foleniMkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania, Kamanda Mohamed Mpinga, amesema ni uonevu mkubwa kumtoza mtu nauli kubwa tofauti na ile iliyoelekezwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA).

Kamanda Mpinga amewataka wananchi kuwa na msimamo wa pamoja wa kutokukubali kutozwa nauli kubwa, badala ya kuwapa jeuri madereva na makondakta wenye kuendekeza tamaa ya fedha. “Sina uhakika kama viwango vya nauli vimepanda na wanaotoza nauli kubwa wanaeleweka, sasa hivi kwa kushirikiana na Sumatra tunalifuatilia suala hili katika maeneo yote ya jiji na wale tutakaowakamata tutawachukulia hatua za kisheria,” anasema Kamanda Mpinga.

Kadhalika, bosi huyo wa matrafiki amewataka wananchi kutoa taarifa mapema kuhusu mabasi yanayotoza viwango vikubwa vya nauli tofauti na iliyoelekezwa na Sumatra na ukiukwaji mwingine wa sheria za barabarani unaohatarisha maisha ya watu.

Hatua ya Kamanda Mpinga kutoa amri hiyo inatokana na wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kulalamikia vitendo vya wamiliki wa daladala katika baadhi ya maeneo kutoza nauli kubwa tofauti na ile iliyotangazwa na Sumatra.

Wakazi hao kwa nyakati tofauti wameieleza JAMHURI kwamba wameshangazwa na vitendo vya baadhi ya makondakta wa daladala kuwatoza nauli kubwa ambayo haijatangazwa, na wanapohoji uhalali wa nauli hizo wanaelezwa kwamba hayo ni maelekezo ya Sumatra.

Kwa mfano, viwango vipya vya nauli ni Sh 500 kutoka Tegeta hadi Makumbusho badala ya Sh 400 iliyokuwa ikitozwa awali na kuandikwa ubavuni mwa daladala hizo yakiwa ni maelekezo ya Sumatra. Lakini baadhi ya daladala zimekuwa zikitoza nauli ya Sh 1,000 kutoka Makumbusho hadi Tegeta kuanzia muda wa saa moja jioni na kiasi hicho hicho kinatozwa kwa baadhi daladala zitokazo Ubungo hadi Tegeta.

Viwango hivyo vimedumu kwa muda mrefu huku baadhi ya wananchi wakilalamikiana wao kwa wao kwamba ni chanzo cha kuendelea kutozwa nauli hizo kinyume na maelekezo ya Mamlaka hiyo.

Joyce Lucas, aliyejitambulisha kuwa ni mkazi wa Tegeta Nyuki, anasema kutozwa nauli kubwa za daladala kwa wakazi wa jiji hili ni jambo la kawaida na limezoeleka kutokana na wao kukubaliana na makondakta na kulalamika baada ya kulipa nauli hizo.

“Utozaji nauli holela unatuumiza sana na tunapolalamika baadhi ya abiria wenzetu wanatoa majibu ya hovyo kwamba kama huna kiasi hicho kilichotangazwa na kondakta ushuke, inatulazimu kulipa tu kutokana na mazingira magumu ya usafiri,” anasema Joyce katika mahojiano na JAMHURI, katika kituo cha daladala cha Makumbusho.

Naye Ramadhan Rajabu, mkazi wa Kunduchi, anasema zaidi ya miezi miwili sasa  wanatozwa nauli mpya za daladala wakati hakuna mabadiliko yoyote ya ongezeko au punguzo la nauli hizo, lililotolewa na Sumatra kupitia vyombo vya habari kama inavyofanya mara kwa mara inapotoa taarifa zake.

Anasema ubavuni mwa daladala hizo kuna kiasi cha nauli elekezi iliyotolewa na Mamlaka hiyo, lakini ukiingia ndani utaona limebandikwa karatasi linaloelekeza nauli mpya kutoka Mamlaka hiyo hiyo. Hata hivyo, anasema hilo linachangiwa na watu kufanya kazi kwa mazoea kama watawala hawapo na hakuna anayejali. Jioni wanatozwa nauli ya Sh 1,000 badala ya Sh 400 au Sh 600 kama zilivyoelekezwa.

“Tunalipa viwango vya nauli ambavyo havijaidhinishwa na Sumatra, tunaonewa kwa sababu ya ujinga wetu, na abiria wengine wanashabikia wizi huo, kama tungekuwa na umoja hakuna hata mmoja ambaye angetozwa nauli kubwa,” anasema.

Nao baadhi ya abiria katika kituo cha daladala cha Sinza (Simu 2000) wameieleza JAMHURI kwamba kutokana na kero ya usafiri iliyopo katika maeneo yote ya jiji, madereva na makondakta kwa tamaa ya kupata fedha nyingi wamekuwa na tabia ya kutoza nauli kubwa kadiri wanavyotaka.

