Ndugu Rais karibu mezani

Ndugu Rais, Bwana Yesu alipoona saa yake imekaribia aliwaambia wanafunzi wake waandae meza apate kula nao chakula cha mwisho.

Angeweza kuwaaga kwa namna nyingine yoyote, lakini aliandaa meza.

Namshukuru Mungu kuniwezesha kuingia katika chumba ilipoandaliwa meza kwa ajili ya chakula cha mwisho. Mwenyezi Mungu ambariki yeye na nyumba yake mwanamwema yule aliyeniwezesha kuikanyaga ardhi ya nchi ya ahadi. Nchi takatifu, Israel! Muumba amfanyie wepesi katika kufikia matamanio yake.

Baba karibu mezani nikusimulie. Baada ya kuibusu ardhi takatifu katika Jiji la Tel Aviv tulielekea  Yerusalem, ‘mji wangu’.

Tulifika Jeriko na sehemu zote kama zilivyoandikwa katika maandiko matakatifu. Tukapanda mpaka mahali pa juu kabisa katika Mlima Tabor.

Tuliogelea katika bahari iliyokufa yenye maji ya chumvi kali na mazito kiasi kwamba huwezi kuzama. Ndani yake hakiishi kiumbe chochote.

Galilaya tulisafiri kwa boti katika Ziwa Galilaya ambalo wenyewe wanaliita bahari. Tulifika Carpernaum na katika mji wa Canaan.

Kuelekea mkesha wa Krismas tulikuwa katika Kanisa Kuu la Bethlehem kushuhudia mahali alipozaliwa Mwokozi. Tulipanda kilima hadi Golgota mahali ambako safari ya ukombozi ilikamilishwa, tukamtukuza Mungu.

Ndugu Rais, karibu mezani kwa kuwa ndiyo palipo na kila kitu. Mazungumzo ya hekima na busara yanapatika mezani. Mapigano hufanyika viwanja vya mapigano, lakini amani na mazungumzo yaletayo amani hufanyika mezani.

Watu hukaa wakazungumza. Baba karibu mezani!

Ndugu Rais, kwa kuwa sistahili kuyapita malango ya makazi yako takatifu, lakini ikikupendeza wewe baba, waweza kuja kwangu, nyumbani kwa mjakazi wako. Baba, karibu mezani. Uje tukae mezani tuzungumze, tuone ni kipi kinacholeta tofauti. Kama kuna tatizo tuone hilo tatizo linatoka wapi. Uje wanao tujue kinachotutofautisha. Tuone ni wapi pa kufanya marekebisho. Kama kuna kitu chochote kilichoko katikati ya moyo wako njoo ukiweke mezani. Baba njoo utuambie wanao kama kuna kitu chochote kinachokufanya ukose amani. Karibu mezani kwa maana imeandikwa, ‘’Tazama jinsi ilivyo vema na kupendeza, ndugu wakae pamoja kwa upendo hivyo!’’ Baba karibu mezani.

Nayakumbuka vema maneno aliyowahi kuniambia Komredi Abdulrahman Kinana akiwa bado ni Katibu Mkuu wa Chama Cha mapinduzi.

Aliniambia, ‘’Bwana Mayega haya unayoandika na sisi tunayasema hayo hayo. Lakini sisi tunayasema katika vikao vya chama.’’

Maongezi haya yalifanyika wakati tukiwa katika awamu ya nne. Nakumbuka mwanamwema mmoja alinitumia ujumbe akisema viti vya Ikulu zote katika nchi za Kiafrika, vilitengenezwa na seremala mmoja ndiyo maana kuna ugonjwa unaofanana’. Baba karibu mezani.

Tuliwaona walivyopita wanawema wa bara hili na dunia hii kwa ujumla.

