Ndugu Rais, kinywa kilikiponza kichwa ni maneno yenye hekima yaliyosemwa na wahenga wetu. Jikwae sehemu yoyote, lakini usijikwae ulimi.

Maneno yakishamtoka mtu hawezi kuyarudisha mdomoni. Sijui wanakuwa na maana gani wanaosema futa maneno yako. Maneno yaliyokwisha tamkwa hayawezi kufutwa wala kufutika. Eti iwe kama vile hayakutamkwa. Haiwezekani. Unachoweza kufanya ni kutamka maneno mengine ya kupooza yale yaliyokwisha tamkwa. Hii tumeona na kusikia mara nyingi.

Karimjee, mahali ulipolazwa mwili wa marehemu Reginald Mengi yalitamkwa maneno mbalimbali. Mema ya msingi yalitamkwa na yaliyojaa udhaifu wa watamkaji pia tuliyasikia. Walisema kuwa Reginald Mengi aliwahi kutamka kuwa wako wanadamu wenye ulemavu wa fikra. Tunadhani hao kama vichwa vyao vingekuwa ni mashine, grisi imekauka. Kufikiri kwao ni vyuma tu vinasagana nakutoa unga. Ah! Baba, inauma sana kuona hawa nao ni baadhi ya viongozi wetu!

Baba, Profesa Kabudi alisimama akasema, “Marehemu amepigana vitavilivyo vyema. Mwendo ameumaliza na imani ameilinda’’. Maneno kutoka katika Biblia Takatifu. Akaendelea kusema kila kitu kina majira yake na kila jambo hapa duniani lina wakati wake. Kuna wakati wa kuzaliwa na wakati wa kufa. Wakati wa kupanda na wakati wa kuvuna tulichopanda.

Kuna wakati wa kulia na wakati wa kucheka. Aliposema imeandikwa, jina la Bwana libarikiwe, waombolezaji wengine wakachanganyikiwa. Baraka zote ni za Bwana; huyo wa kulibariki jina la Bwana hiyo baraka ataitoa wapi?

Ndugu Rais, tulitamka kuwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho 2020 ni kaa la moto. Tusiende katika Uchaguzi Mkuu mwakani tukiwa tumeparaganyika hivi – ni hatari kubwa. Watu wazima walio makini walitusoma wakatuelewa.

Kumbe Reginald Mengi naye alitusoma akatuelewa. Ndugu James Mbatia aliwaambia waombolezaji kuwa Dk. Mengi alipoongea na Kituo cha Demokrasia, alisisitiza sana umuhimu wa maridhiano katika nchi yetu kabla ya kwenda kwenye Uchaguzi Mkuu.

Alisema ni muhimu maridhiano yakafanyika kabla ya Uchaguzi Mkuu ili uchaguzi huo ujao, usiwe wa kumwaga damu. Akimnukuu anasema alisema, “Maisha yako kwenye ulimi wa binadamu. Tukitumia vizuri ndimi zetu hasa sisi wanasiasa Tanzania itakuwa sehemu salama na nzuri zaidi ya kuishi’’. Yako maneno mengi yaliyokwishatamkwa na baadhi ya viongozi wetu yanayohitaji suluhu.

Sasa wengi wameanza kuonyesha hofu yao kubwa tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020. Askofu Gwajima anasema, ‘’Mkumbuke niliwahi kufanya uchambuzi humu na kwenye gazeti la The Drum la South Africa na Radio DW (Ujerumani), kwamba uchaguzi Mkuu wa 2020 Tanzania utakuwa mgumu haijawahi kutokea tangu vyama vingi vya siasa vianzishwe nchini, hasa kwa upande wa chama changu cha CCM. Mpasuko ndani ya CCM usiposhughulikiwa, vyombo tegemewa havitofua dafu, maana ni uchaguzi wa kwanza kuwahi kutokea utakaosimamiwa na nchi za Magharibi utake usitake’’.

Baba, penye wengi dhaifu hawakosekani. Mmoja aliwaambia waombolezaji kuwa Chama Cha Mapinduzi ni chama muhimu kwa sababu hata watu mashuhuri kama Reginald Mengi alikuwa ni mwanachama wa CCM. Katika shughuli kubwa kama ile, alichoona cha muhimu na kikubwa kupita vyote ni Reginald Mengi kuwa mwanachama wa CCM. Masikini hawa ndiyo baadhi ya viongozi wetu. Bado wanafikiri wakiwa sandukuni. Kwake hilo ni kati ya mafanikio makubwa yaliyofanywa na chama chake.

