image12Simu yenye namba 0768 299534 inaita. Kwenye orodha ya namba nilizonazo haimo. Ni namba mpya.

Napokea, na mara moja nasikia sauti ya unyonge ikilitaja jina langu. Bila kuchelewa anataja jina lake.

‘Naitwa Mangazeni, nipo hapa Butiama, naomba ndugu yangu unisaidie kufikisha kilio changu kwa walimwengu ili waweze kunisaidia.”

Anaendelea: “Naomba uweze kufika hapa nyumbani kwangu uone mtoto wangu anavyoteseka. Nimemhudumia hadi nimeishiwa kabisa. Sina uwezo wa kifedha, kwa hiyo nimekwama kumnunulia dawa, chakula na huduma nyingine za kumwezesha kuishi kwa siku ambazo Mungu atakuwa amemjaalia.”

Maneno haya yananichoma moyoni. Bahati nzuri nina safari mkoani Mara. Namhakikishia kuwa nitafika nyumbani kumuona huyo mgonjwa.

Siku imewadia. Nawasili mkoani Mara. Nina majukumu kadhaa, lakini lile la mgonjwa aliye kitandani kwa mwaka wa tatu sasa linanikosesha amani.

Nampigia simu Mangazeni. Namweleza nipo Butiama. Ananielekeza mahali anakoishi. Nyumba yake iko katika Kitongoji cha Makore ndani ya Kijiji ambacho sasa ni Wilaya ya Butiama.

Muda ni alasiri. Nawakuta wenyeji wakiwa wameketi kivulini. Mangazeni yu miongoni mwao. Huyu ndiye baba mzazi wa mtoto aliyekwama kitandani kwa miaka mitatu sasa.

Baada ya salamu, Mangazeni ananikaribisha katika moja ya nyumba ndogo zilizo hapa nyumbani kwake. Ni nyumba iliyoezekwa kwa bati, ikiwa na vyumba viwili. 

Naam, nakaribia. Naye anasema: “Karibu, mgonjwa mwenyewe ndiye huyu.”

Namwuliza kama mgonjwa anaweza kuzungumza. Kabla hajajibu, mgonjwa anajibu: “Naweza kuzungumza. Shikamoo. Naitwa Said Ibrahim Mangazeni, umri wangu ni miaka 30 sasa.”

Pengine kutokana na hali ya hewa na joto kiasi, kifua amekiacha wazi, lakini kuanzia kwenye nyonga hadi miguuni amefunikwa shuka.

Baba anaanza kunieleza: “Alipata ajali ya kuanguka kwenye shimo lenye urefu wa futi 25. Shimo lipo hapo nyuma.

“Ilichukua muda kumtoa humo, na ilikuwa bahati tu ndugu yetu mmoja ndiye aliyesikia sauti ya mtu anayeomba msaada. Nakumbuka ilikuwa Mei 19, 2014. Tulipomtoa shimoni tukampeleka Hospitali ya Butiama, hapo ikaonekana tatizo ni kubwa zaidi. Tukampeleka DDH Bunda. Hapo nako wakasema tatizo ni kubwa. Akapewa rufaa kwenye Bugando, Mwanza. Hapo akapimwa na kuonekana mgongo umevunjika. Alilazwa Bugando kwa mwaka mmoja akiwa anahudhuria kliniki, lakini mwishowe ikaonekana hakuna matumaini ya kupona.

“Baada ya mwaka mmoja nikamhamishia kwa dada hapo hapo Mwanza, lakini baadaye ikaonekana hakuna matumaini ya kupata uponyaji katika ngazi hiyo ya matibabu. Tukaamua kurejea hapa nyumbani.”

Wakati baba akizungumza maneno haya, kimya kikamfika. Akawa analengwalengwa na machozi. Kuona hivyo, Said akiwa amelalia ubavu, akasema: “Hapa nilipo siwezi kusogea hadi nibebwe. Kuanzia hapa (nyongani) hadi miguuni kote sisikii kitu. Nikichomwa hata sindano sisikii kitu kabisa.

“Natokwa na haja kubwa bila kujijua. Haja ndogo ndiyo natolea hapa (anafungua shuka na kuonesha sehemu ya chini ya kitovu iliyotobolewa na kuwekwa mpira). Haja kubwa inatoka lakini sijui wakati inapotoka.

“Naomba baba (mwandishi wa makala hii) unisaidie niende hospitali kubwa.”

Maneno ya Said yanazidi kunitia simanzi. Baba yake (Mangazeni) anaongeza kusema: “Uwezo sina, laiti  kama ningekuwa nao, tayari nimeshampeleka kwa wataalamu wakubwa zaidi hata nje ya nchi. Sina uwezo kabisa.

