United kutofanya vizuri na uongozi wa timu hiyo hauko tayari kuona Chelsea, Liverpool au Manchester City wanachukua kombe huku wao wakibaki kuwa wasindikizaji.
Kama Mashetani Wekundu watamtimua Mourinho, watatakiwa kumlipa kiasi cha pauni milioni 12 kama gharama za kuvunja mkataba, kiasi hicho cha fedha ni sawa na mshahara wake wa mwaka mzima.
Jose Mourinho alisaini mkataba mpya na United utakaomweka klabuni hapo hadi mwaka 2020, lakini klabu hiyo ili kuogopa hasara waliamua kuweka kipengele katika mkataba wake ambacho hawatampa pesa yote ya mkataba wake kama utaishia katikati.

Mourinho ameiongoza Man United katika michezo yake 120, huku akishinda michezo 74, suluhu 25 na amepoteza michezo 21. Manchester United haijashinda mataji makubwa, ukiondoa lile la Europa League tangu aondoke kocha aliyedumu klabuni hapo kwa miaka zaidi ya 20, Sir Alex Ferguson.
Manchester United imetumia fedha nyingi kupata makocha tangu aondoke Sir Alex Ferguson. Hapa chini ni orodha ya makocha na fedha zilizotumika.
David Moyes: Ndiye alikuwa mrithi wa Sir Alex Ferguson.  Alipojiunga tu alipewa pesa akamnunua Marouane Fellaini kwa pauni milioni 27.5. Fellaini alinunuliwa kutoka Everton na Juan Mata, Chelsea.
Louis Van Gaal: Baada ya Moyes kutimuliwa kutokana na timu kufanya vibaya, nafasi yake ilichukuliwa na Mdachi Louis Van Gaal, ambaye aliwanunua Ander Herrera kutoka Athletic Bilbao, Luke Shaw kutoka Southampton na Marcos Rojo kutoka Sporting.

Wengine walionunuliwa na Mdachi huyo ambaye pia hakudumu klabuni hapo ni pamoja na winga, Angel Di Maria, aliyenunuliwa kwa pauni milioni 60 kutoka Real Madrid na beki Daley Blind, aliyenunuliwa kwa pauni milioni 14 kutoka Klabu ya Ajax ya Uholanzi.
Wachezaji hao kwa jumla waliigharimu Manchester United pauni milioni 149. Msimu wa 2015/2016 aliwanunua Memphis Depay kwa ada ya pauni milioni 25 kutoka Klabu ya  PSV Eindhoven ya Uholanzi, Matteo Damian kwa ada ya pauni milioni 12.7 kutoka Torino ya Italia na Bastian Schweinsteiger alinunuliwa kwa ada ya pauni milioni 6.5 kutoka Bayern Munich.

Wengine ni Morgan Schnedelin, kiungo aliyenunuliwa kwa pauni milioni 25 kutoka Southampton pamoja na Anthony Martial, aliyenunuliwa kwa pauni milioni 58 kutoka Klabu ya Monaco ya nchini Ufaransa.
Jose Mourinho: Baada ya kutimuliwa Van Gaal, Mourinho akachukua mikoba yake, akaanza kusuka kikosi chake kwa kuwanunua Eric Bailly kwa ada ya pauni milioni 30, kutoka Villareal ya Hispania, Ibrahimovic aliyesajiliwa kama mchezaji huru kutoka kwa mabingwa wa Ufaransa – Klabu ya PSG na Henrikh Mkhitarian, aliyesajiliwa kwa ada ya pauni milioni 27, kutoka Klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani. Vilevile Mourinho alimsajili Paul Pogba kwa ada ya pauni milioni 89 kutoka kwa mabingwa wa Italia, Juventus. Jumla alitumia pauni milioni 146.

Katika msimu wa 2017/2018 akamnunua Romelu Lukaku kwa ada ya pauni milioni 75 kutoka Klabu ya Everton, Victor Lindelof aliyenunuliwa kwa ada ya pauni milioni 30 kutoka Klabu ya Benfica nchini Ureno na Nemanja Matic aliyenunuliwa kwa pauni milioni 35 kutoka Klabu ya Chelsea ya Uingereza.
Katika msimu wake wa pili Old Trafford, Mourinho alitumia kiasi cha pauni milioni 140.

Kwa ujumla makocha hawa watatu wametumia zaidi ya pauni milioni 600 tangu Ferguson aondoke na hii inawafanya United kutokuwa na huruma pale kocha anaposhindwa kuwaletea matokeo mazuri ya uwekezaji wao.

Mtiririko wa matukio ya Mourinho

•Meneja wa Manchester United Jose Mourinho ameongoza klabu hiyo katika mechi nne za ushindani nyumbani bila ushindi kwa mara ya kwanza katika maisha yake kama kocha.
•Manchester United hawajashinda mechi zao nne za karibuni zaidi Old Trafford tangu Desemba 2015 (chini ya Louis van Gaal).
•Mechi tatu kati ya nne za karibuni zaidi za Manchester United dhidi ya klabu za Hispania, Klabu Bingwa barani Ulaya zilikwisha kwa sare ya 0-0.

Mechi za hivi karibuni

Manchester United waliwakaribisha Newcastle United katika Uwanja wa Old Trafford Jumamosi na kuwafunga magoli 3-2.
Mechi yao inayofuata Ligi ya Mabingwa barani Ulaya ni mechi ya nyumbani dhidi ya Juventus, mechi hiyo itachezwa Oktoba 23.

Please follow and like us:
Pin Share