Alipita Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa kwanza wa nchi hii. Akapita na Mzee Madiba, Rais mweusi wa kwanza wa Afrika Kusini, Nelson Mandela. Hawa walikuwa ni watu wa mazungumzo na walishinda vita nyingi wakiwa mezani. Lakini Iddi Amin Dada wa Uganda, Mobutu Sesseseko wa Zaire, Jean Bokassa, Adolf Hitler na wengine nao pia walipita. Hawa waliikataa meza ya mazungumzo. Mwisho wao ulikuwa mchungu kama shubiri. Kusimulia mateso yao ya mwisho kunaleta mateso makubwa katika kumbukumbu. Lakini wewe karibu mezani.

Ndugu Rais, wacha nikubali kuwa mimi ni kizazi cha zamani, lakini nasikiliza nyimbo za vijana wetu. Wao wanasema ni kizazi kipya.

Nilipomsikia kijana wetu akiimba kuwa nchi imeingia matope, kila nyumba inanong’ona kuwa kiongozi atoke, alinifikirisha sana. Baba karibu mezani. Anasema anatoka nje aende dukani kwa Mangi akanunue supageti anakuta watu badala ya kutafuta senti wamekaa wanasema redio imevamiwa geti. Najiuliza ni nani alivamia geti la redio? Anamlilia Kambarage maskini hata hamjui anasema alikuwa ni baba mmoja wa wote.

Anauliza kama nchi tunakwenda wapi? Mama yake akamwambia, we Abdul, wewe bado mtoto mdogo sana. Hii ‘itakukosti’. Anasema kuona rafiki yake kipenzi ambaye hata wimbo wake alikuwa bado hajauposti kakamatwa, na juzi kapotea na Roma akaona bora afunge bakuli lake, akakojoe akalale! Baba karibu mezani. Kwanini mtoto wetu amlilie Kambarage asiyemjua wakati baba upo? Huyu hata akicheka hawezi kumpenda mtu.

Mwingine kwa kuchoshwa na nchi yake anaamua kuiimba Zimbabwe. Nimekaa Zimbabwe. Mama yake naye akamwambia, wewe utatekwa tena! Lakini yeye ameapa kubaki ngangari kuililia amani katika nchi yake. Baba karibu mezani. Kuna kijana aliuliza, hivi uhuru wa kuongea katika nchi hii upo? Usije ukaongea halafu kesho ukajikuta uko ‘sentro’. Akasema unamjua nani sijui kuwa ni jipu jipya kutoka wapi sijui, hapo sijashika vizuri.

Ndugu Rais, ninapomsikia mwanetu leo analia kuwa yuko tayari kwenda Golgota, vichomi vya mbavu vinanibana. Nimefika Golgota mahali ambako safari ya ukombozi ilipohitimishwa, lakini baada ya mateso makali sana ya Yesu Kristu. Anasema yuko tayari naye asulubiwe damu yake imwagike kwa ajili ya amani ya watakaobaki. Wimbo wake unaanza na maneno ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Mwalimu alisema, ‘’Lazima tujenge utaratibu wa kuwadhibiti viongozi wetu, vinginevyo…’’ Namba ya vijana wanaohamasishwa kwa nyimbo hizi inazidi kuongezeka siku hadi siku. Tuendako kunachimbika.

Ndugu Rais, nguvu ya taifa lolote ni vijana. Hawa vijana sisi tunaona wanaimba, lakini ukweli ni kwamba hawa vijana wanalia! Machozi yao yanadondokea katika mioyo yao. Mioyo yao ni ya nyama iko siku itajaa.

Wakiimba vijana wote maelfu kwa maelfu wanasisimka na kupandwa mori wa kutaka kutenda mara moja. Kabla mioyo yao haijapasuka wakasema liwalo na liwe, baba karibu mezani tuyazungumze. Vijana wana haki ya kuishi katika nchi yao hii bila kuwa na hofu kama sisi tulivyoishi kwa amani, upendo wa kweli, umoja na mshikamano wakati wa uhai wa baba yetu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Imeandikwa ole wake siku hiyo kwa maana hakuna jiwe litakalobaki juu ya jiwe! Itakuwa ni kulia na kusaga meno. Baba karibu mezani!