Ndoto ya pensheni kwa wazee wote kutimia (1)

 

Siku za karibuni tumesikia misamiati mbalimbali juu ya kuwasaidia wazee wote wa Tanzania. Upo msamiati wa wazee kupatiwa PENSHENI huko tuelekeako. Wengine wanasema wazee watapata Cash Grant. Msamiati mwingine unasema wazee wanaandaliwa mpango unaojulikana kama Universal Pension Scheme. Kitaifa ipo mifumo kadhaa ya kuwasaidia watu inayoitwa Mifuko ya HifadhiI ya Jamii kama vile NSSF, PPF, NHIF na LAPF.

Katika mifuko hiyo, wazee tunapata mkanganyiko wa misamiati mingi, lakini la msingi wazee tuambiwe tutalipwa kwa Mfuko upi? Ilielezwa bungeni na Waziri wa Nchi (Sera na Uratibu) hivi karibuni kuwa Serikali imo katika mchakato wa kuwaandalia wazee malipo ya uzeeni.

 

Mzee kama mimi, nikiangalia matatizo ya malipo kwa wastaafu nabaki nashangaa ni Mfuko upi utakaotumiwa na Serikali kuwalipa wazee hicho wanachokiita pensheni kwa wazee wote wa nchi hii? Kwa nini nasema hivi? Nina uzoefu kiasi juu ya utumishi serikalini na namna wazee wastaafu wanavyosumbuka kupata hiyo haki yao ya pensheni.

 

Tanzania humu tupo wazee wa makundi mawili. Kundi la kwanza ni wale wazee waliostaafu kutoka utumishi wao katika ile sekta rasmi. Kundi hili lina watu wachache tu kati ya mamilioni ya nguvukazi watu (production group) katika Taifa hili. Kimahesabu wastaafu hawa wanafikia kama asilimia tano na ushei hivi (5.4%) ya watu wote wa nchi hii. Hawa ni wale waliokuwa watumishi katika ajira serikalini na mashirika ya umma yaani katika ile sekta rasmi. Ajira za wazee hawa zilitawaliwa na masharti mbalimbali. Watumishi wote wa Serikali waliajiriwa kwa barua maalumu (letters of appointment) nazo zilikuwa katika makundi matatu tofauti.

 

Wapo watumishi walioajiriwa kwa masharti ya KUDUMU SERIKALINI- barua zao zilisema “On Permanent and Pensionable Terms”. Hawa wote baada ya kustaafu walilipwa kiinua mgongo (lump sum gratuity) kisha wakawa wanapokea malipo ya uzeeni kiasi fulani kila mwezi mpaka kufa kwao. Ndivyo mimi ninavyojua kuhusu pensheni katika nchi hii.

 

Pili, wapo waajiriwa serikalini waliopata barua zao za ajira zilizoonesha masharti yao ya kazi kuwa ni ya muda tu zilisema “…on Temporary Terms”. Hawa baada ya muda wao wa kazi kumalizika walipewa kiinua mgongo na huo ndiyo ulikuwa mwisho wa mafao yao. Hawana pensheni yoyote.

 

Na tatu, wapo watu ajira zao serikalini ni kwa masharti ya mikataba maalumu. Hawa barua zao za mikataba zilisema “on Contract Terms”. Hapo jamaa hao mikataba ikimalizika walilipwa kile kilichokubalika katika mkataba na wakaagana na kuachana kabisa na waajiri. Wazee wote wa makundi haya mawili hawana haki yoyote ya kupatiwa malipo ya uzeeni.

 

Serikali ya mkoloni ilituandalia sheria ya kutulipa hiyo pensheni kwa utaratbu wao wa kionevu. Sheria yao waliyotuachia iliitwa “The Pensions Ordinance of 1954”. Sheria hii imetumika hadi Juni 30, 1999. Kwa maana hiyo, imewaathiri wazee wote waliostaafu tangu enzi za Awamu ya Kwanza na Awamu ya Pili.

 

Vijana wa siku hizi kwa kuona ubovu wa sheria ile na adha wanazopata wazee wao, basi wakajiandalia sheria nzuri za mafao ya uzeeni. Wakajiandalia mifuko mahsusi ya malipo ya uzeeni. Kila shirika likawa na Mfuko wake wa mafao ya uzeeni kwa watu wake. Serikali iliandaa sheria inayoitwa “The Public Service Retirement Benefits Act”. Humo walijipangia mafao ya kuridhisha kwa wastaafu wote wa Serikali na wa umma kwa jumla. Sheria hii inatoa mafao kwa watumishi wa Serikali na kwa wanasiasa. Hivyo kuna sheria mbili; moja kwa watumishi wote na hii inaitwa “The Public Service Retirement Act No. 2” ya mwaka 1999 na ilianza kutumika Julai Mosi, 1999 mpaka sasa. Mfuko ule unaitwa PSPF (yaani Public Service Pension Fund) na wote wanachangia.

 

Pili, ipo “The Political Pensions Act No. 3” ya mwaka 1999 na hii ni kwa wanasiasa wote marais, mawaziri, ma-RC, ma-DC na kadhalika. Ilianza kutumika tangu Novemba Mosi, 2000. Hii ya wanasiasa wanapata kiinua mgongo (gratuities), wanapata na posho ya kufungia au kuondokea ofisini (winding up allowances) na pensheni ya uzeeni.

