Mheshimiwa Kangi Lugola,
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, sisi
askari wastaafu wa Jeshi la Polisi
tunakupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya
ingawa kuna changamoto za hapa na pale.
Tunakutia moyo na tunaomba Mungu
akuzidishie hekima katika utendaji wako.
Ndugu Waziri, Wizara ya Mambo ya Ndani
ya Nchi ni kubwa. Inaundwa na Jeshi la
Polisi, Jeshi la Magereza, Jeshi la
Zimamoto na Uokoaji; na Uhamiaji.
Kutokana na ukubwa huo, wakati mwingine
si rahisi kufahamu kila jambo pengine
mpaka ujulishwe.
Ndugu Waziri, sidhani kama unatambua

kuwa hadi sasa karibu askari Polisi wote
tuliostaafu mwaka 2017 bado tunaishi
makambini kutokana na kutolipwa pesa za
kusafirisha mizigo yetu kwenda makwetu.
Kila tunapouliza kwa viongozi wetu mikoani
tunajibiwa kifupi tu kuwa makao makuu
hawajatoa pesa. Baadhi ya wastaafu ambao
wamebahatika kulipwa mafao yao
walijisafirisha wenyewe.
Ndugu Waziri, kama tulivyotangulia kusema
kuwa hata Jeshi la Magereza lipo chini
yako, cha kushangaza wenzetu wa
Magereza wote waliostaafu mwaka 2017 na
mwaka huu wa 2018; na hata
wanaotazamiwa kustaafu Oktoba, 2018
wameshalipwa pesa za kusafirisha mizigo.
Ndugu Waziri, sisi Polisi kuna tatizo gani,
wakati wote ni wa baba mmoja na katibu
mkuu ni wetu sote?
Ndugu Waziri, ebu fikiria mtu amestaafu
lakini bado anaendelea kuishi kambini.
Wewe uliwahi kuwa askari Polisi, hakuna
jambo usilolifahamu.
Tunateseka. Tunaomba tupewe fedha zetu

ili twende makwetu.
Asante,
Wastaafu wa Jeshi la Polisi.

Mwisho

By Jamhuri