Sao Paulo, Brazil

Vyombo vya usalama nchini Brazil
vimekamata fedha taslimu na mali za
kifahari za mtoto wa Rais wa Equatorial
Guinea, Teodoro Obiang Nguema, vyote
vikiwa na thamani ya dola milioni 16 (Sh
bilioni 36).
Miongoni mwa vito vya thamani
vilivyokamatwa ni saa zilizokuwa kwenye
mabegi ya msafara wa mtoto huyo.
Teodoro Obiang, ambaye ni Makamu wa

Rais wa Equatorial Guinea, anaelezwa
kuwa ni mjivuni na mwenye mbwembwe
nyingi.
Alikamatwa na vitu hivyo kwenye ndege
yake binafsi alipowasili Brazil.
Fedha na saa hizo vilikamatwa ndani ya
mabegi kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Viracopos jijini Sao Paulo.
Polisi walikamata dola milioni 1.5 (zaidi ya
Sh bilioni 3) taslimu kwenye begi moja na
saa zenye thamani ya dola milioni 15 (zaidi
ya Sh bilioni 30).
Maofisa wa Serikali ya Equatorial Guinea
wamenukuliwa wakisema fedha hizo
zilikuwa kwa ajili ya matibabu ya Obiang
jijini Sao Paulo.
Saa zilikuwa na vifupisho vya majina yake,
na ilielezwa kwamba zilikuwa kwa ajili ya
matumizi binafsi.
Mwaka jana mahakama moja nchini
Ufaransa ilimtia hatiani Obiang kutokana na
udanganyifu na kumhukumu kifungo cha
miaka mitatu. Alitiwa hatiani licha ya
kutokuwapo mahakamani.

Mali zake, zikiwamo nyumba zilizoko katika
Mtaa wa Foch jijini Paris zilitaifishwa.
TV Globo ilitangaza kuwa makamu huyo wa
rais alikuwa pekee mwenye hadhi ya
kidiplomasia kwenye msafara wake.
Kwa sheria za Brazil, ni makosa kuingia
nchini humo ukiwa na fedha taslimu
zinazozidi dola 2,400.
Serikali ya Equatorial Guinea haijatoa
taarifa rasmi kuhusu tukio hilo.

..tamati…

By Jamhuri