“Hapa alipo anahitaji dawa na chakula. Vifaa vya tiba anavyotumia ni fedha nyingi, nimejitahidi nimefikia hatua ya kukwama kabisa. Nahitaji wafadhili waweze kunisaidia. Naomba wajitokeze wanisaidie  kama wanavyosaidia binadamu wengine.”

Maneno haya ya baba yanamfanya Said aonekane kulengwalengwa na machozi. Namwuliza hali aliyokuwa nayo kabla ya kufikwa na ulemavu huu. Anajibu: “Nilikuwa fundi seremala, na pia nilipitia mgambo. Nimehitimu kidato cha nne katika Sekondari ya  Victoria mjini Musoma mwaka 2005.

“Nilikuwa nasoma Chuo cha Ardhi, ikabidi nisimame nikiwa field (mafunzo kwa vitendo) ya mwisho. Ajali hii imemaliza kabisa matumaini yangu yote.”

Baada ya maneno hayo, na kwa kutaka kunithibitishia ukubwa wa tatizo alilo nalo Said, baba yake anamfunua sehemu za siri na kwenye makalio! Ni hali ya kusikitisha. Kwa sababu ya kulala kwa mwaka wa tatu sasa, vidonda vimeenea sehemu kubwa.

“Hivi vidonda vinatakiwa kusafishwa kwa dawa kila siku, vingine vimeanza kuwa mashimo kabisa. Tukikosa dawa siku moja tu hali inakuwa mbaya sana, ndiyo maana naomba jamii inisaidie,” anasema Mangazeni.

Baada ya mazungumzo yetu, na kwa kuona Said ameshachoka, najiandaa kuaga ili nitoke nje. Wenzangu nilionao, pamoja na baba yake wanatangulia kutoka. Nakuwa wa mwisho. Kabla sijatoka nje, ananitazama kwa jicho la huruma kweli kweli. Ananiambia: “Baba, naomba unisaidie. Nisaidie baba. Mungu atakubariki. Fikisha habari hizi kwa walimwengu wengine ili nipate msaada.

“Ninavyoona ni kuwa Mungu alikuwa anapenda bado niendelee kuishi, lakini kwa kukosa dawa na chakula naweza kufa mapema. Nisaidie baba.

“Napata shida sana. Maumivu ni makali. Hayaelezeki. Maumivu niliyonayo ni ya kuanzia hapa (nyongani) kuja juu. Huku chini hapo unaona naoza, sisikii kabisa maumivu maana sina mawasiliano yoyote ya fahamu.

“Naomba nipate msaada ili Mungu atakaponiita, basi aniite kwa sababu maradhi haya si ya kupona, lakini nisife kwa kukosa dawa za maumivu, hizi za mirija ya haja ndogo, za vidonda na chakula. Mbaya zaidi, chakula ninachotakiwa kula ni kile ambacho ni laini. Huku kwetu chakula kikuu ni ugali, sasa utaona ni vigumu mimi kupata aina ya chakula kilichopendekezwa na madaktari.”

Maneno haya anayahitimisha kwa kujiinamia akisema: “Mungu alikuwa bado ananipenda, nisaidieni jamani.”

Kauli hii inanifanya nisiendelee kuwa karibu naye. Natoke nje ya chumba hiki alimolala Said nikibubujikwa na machozi. Ni tukio la kuhuzunisha. 

Julai 27, saa 5:06 Said aliniletea ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu yake. Aliandika haya: “Mungu akusimamie, usichoke kunipigania, akupe moyo na nguvu ya ushindi, aondoe roho ya kukata tamaa, akufanyie wepesi katika maisha ya shughuli zako. By Said, mgonjwa -Butiama.”

Nilitafakari nimjibu nini, lakini nikapita katika Zaburi 40:18 na kukutana na maneno haya ya kumtia faraja yasemayo: “Nami ni maskini na mhitaji, Unikumbuke, ee BWANA. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu; ee Mungu, wangu, usikawie!”

Nikasema wausomao ujumbe huu warejee maandiko ya Kitabu cha Zaburi 41: 1-4 yasemayo: “Heri mtu amkumbukaye mnyonge; Siku ya shida, BWANA atamwokoa. BWANA atamlinda na kumtunzia uzima, atamjalia kuwa na heri duniani, wala hatawaacha adui zake wamtende wapendavyo. BWANA atamtegemeza ataabikapo kitandani, atamrudishia nguvu awapo mgonjwa kitandani.” 

Kwa wale wenye kuguswa na matatizo ya kijana Said, wanaweza kuwasiliana naye moja kwa moja kwa simu: 0766 951012; au namba ya baba yake, Mangazeni: 0768 299534.

2019 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!