Mashirika yote ya umma yana mifuko yao ya kulipa pensheni zao. Hivyo kuna mfuko wa NSSF, mfuko wa PPF, mfuko wa NHIF (yaani National Health Insurance Fund) na mfuko wa LAPF kwa watumishi wa Serikali za Mitaa. Hii Pensheni inayosemwa kwa wazee wote wa nchi hii iwe “Cash Grant” au “Universal Pension Scheme” ndiyo inayongojewa kwa hamu sana na wazee wote.

 

Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii ulifanya warsha jijini Dar es Salaam mnamo Machi 26, 2013 katika ukumbi wa JB Belmont Golden Jubilee Tower, Mtaa wa Ohio. Warsha ile ilikuwa elimishi kwa wazee. Wazee kutoka asasi mbalimbali za wazee tulikaribishwa. HelpAge International ilishiriki kikamilifu. Tulielezwa matarajio ya Serikali katika kufikia kuwalipa wazee pensheni ya jamii.

 

Kilipendekezwa kiasi cha pensheni kwa wazee kingekuwa si chini ya Sh. 17,167.51 kwa mwezi. Aidha, Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii ilituelewesha kuwa baadhi ya nchi humu Afrika mathalani Kenya , Uganda , Lesotho , Namibia , Zambia na Afrika Kusini wanao utaratibu wa kulipa wazee pensheni ya jamii (universal pension). Kenya , majirani zetu wanatoa Sh. 2,000 za Kenya kama Pensheni ya Jamii kwa wazee (hizi ni sawa na Sh. 40,000 za Tanzania ). Uganda wao kule wanalipa kama Sh. 23,000 kwa mwezi hiyo pensheni ya jamii kwa wazee. Hapo tukapata kitulizo cha moyo.

Jitihada zimefanyika kitaifa kuwafikiria wazee wale wa sekta isiyo kuwa rasmi, wazee wanaojishughulisha kujiajiri wenyewe nao wataweza kupata angalau fedha za kujikimu kila mwezi.

 

Lipo kundi la pili na lenye wazee wengi zaidi. Nchi hii nguvu kazi kubwa katika uzalishaji mali ni watu wa kundi hilo la pili la watu wa SEKTA ISIYOKUWA RASMI. Hawa ndiyo wakulima wote wa mazao ya biashara kama pamba, kahawa, korosho, mkonge, alizeti na kadhalika. Aidha, hawa ni wazalishaji wa chakula chote cha nchi hii – wanalima mahindi, mpunga, muhogo, mtama, mboga mboga na matunda katika nchi yetu. Kundi hili lina wavuvi wote, wafugaji wote, wachimba madini, wasusi na mafundi wa kila fani. Kundi kubwa hili ni asilimia 94.5 ya nguvu kazi yote (production group) katika Taifa. Wote wametumia nguvu zao nyingi wakati wa ujana wao katika kazi zao kujipatia riziki. Kumbe kwa kufanya vile wameinua sana uchumi au wamebeba uchumi wote wa Taifa letu.

 

Lakini nguvu kazi kubwa hii ikizeeka hawana chochote cha kufutia jasho lao. Hili wazo la kulipa universal pension kwa wazee limepokewa kwa furaha kubwa sana na linangojea utekelezwaji wake tu.

 

Mwaka 2010 tukiwa Morogoro tunasherehekea Oktoba Mosi, Mheshimiwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitamka hivi, namnukuu;

“Kuhusu pensheni ya jamii kwa wazee wote nataka niseme tu kwamba ni kweli mwaka jana 2009 wazee walituomba jambo hilo na tulilipokea, lakini hatukuwa tumefanya utafiti wa namna yoyote…” ndiyo kumaanisha maombi ya wazee yamefika serikalini, lakini bado wanalishughulikia.

 

Mei 17, 2013 kule Dodoma Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Jakaya Kikwete alikaribishwa kufunga wiki ya maonesho ya sherehe za Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii. Katika nafasi ile alidokezea suala la malipo ya uzeeni kwa wazee wote wa Tanzania.

 

Rais alionya hivi; “Nakuagiza Waziri Kabaka, kuwa anzeni sasa kufikiria namna ya kuwalipa WAZEE PENSHENI, lakini msikurupuke kufanya hivyo kwani ni lazima kujiridhisha kwanza kabla ya kuanza kutoa mafao hayo maana ‘mtaaibika’. Nawaomba msiahidi kwa watu kitu msichokiweza kukifanya na kuwa endelevu kwani mtaaibika, hivyo jipangeni vizuri kabla ya kuanza kutoa. Waelezeni ukweli wazee” (Mwananchi Toleo Na. 4710 la Jumamosi, Mei 18, 2013 uk. 1 na 4).

 

Maelezo au mwongozo ule wa Raisi ulilengwa kwetu sisi wazee tuelezwe wazi nini kinaendelea. Kutokea hapo mimi napata kigugumizi. Wazee wa Tanzania tuna chombo cha umoja wetu? Tuna chama tunachoweza kujigamba kuwa ndiyo sauti ya wazee wote wa Tanzania? Serikali itakapokuwa tayari kutueleza ukweli itatumia njia gani? Pensheni kwa wazee sote tunaihitaji! Sote tunafurahia wazee wa Taifa hili kupata Pensheni hiyo!

 

Itaendelea