Wanasema licha ya utaratibu huo kudumu kwa muda mrefu, hakuna mwananchi anayethubutu kutoa taarifa kwenye vyombo husika na hivyo kuwapa jeuri madereva kufanya watakavyo huku wakijua wanavunja sheria zilizowekwa.

Kwa upande wake, Mwanahamisi Juma, mkazi wa Mwananyamala, ameilalamikia Sumatra kwamba inafahamu haya yote yanayofanyika na jinsi wananchi wa kipato kidogo wanavyonyonywa na wamiliki wa daladala ambao hawako tayari kutii sheria zilizowekwa katika utoaji wa huduma ya usafiri lakini imeendelea kufumbia macho vitendo hivyo.

“Sumatra wanaelewa haya yote lakini wameamua kuziba masikio yao na kufurahia mateso haya tunayoyapata kila siku katika vyombo hivyo vya usafiri,” anasema.

Meneja wa Mawasiliano ya Umma wa Sumatra, David Mziray, anasema Mamlaka hiyo haijapandisha nauli za daladala na kiwango kinachotozwa ni kile kilichoandikwa ubavuni mwa kila daladala.

Akielezea wale wanaotoza nauli nyakati za jioni kwa Sh 1,000 badala ya Sh 400 au Sh 600 kama ilivyoelekezwa, anasema taarifa hizo wanazo na kwamba hatua zitachukuliwa mara moja dhidi ya wahusika. “Tunawaomba tena wananchi watoe taarifa mara moja kupitia namba zetu za simu ambazo zipo kila mahali, kuhusu madereva wanaotoza nauli kubwa, kukatiza njia na ukiukwaji mwingine wa sheria ili hatua zichukuliwe mara moja.

“Kwa daladala ziendazo Tegeta na Bunju na kutoza nauli kubwa, wahusika wote waache kufanya hivyo, maofisa wetu wameanza kufuatilia suala hilo katika vituo vyote, ikiwa ni pamoja na Makumbusho, Ubungo na Tegeta,” anasema Mziray.

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Daladala wa Dar es Salaam (DACOBOA), Sabri Mabrouk, anasema hana uhakika kama nauli za daladala kutoka Makumbusho kwenda Tegeta zimepanda, na suala hilo watalifuatilia ili kujua kama liliridhiwa na Sumatra au ni mbinu chafu za baadhi ya wamiliki wa daladala hizo.

Mabrouk anasema kwa daladala zinazowatoza wananchi viwango vikubwa vya nauli hadi kufikia Sh. 1,000 ni uhuni ambao haupaswi kufumbiwa macho.

“Wanaotoza nauli kubwa za daladala tofauti na zile zilizoelekezwa na Sumatra kwa njia za Makumbusho hadi Tegeta, na Ubungo hadi Tegeta kwa nyakati za jioni haikubaliki na huu ni uhuni,” anasema mwenyekiti.

Hata hivyo, amewataka wananchi kutoa taarifa mapema zinazohusu kupandishwa viwango vya nauli tofauti na maelekezo ya Sumatra kwa maofisa wa Mamlaka hiyo na Jeshi la Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kupungua bei ya mafuta, wadau na wananchi kwa ujumla walitoa maoni yao kuhusu haja ya kutathmini upya viwango vya tozo mbalimbali katika huduma za usafiri wa nchi kavu na majini.

“Kwa sehemu kubwa maoni ya wadau yalijikita katika haja ya kuangalia upya viwango vya nauli za mabasi kwa usafiri wa mijini na masafa marefu, lakini hoja iliyojitokeza ni gharama za uendeshaji kwa watoa huduma zilipungua kufuatia kushuka kwa bei za mafuta, hali inayoleta ulazima wa kushusha viwango vya nauli ili watumiaji wa huduma za usafiri na wananchi kwa ujumla wanufaike kutokana na punguzo hilo,” imeeleza taarifa iliyotolewa na Sumatra. 

Sumatra ina jukumu la kuridhia viwango vya tozo mbalimbali za usafiri na nauli ikiwa ni sehemu ya tozo hizo na katika kutekeleza hili, Mamlaka inafuata utaratibu wa kisheria ulioainishwa katika sheria inayounda Mamlaka hiyo na kufafanuliwa na kanuni za tozo za mwaka 2009.

