NA MOSHY KIYUNGI

Jina la Sam Mangwana si geni masikioni mwa wapenzi wa muziki wa dansi Afrika Mashariki na Kati.
Ni mwanamuziki mwenye vipaji vya utungaji na kuimba nyimbo za muziki wa dansi akitokea Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mangwana alizaliwa Februari 21, 1945 katika mji wa Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wazazi wake walikuwa wahamiaji ambapo baba yake alikuwa raia kutoka nchini Zimbabwe, wakati mama yake ni raia wa Angola.
Bendi yake ya kwanza kupiga muziki ilikuwa ni Festival des Maquisards kisha African All Stars.

Mangwana alikuwa mwanachama katika bendi ya T.P. OK Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Franço Luambo Makiadi.
Vilevile alikuwa katika bendi zilizokuwa zikiongozwa na Tabu Ley Rochereau za African Fiesta, African Fiesta National na Afrisa International.
Weledi wake katika muziki ulijulikana zaidi mwaka 1963, alipokuwa akipiga muziki wa rhumba katika bendi ya African Fiesta iliyokuwa ikimilikiwa na kuongozwa na Tabu Ley Rochereau.
Baadaye Sam Mangwana alivuka Mto Kongo akaingia katika mji wa Brazzaville, nchini Kongo.

Nchi hizo za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Kongo Brazzaville zinatenganishwa na Mto Kongo.
Alipofika mjini humo aliunda bendi ya Los Batchichas, ambayo haikudumu kwa kipindi kirefu.
Sam Mangwana aliwahi kufanya kazi katika bendi zilizoanzishwa za Negro Band na Orchestra Tembo mjini humo.
Baadaye akavuka Mto Kongo kurejea kwao katika Jiji la Kinshasa, ambako aliungana na Tabu Ley kupiga muziki katika bendi ya African Fiesta National.
Mwaka 1967, Mangwana kwa mara nyingine aliamua kuunda bendi yake akaipa jina la Festival des Maquisards.

Bendi hiyo alisheheni wanamuziki wakiwemo mwimbaji Dalienst, mpiga  gitaa Dizzy Mandjeku na Michelino aliyekuwa akipiga gitaa la solo.
Miaka miwili baadaye, Sam Mangwana aliondoka tena akaenda kujiunga na mpiga gitaa maarufu aliyekuwa akiitwa Jean Paul ‘Guvano’ Vangu, hadi mwaka 1972.
Mwaka huohuo wa 1972, alijiunga katika bendi ya T.P. OK Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Franco Luambo Makiadi.
Aidha, Mangwana alishirikiana vema kuimba nyimbo zilizotungwa na mpiga gitaa wa bendi ya T.P. OK Jazz, Simaro Massiya Lutumba. Umaarufu wake ukapanda haraka wakati huo.
Ushirikiano wake na Simaro, waliweza kuachia vibao vikali vya ‘Ebale ya Zaire’, ‘Cedou’ na ‘Mabele’.

Mangwana aliiacha bendi ya T.P. OK Jazz na kurudi tena kwenye bendi ya Tabu Ley ya Afrisa Interantionale.
Hata hivyo hakudumu kwa kipindi kirefu katika bendi hiyo, akaenda katika mji wa Abidjan, nchini Côte d’Ivoire, Afrika Magharibi.
Mwaka 1978 Mangwana pamoja na wanamuziki wengine waliunda bendi iliyoitwa African All Stars.
Mwaka mmoja baadaye bend