Anaweza kuwa na upungufu wake, lakini ni ukweli kwamba Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ni mmoja wa viongozi wenye uamuzi na mbinu zinazoleta nuru ya kuwapo mabadiliko katika utendaji kazi miongoni mwa watumishi wa umma.

Nimefurahishwa na uamuzi wake wa kuwataka wafanyakazi wa forodha katika mpaka wa Tanzania na Zambia (Tunduma), kufanya kazi kwa saa 24 ili kumaliza msongamano wa malori mpakani hapo. Msongamano huo bila shaka yoyote, unachangia pia kuwapo msongamano wa malori bandarini na jijini Dar es Salaam.


Itakumbukwa kwamba Edward Lowassa, akiwa Waziri Mkuu, naye aliwaagiza wafanyakazi wa Bandari ya Dar es Salaam, kufanya kazi kwa saa 24 ili waukabili mlundikano wa kazi na ucheleweshaji utoaji na usafirishaji shehena. Kama ilivyo ada ya Serikali yetu, pamoja na ukweli kwamba agizo hilo lilikuwa jema, liliachwa likafa baada ya Lowassa kujiuzulu. Kwa hili la Mwakyembe, sina shaka nalo litakoma baada ya kuiacha wizara hiyo. Lazima tuwe na mfumo endelevu kwa mambo yenye tija kwa nchi yetu kama hili la Tunduma.


Lakini nisema kwamba wapenda usingizi hawapo Tunduma au mipakani pekee. Watumishi wa idara nyingi katika nchi hii ni wapiga usingizi.


Tanzania ndiyo nchi katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati ambayo watumishi na wananchi wake tunafanya kazi kwa nusu siku.


Tena basi, hata nusu siku yenyewe haifiki. Watumishi kila siku wana udhuru-kama hawakufiwa, basi wanauguliwa! Visingizo ni vingi mno.


Serikalini wachapakazi ni wachache. Mkubwa anaweza kuagiza watu fulani walipwe, lakini mhasibu kwa kiburi tu, akakwamisha. Walau tunaweza kuwatetea walio katika sekta binafsi na zisizo rasmi! Hao ndiyo wale ambao ukienda Kariakoo saa nane usiku utawakuta wakijibidisha kwa biashara na utoaji huduma. Hawana njoo kesho!


Tanzania ndiyo nchi ambayo abiria katika basi anaruhusiwa kusafiri kuanzia saa 12 alfajiri na mwisho wake ukawa saa 4 usiku! Pamoja na kujinadi kwetu kwamba tuna amani, Tanzania ndiyo nchi ambayo polisi wanaweza kuwazuia msipite Mlima Sekenke saa 5 usiku kwa sababu kuna majambazi! Kenya, Uganda au hata Rwanda ambako kumezagaa silaha na wahalifu, watu wanasafiri saa 24.


Wanachapakazi muda wote. Hakuna jambazi wala kibaka wa kuwasumbua barabarani. Vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania vimesalimu amri kwa majambazi na wahalifu wengine. Aibu.


Miji kama Kampala , maduka yanakuwa wazi hadi usiku wa manane. Biashara inaendelea bila hofu ya Joseph Konny wala wapuuzi wengine. Sisi hapa kuyakuta maduka ya Magomeni yakiwa wazi saa 4 usiku ni jambo la kumstaajabisha mpita njia. Hatuwezi kuendelea kwa staili hii.


Katika Uwanja wa Ndege unaoitwa wa “kimataifa” wa Julius Nyerere, ni aibu! Wanaosafiri alfajiri hawawezi kupata kahawa, chai wala soda.


Watalii wanaoondoka usiku au mapema alfajiri hawapati fursa ya kununua zawadi za mwisho-mwisho kwa ajili ya jamaa zao ughaibuni.


Hawanunui kwa sababu hakuna duka la vinyago wala la zawadi linalokuwa wazi wakati huo. Sana sana maduka yaliyo ndani uwanjani ndiyo yanayoweza kuwa wazi, lakini yale ya nje ya uwanja, hakuna. Tumekuwa Taifa la kimwinyi.


Taifa la wapiga usingizi. Haishangazi kuona polisi wakishiriki vema kutekeleza amri ya “kufukuza” watu baa kwa kisingizio kwamba wanapambana na wahalifu! Akili zetu zimegota katika kuamini kuwa uhalifu unapunguzwa kwa kufukuza watu kwenye sehemu za starehe! Dhamana polisi eti inatolewa mchana. Usiku, hata kama mtu ana haki ya kupata dhamana, ananyimwa. Kwetu Tanzania , giza linazima kila kitu!


Tufanye nini? Lazima tubadilike. Hatuwezi kupata maendeleo kwa kuendelea kufanya kazi kwa nusu siku.


Hatuwezi kuendelea kama maduka ya M-Pesa, Airtel Money, Tigo Pesa na mengine yanayotoa huduma kadha wa kadha, yatafunguliwa saa 4 asubuhi badala ya saa 10 alfajiri au yakawa wazi kwa saa 24.


Kama tatizo ni majambazi na ujambazi, suluhu ni kuutokomeza. Hatuwezi kuendelea kama mchana pekee ndiyo muda wa kusafiri na kufanya kazi, ilhali usiku ukawa muda wa watu kulazimishwa kulala.


Huko walikoendelea, hawakulala. Tena basi, hata kwenda likizo walilazimishwa! Japan na Wajapan ni mfano hai. Tubadilike.

1365 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!