Duniani kuna watu. Hizo ndizo fikra za watu walio wengi wenye akili za kawaida. Habari kuu iliyoenea  katika kila barabara siku hizi ni habari za mpira wa miguu. Haishangazi kumwona mswahili ambaye hata nchi jirani tu hajafika, lakini ni mpenzi kindakindaki wa timu ya mpira ya Ulaya. Anapostahili kuwa mtu huyu ni barabarani; siyo ofisini aliko sasa. Wenye akili kubwa kumtegemea huyu awe ni mtu wa kuwasemea, hawajui tu kuwa hilo ni kwa hasara yao wenyewe.

Baba, alipouawa binti yetu mwema Akwilina Akwilini wapo waliosikika wakisema, ‘’Ndiyo, kwa sababu tuliambiwa wengine watakuwa wanaandamana wakiwa ndani ya daladala’’. Baba hakika aliyeitamka sentensi hii hastahili kuwa bado ni kiongozi wa watu. Kwa kauli hiyo huyu anawatarajia Watanzania wasadiki  kuwa aliyemuua Akwilina hajulikani?

Baba, ulisema vema kuwa Watanzania siyo wajinga. Wana uwezo wa ‘kuanalaizi’ na kuchambua mambo. Hivi huyu baba hakukusikia?

Yakaja yaliyo mazito zaidi. Wakiwa kanisani kule Moshi katika ibada ya misa ya kumzika marehemu Reginald Mengi, Baba Askofu Dk. Fredrick Shoo alisikika akibembeleza kwa unyenyekevu kuwa, ‘’Basi mwanangu kama tumekukosea utusamehe, nenda kakae. Ananiuliza mnaniitia nini?’’

Akawaambia waumini. Kanisa lote likazizima. Mabishano yakaendelea Madhabahuni! Ndipo Katibu wetu Mkuu wa CCM Ndugu Bashiru Allyaliposimama kumjibu Baba Askofu aliyetaka kujua kama vijana wadogo wanaopewa madaraka wanaandaliwa? Akasema, ‘’…Lipo ulilolitaja Baba Askofu nimalizie kwa sababu muda hautoshi. Kuhusu viongozi na umuhimu wa kuwaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora. Baba Askofu kazi hiyo hatujaifanya. Na kwa sababu hatujaifanya tunaanza kuvuna matunda ya kutowaandaa vijana wetu kuwa viongozi bora, watiifu, wakweli, wanyenyekevu na wenye heshima. Naomba nitumie fursa hii kumwombea msamaha kijana wangu’’.

Baba, hivi wote waliokwenda Moshi lengo lilikuwa ni msiba? Utamtambua mwenye huzuni ya msiba kwa mavazi yake kama unavyoweza kumtambua ‘chekibob’ kwa mavazi yake. Tunatoa fursa kwa watu wengine kudhani wengine walienda kule kuthibitisha tu kuwa Reginald Mengi amezikwa kweli. Katibu Mkuu wetu wa CCM, Ndugu Bashiru Ally alionyesha busara kubwa; busara ambayo wengi walidhani ndugu Abdulrahman Kinana –Katibu Mkuu wa CCM aliyepita angekuwa ameondoka nayo na kuiacha CCM ikiwa sawa na debe shinda lisiloacha kutika! Wengi tuna imani kubwa na mtu huyu.

Huko nyuma aliwahi kusema, ‘’Bila kusimamia haki na usawa nchi haiwezi kuepuka machafuko. Anayekiuka haki na usawa anachagua kuwa mpweke na atakuwa kiongozi anayetumia mabavu. Hataheshimika, hataaminika: na kiongozi asipoheshimika na kuaminika ndiyo chanzo cha mabavu kwa sababu anapoteza uhalali wa kisiasa. Hawezi kumshawishi mtu yeyote kwa sababu ushawishi na uongozi msingi wake ni kuaminika na heshima inatokana na kuaminika kwake’’. Bila tahadhari vinywa vyetu vitaviponza vichwa vyetu!

980 Total Views 1 Views Today
||||| 2 I Like It! |||||
Sambaza!