Baadhi ya watu, wakiwamo ajuza na vikongwe katika vijiji vya Kongolo na Shilingwa, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza wamekimbia makazi yao wakihofu kuuawa.

Miongoni mwa waliokimbia ni Sophia Pondi (54) aliyevamiwa nyumbani kisha wavamizi hao kumpigilia msumari tumboni.

Wakazi wa Kijiji cha Shilingwa; Tabiza Genge (72), Kazungu Luhwegula (82) na Lukanya Kidai wamehamia kwa Diwani wa Kongolo, Herbert Faustine, punde baada ya kupokea barua wakitishiwa kuchomewa nyumba.

Vitisho hivyo vinatolewa kukiwa tayari kumefanywa mauaji ya Kija Bugomola na Laurencia Kalogi, aliyeuawa kwa kutenganishwa kichwa na kiwiliwili Agosti, mwaka juzi.

Watu watano wakiwamo wana familia wawili walitiwa mbaroni kwa mauaji hayo ya Laurencia, lakini wakaachiwa baadaye.

Tabiza aliyepoteza uwezo wa kuona miaka 10 iliyopita, ameliambia JAMHURI kijijini Shilingwa kuwa usiku wa manane Septemba, mwaka huu alivamiwa na kutishiwa kuuawa. Aliripoti Kituo cha Polisi Nyanguge, Magu. Anadai mhusika kwenye tukio hilo ni mtoto wa mjomba wake (jina tunalo).

Anasema alitishiwa baada ya kulalamika kwa Mbunge wa Magu, Bonaventura Kiswaga.

Anadai kuwa mashamba ya mama yake, marehemu Mpejiwa Machimu, yenye ukubwa wa ekari 57 yamechukuliwa na nduguye huyo anayemtuhumu kutaka kumuua.

Mkazi wa Kijiji cha Shilingwa, Kalogi Makolobela, anasema anaufahamu mgogoro huo wa ardhi, na kusema mashamba hayo ni mali ya wazazi wa Tabiza.

“Dohayaga guchomelwa numba yiswe, kisa mashamba yiswe gang’wamayu one,” anasema Tabiza kwa lugha ya Kisukuma, akimaanisha wanataka kuchomewa nyumba yao, kisa mashamba ya mama yake.

Ajuza huyo anayeishi kwa msaada wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF), yeye na mume wake, Kazungu Luhwegula na kaka yake, Lukanya Kidai, baada ya vitisho hivyo walikwenda kuishi kwa diwani.

Tabiza aliyezungumza akitokwa machozi, anasema waliishi kwa diwani kwa siku tatu.

“Alikuja akapiga mlango na kusema mmedanganywa na mbunge wenu. Nitawachomea ndani. Nilikaa hadi asubuhi, nimeogopa sana, maana nilikuwa peke yangu tu,” anasema.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Kongolo, Wilbroad Mbuga, amekiri kuwapo kwa matukio hayo anayoyahusisha na ushirikina na migogoro ya mashamba. Anasema suala hilo lipo mahakamani.

Kuhusu Sophia Pondi, Mbuga anasema amekimbia nyumba yake akihofu kuuawa.

Pondi alifanyiwa upasuaji katika Kituo cha Afya Nyanguge wilayani Magu. Polisi hawajamkamata mtuhumiwa.

Mbuga anasema kwa mujibu wa maelezo ya Sophia, alipovamiwa wahalifu walimwangusha chini na kuanza kumpigilia msumari tumboni.

“Baadaye mmoja wa watu hao alisema, ‘huyu siye tunayemtafuta, mwacheni’. Wakamuacha na msumari ukiwa tumboni,” anasema Mbuga.

Anasema kabla ya mwaka 2015, wastani wa wazee watano waliuawa kila mwaka.

Mganga Msaidizi wa Kituo cha Afya Nyanguge, Dk. Salome Kanfune, anasema Sophia alifanyiwa upasuaji uliosaidia kuondoa msumari tumboni.

Anasema elimu ya kuwalinda wazee inahitajika hasa wilayani Magu.

Diwani Faustine ameomba polisi wawakamate watuhumiwa na wawafikishe mahakamani.

“Kongolo nahitaji watu wote wawe salama. Matukio haya ni vema polisi ikawashughulikia wanaotishia au kuua wazee wetu. Wana Kongolo tunataka maendeleo, si mauaji,” anasema.

Anaiomba serikali na mashirika ya kiraia wilayani Magu kuongeza kasi ya utoaji elimu ya kuwalinda wazee.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Dk. Philemon Sengati, ameahidi kuzuru kata hiyo ili kuwaondoa hofu wananchi.

“Tukio la yule mama wa mashamba kutishiwa kuuawa nalifahamu. Nilishamuagiza OCD (Mkuu wa Polisi wa Wilaya) wawakamate wahusika.

“Lakini hili tukio jingine unaloniambia (la Sophia Pondi – aliyekomelewa msumari wa nchi sita tumboni) silijui. Siku moja Diwani wa Kongolo alinipigia (simu). Inaonekana kuna tatizo huko.

“Ngoja niwasiliane na diwani waniandalie, nitakwenda na vyombo vyangu vya usalama tuanze kuwasaka wahusika,” amesema DC Sengati.

Gazeti la JAMHURI limethibitishiwa kuwa katika Kijiji cha Kongolo wananchi; Elizabeth Andrew (66) na Lorencia Lwangalila (77) wameandikiwa barua wakitishiwa kuuawa.

Walipata barua hizo Novemba 10, mwaka jana mlangoni mwa nyumba anamoishi Lorencia.

Tukio hilo limeripotiwa Kituo cha Polisi Nyanguge Novemba 14, mwaka jana na kupewa namba ya uchunguzi NYG/RB/1041/2017. Hadi sasa hakuna aliyekamatwa.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu, Hilary Elisha, amesema: “Tumeshaomba Sh bilioni tatu Wizara ya Ardhi ili tuboreshe kwa kupima na kupanga maeneo ya vijiji vyote 82. Tukipata fedha tutapima kwa kila mtu ili kuondoa migogoro ya ardhi.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jonathan Shana (Dakika Sifuri) hakupatikana. Afisa Habari wa jeshi hilo mkoani Mwanza, Oscar Msuya, amekataa kuzungumza akisema mwenye dhima hiyo ni Kamanda Shana mwenyewe.

Please follow and like us:
Pin Share