Ndugai tafuta busara katika upuuzi wa wanaopinga

Wiki iliyopita Spika wa Bunge, Job Ndugai, alinukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari akieleza dhamira yake ya kuliongoza Bunge kutunga kanuni mpya ambazo anaamini zitaleta ulingano kati ya wabunge wa kambi mbalimbali. Spika Ndugai amesema kanuni hizo zitaachana na utambulisho wa sasa wa wabunge; wa chama tawala na wabunge wa upinzani.

Badala yake, mfumo mpya utawatambua wabunge kulingana na wingi wao bungeni.

Spika amesema kwa utambuzi wa sasa, wapo wabunge ambao wanajiona dhima yao ni kupinga tu kwa sababu wanaitwa wapinzani.

Lakini Spika akaenda mbali zaidi na kuwaita wale wanaopinga, hasa wanaoipinga Bajeti ya Serikali kuwa ni wapuuzi. Spika amesema bajeti inakuwa na mambo mengi ndani yake na kuipinga ni upuuzi.

Tunadhani kuwa kauli hii ni ya bahati mbaya sana kutolewa na kiongozi wa hadhi ya Spika kwa sababu katika hayo mambo mengi yaliyomo ndani ya bajeti kuna uwezekano wa kuwepo mengine ambayo hayafai. Katika hali kama hiyo, unapounga mkono mambo hayo kwa pamoja, yakiwemo mazuri na mabaya, ina maana unaunga mkono yote. Na kwa upande mwingine, unapopinga mambo hayo kwa pamoja, yaani mabaya na mazuri yaliyowekwa pamoja, ina maana utakuwa unayapinga yote.

Kwa maana hiyo, kama ni upuuzi, basi hata wale wanaounga mkono mambo yote, yakiwamo na mabaya, nao wanaweza kuonekana wapuuzi.

Lakini sisi tunaamini kuwa wote, wanaopinga na kuikubali bajeti hawastahili kupachikwa upuuzi.

Wanaopinga ni haki yao kikatiba kupinga pale wanapojiaminisha kuwa kilichomo ndani ya bajeti hakiendani na kile ambacho wao wanakiamini na kukitaka.

Lakini pia, kama suala la kupinga bajeti lingekuwa halipaswi kuwepo, basi hata mfumo wa kupitisha bajeti ungelitambua hilo. Hivi sasa mfumo wa kupitisha bajeti una nafasi tatu; anayeunga mkono, anayepinga na asiyetaka kushiriki. Kama kuna nafasi hizo zinazotolewa kikanuni, kwa nini wanaopinga wanaonekana kuwa ni wapuuzi?

Lakini ifahamike kuwa wanaoipinga bajeti wanakuwa na sababu zao. Tatizo linaweza kuwa tunawaangalia kwa uamuzi wao wa mwisho wa kupinga bila kuangalia kwa nini wanapinga au wanapinga kitu gani. Tunafanya dhambi kwa kuwahukumu kwa uamuzi wao wa mwisho bila kuangalia sababu zao.

Tunaamini Spika akiamua kujipa kazi ya kuchunguza ni kwa nini wanapinga na wanapinga kitu gani, anaweza kuiona busara ya wanaopinga katikati ya kile yeye anachoamini kuwa ni upuuzi.