Juni 1964 Tanzania ilitembelewa kwa mara ya kwanza na kiongozi wa ngazi ya juu kutoka China. Alikuwa Wazari Mkuu Chou en-Lai.

Februari 1965 China ilitembelewa kwa mara ya kwanza na kiongozi wa ngazi ya juu kutoka Tanzania. Alikuwa Rais Julius K. Nyerere.

 

Akizungumza ziarani China Februari 21, 1965 Rais Nyerere alitaja msimamo wa Tanzania kuhusu uhusiano wa kimataifa.

 

Mwalimu Nyerere alitamka bayana kwamba sisi (Tanzania) ni taifa changa lakini lenye kujivuna sana. Tunataka urafiki na wote lakini hatutathubutu kuwaruhusu rafiki zetu watuchagulie maadui. Afrika Mashariki tunao msemo usemao “wapiganapo ndovu nyasi ndizo zinaumia”.

 

Hivyo tumeamua kufuata siasa ya kutofungamana na upande wowote katika siasa ya nchi za nje, kwa ajili ya kujiepusha na migogoro ya ulimwengu isiyotuhusu.

 

Wakati huo huo, Mwalimu Nyerere alisisitiza kuwa Tanzania inataka urafiki na nchi yoyote inayozingatia misingi ya uhuru, usawa na kuheshimiana. Kuanzia wakati ule, urafiki kati ya Tanzania na China umekuwa kama wa damu.

 

Kwa upande wa China, nchi hiyo imetoa mchango mkubwa  katika maendeleo ya Tanzania. Kwa mfano, Tanzania ilijenga Kiwanda cha Nguo cha Urafiki Dar es Salaam kwa kushirikiana na China.

 

Vile vile ni China ilitoa mkopo uliowezesha Tanzania na China kujenga Reli ya Uhuru (TAZARA), na hivi majuzi Rais Xi Jiping wa China alipotembelea Tanzania, tulitangaziwa miradi isiyo na idadi ambayo China itachangia utekelezaji wake.

 

Lakini ukitaka kusema kweli kinachoonekana mpaka sasa, urafiki kati ya Tanzania na China ni urafiki wa wakubwa. Wao ndiyo wanaoheshimiana. Huku chini Wachina wanamwangalia Mtanzania wa kawaida kama mbwa tu! Hawampi heshima yoyote wakati Mwalimu Nyerere alitaka urafiki unaozingatia uhuru, usawa na kuheshimiana. Leo Wachina hapa nchini hufanya chochote wanachotaka, na mara nyingi hawachukuliwi hatua.

 

Je, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imeshindwa kufuatilia vitendo vya Wachina? Au tumekubali watudhalilishe kwa sababu tu nchi yao ndiyo inayotusaidia?

 

Hii ni kusema kwamba Mwalimu Nyerere aliposema katika Azimio la Arusha kwamba misaada huhatarisha uhuru wetu hakukosea.

 

Mara kwa mara tumesikia malalamiko ya wananchi wanaodai kwa haki kabisa kwamba Wachina wanaingia nchini kama wawekezaji lakini unakuta wengi wao hawashughuliki na uwekezaji. Hufanya biashara ambazo hufanywa na wananchi wa Tanzania. Je, Wachina ni sehemu ya wananchi wa Tanzania? Mbona huko kwao Watanzania si sehemu ya Wachina?

 

Tumesikia kwamba pale Kariakoo jijini Dar es Salaam Wachina hawajawekeza chochote cha maana, wamekaa kuuza maua tu, waliruhusiwa Tanzania ili wauze maua?

 

Tumesikia kule Mwanza Wachina wamejiingiza kwenye biashara ya mapanki. Walitoka kwao China ili kuja Tanzania kuuza mapanki?

 

Tumesikia hapa na hapo Wachina wanafanya shughuli nyingine zinazopaswa kufanywa na Watanzania, na hakuna anayewachukulia hatua. Kwa nini? Kwa sababu tunapata misaada mikubwa kutoka China? Tunauza uhuru wetu! Tumeuza heshima yetu!

 

Lakini kikubwa na kibaya zaidi ni ukweli kwamba Wachina hawawaheshimu Watanzania wa ngazi ya chini ambao ndiyo walio wengi. Wachina huwafanyia chochote wanachotaka.

 

Nimeshuhudia pale Kariakoo jijini Dar es Salaam Wachina wanaosimamia ujenzi wa majumba ya ghorofa wakiwasukuma vibarua Waafrika na kuwanenea maneno mabaya kwa ukali. Utadhani Watanzania wako ugenini China! Kumbe ni Wachina walio ugenini Tanzania!

 

Imeripotiwa majuzi tu Wachina wa Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group ya China inayohusika na ujenzi wa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam walivyompiga hadi kumuua kinyama kibarua wao aliyefahamika kwa jina la Juma au Juma Mgogo.

 

Imeelezwa kuwa tukio hilo la kutisha lilitokea usiku wa Jumapili ya Mei 26, mwaka huu. Imeelezwa kuwa Wachina walimfunga kamba miguuni na mikononi Mtanzania kibarua wao huyo na kumpiga maeneo ya tumboni na vyuma wanavyotumia kujenga, kisha walimwacha katika eneo hilo mpaka alipofikwa na mauti!

 

Katika nchi nyingine, na hata katika nchi yetu hii enzi za Mwalimu Nyerere, Wachina hao walikuwa wa kufukuzwa mara moja Tanzania. Lakini wanaendelea kupeta. Tumewaacha Wachina wafanye chochote wanachotaka kwa sababu wanatusaidia!

 

Lakini dharau ya Wachina haiko tu kwa wananchi. Iko pia kwa Serikali yetu maskini! Kwa mfano, tangu wakati wa ujenzi wa Reli ya Uhuru mpaka leo Wachina wanaporejea kwao mizigo yao haipekuliwi uwanja wa ndege. Kwa njia hiyo Wachina wanaendelea kutoroshea kwao madini ya Tanzania, na hakuna aliyewachukulia hatua! Si wanatupa misaada mikubwa?

 

Ni katika mazingira hayo, majuzi tu wananchi na wala si Serikali wamewashtukia Wachina wakitorosha madini katika malori saba kule Igunga, Tabora. Kuna madai ya siku nyingi kwamba hali ya uvunjifu wa amani inayotokea kila mara katika Tanzania yetu ya leo ni matokeo ya Serikali kukosa usikivu.

 

Tusije tukasahau kwamba Afrika Kusini miaka michache iliyopita wananchi walipambana vikali na wageni walioonekana walikuwa wanapendelewa na Serikali. Kwa hiyo, Serikali ikifumbia macho vitendo vya Wachina kunyanyasa wananchi na kujifanyia chochote wanachotaka bila kuchukuliwa hatua, basi Serikali ijiandae kuona mapambano makali dhidi ya Wachina nchini.

 

Yakitokea hayo Serikali itapata aibu kubwa mbele ya viongozi wa China. Twende tusubiri.

Please follow and like us:
Pin Share