 Utaratibu wa kisheria wa namna ya kushughulikia na kuridhia viwango vya tozo mbalimbali za huduma zinazodhibitiwa na Sumatra ni kuhakikisha kuwa uamuzi ambao unagusa umma unafanyika kwa uwazi na ushirikishwaji. Katika utaratibu huu mdhibiti ana jukumu la kuhakikisha kuwa maslahi ya watumiaji wa huduma na watoa huduma yanalindwa ili kukuza ustawi wa wananchi wa Tanzania kama ilivyoainishwa katika sheria za Mamlaka hiyo. Hata hivyo, viwango vya tozo za nauli mpya havikuhusu daladala ambazo ziliendelea kutoza nauli zilizowekwa awali kutokana na gharama kubwa za uendeshaji kwa watoa huduma.

Wakati Sumatra ikikana kuhusika na upandishaji wa nauli za daladala kinyemela, madereva wameitupia lawama Mamlaka hiyo kuwa ndiyo iliyoidhinisha viwango hivyo kwa daladala zinazofanya safari zake kati ya Makumbusho na Tegeta. Baadhi ya madereva waliohojiwa kuhusu nauli hizo mpya zilizoanza kutozwa zaidi ya miezi miwili iliyopita, wanasema zimetolewa kihalali na kilichokuwa kikifanyika ni kuwakumbusha abiria wanaopanda daladala hizo sambamba na kubandikwa tangazo la viwango vya nauli mpya kama lilivyotolewa na Mamlaka hiyo.

Wakati mvutano kuhusu kupanda kwa nauli kwa baadhi ya daladala ukichukua sura mpya na kuibua maswali kwa watumiaji wa huduma hiyo, imeelezwa utaratibu wa Sumatra pamoja na mambo mengine ni kuandaa mikutano ya wadau na mwombaji hutakiwa kueleza maombi yake kwa wadau ambao hupewa nafasi ya kuuliza maswali au kutoa maoni yao. 

 Kama utaratibu huo utafuatwa, Sumatra huridhia viwango kwa kuzingatia mambo yote yanayoathiri gharama za uendeshaji na mafuta ikiwa ni moja kati ya mambo yanayozingatiwa katika kukokotoa tozo zinazostahili kuridhiwa.

Mziray anasema mambo mengine yanayozingatiwa ni umuhimu  wa kuwa na huduma endelevu, kulinda maslahi ya watumiaji na watoa huduma kwa kuweka mizania sawa, gharama za uendeshaji ikiwa ni pamoja na mishahara, gharama za matengenezo, gharama za vipuri, matairi, gharama za ununuzi wa mabasi, riba kutokana na mikopo, gharama za bima, mafuta na vilainishi, gharama nyingine za kiutawala, kodi na tozo mbalimbali.

Si hayo tu bali pia viashiria vya kushuka kwa uchumi, mfumuko wa bei na kuporomoka kwa thamani ya shilingi na kujenga mazingira ya ushindani.  

Katikati ya Aprili mwaka huu, Sumatra ilipunguza nauli za mabasi ya mikoani huku ikitangaza kubaki kama zilivyokuwa zile za daladala baada ya ukokotoaji wake kuonesha tofauti ndogo ya punguzo kulinganisha na viwango vya sasa.

Ukokotoaji huo ulibainisha nauli ya daladala kwa umbali wa kilometa 10 kuwa Sh 376 badala ya Sh 400, Sh 448 badala ya Sh 450 kwa kati ya kilometa 11 hadi 15, Sh 485 badala ya Sh500 kwa kilometa 16 hadi 20, Sh 583 badala ya Sh 600 kwa kilometa 21 hadi 25 na Sh742 badala ya Sh 750 kwa umbali wa kilometa 26 hadi 30.

Mkurugenzi Mkuu wa Sumatra, Gilliard Ngewe, alieleza kwamba pamoja na kupungua kwa kiasi hicho, Bodi ya Wakurugenzi ya Sumatra iliridhia kuwa nauli zinazotumika sasa ziendelee ili kupunguza usumbufu.

Alieleza kwamba uamuzi huo unatokana na punguzo lililokokotolewa kuwa dogo ikilinganishwa na viwango vilivyopo sasa na iwapo vitapitishwa vitasababisha usumbufu katika malipo, na kusisitiza kuwa nauli kwa wanafunzi itaendelea kuwa Sh 200 kama ilivyo sasa.

Anasema Machi 9 walipokea maombi ya kushusha nauli kutoka kwa Baraza la Ushauri na Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Sumatra (Sumatra – CCC) likitoa hoja ya kushuka kwa bei ya mafuta na kodi ya forodha kwa mabasi mapya yanayoingia nchini kutoka asilimia 25 hadi 10.

Kufuatia hoja hiyo, Mkurugenzi huyo alieleza kwamba Bodi ya Wakurugenzi alibaini kuwa gharama za utoaji huduma za usafiri mijini zinapaswa kutazamwa kwa ujumla wake, ikiwa ni pamoja na punguzo la bei ya mafuta ili kufikia viwango vya nauli inayostahili.

By Jamhuri