Ndugu Rais, kwa urais wako nchini mwetu wewe ndiye baba wa sisi wote.
Mwisho ni mwaka 2020 au mwaka 2025 au labda hata kuendelea, nani anajua? Marehemu mama
yangu alikuwa ananiambia: “Umwenzo wa mtu inkama.’’ Maana yake: “Moyo
wa mtu una siri nyingi.”

Waliojibu kuwa “Mtwara kuchele” zilifanana na zile tunazozisikia tunapotembelea wodi za wagonjwa wa muda mrefu. Hawa wamekata tamaa na kupoteza matumaini. Kuwarejeshea imani yao kwetu ilikuwa ni kwenda na fedha za malipo yao mfukoni na si vinginevyo.
Nguvu ya agizo la walipwe haraka inapotea, ukiangalia urefu wa muda uliokwisha kupita tangu sakata la korosho lianzishwe. Hata hivyo, kwa agizo hilo ilikuwa ni kukiri tu baba kuwa wakulima wa korosho walikuwa hawajalipwa japo kwa baadhi.
Inapotolewa hotuba inayogusa mioyo ya wananchi, wengine hujichanganya na wananchi wa hali ya chini ili kujua hisia zao. Kumbuka ukihutubia Mwanza, Daraja la Furahisha uliuliza: “Niwape milioni 50 za kila kijiji au nijaze madawa [dawa] hospitalini?’’

Ukumbi mzima, tena kwa pamoja kama vile walipangwa, ulilipuka na kusema: “Ah! Mzee, tupe milioni 50 zetu, dawa tutanunua wenyewe!’’ Hawa ni wa Mbagala. Huko vijijini na mashambani walijibu nini? Mwakani tutakapokwenda kuwaomba kura, Sh milioni 50 hatuna, na dawa hospitalini hakuna, watatuweka katika fungu gani?
Kutolewa mamia ya mabilioni ya shilingi, na wakulima wa korosho kulipwa ni vitu viwili tofauti. Hivyo haishangazi kusikia kwamba waliokwisha kulipwa hawajulikani waliko. Mjini wanasema: “Ndiyo mpango mzima.” Waziri ameagiza yaorodheshwe majina ya wote waliokwisha kulipwa na majina yabandikwe kwenye mbao za matangazo.

Akitoa sababu ya kuagiza hivyo, waziri anasema amelazimika kutoa agizo hilo baada ya kuona kwamba kila aliyemuuliza, alimjibu kuwa hajalipwa. Mpaka kufikia uamuzi huo atakuwa aliwauliza wakulima wa korosho wengi sana. Huu ni ushahidi tosha kutoka kwa waziri kuwa wako baadhi ya wakulima wa korosho hawajalipwa mpaka leo. Kama mabilioni ya shilingi yametolewa na wakulima wa korosho hawajalipwa, kuna ubaya gani?

Hata kama huu ndiyo mchango wao kwa Uchaguzi Mkuu ujao, pia kuna ubaya gani? Kwa urefu wa muda ana haki anayeuliza, nani anajali? Walioshangilia Mtwara kuchele wawasaidie wenzao kulielewa hili kama walivyolielewa wao ili kama ni kushangilia washangilie wote kwa pamoja.
Kama kangomba ni dhambi, basi dhambi ni kama sumu, haionjwi! Nimewasamehe endeleeni, lakini msimu ujao msifanye tena, hapana.
Tofauti ni majina tu. Nenda Feri ndipo utagundua kuwa hata samaki baharini kuna kangomba. Yawezekana jina la hawa wa Mtwara ndilo baya.
Katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa Watu imeandikwa: “Nyoka huuawa kwa jina lake tu.”  Wengine tulikataa kazi hizi za kuteuliwa kutokana na changamoto zake, hasa pale unapoagizwa kutenda tofauti na utashi wako.
Siku ya kufurushwa meneja wa korosho ilipomkuta kama angekuwa na waziri aliyejisimika mwenyewe angetetewa kwa kuisema kweli. Lakini waziri alimwacha meneja wa korosho aende peke yake bila kujua kuwa kumbe naye hakuwa mkaaji.

Leo tunapowaangukia watu wale wale, waliotuambia kuwa wale wanawema, Charles na mwenzake Charles hawakuwa na majibu, tuwajibu nini? Walipotumbuliwa ilitoka damu na maji tu! Wasife moyo, bali watambue kuwa nchi bado ni kubwa kwa maana hakuna aliye mkubwa kuliko Tanzania.
Majukumu ya kitaifa ni mengi. Yaonekana faili la malipo kwa wakulima wa korosho lilikuwa chini sana, hivyo imechukua muda mrefu kufika juu. Lakini aliyelianzisha hili sakata la korosho ni nani hata asikumbuke kufuatilia malipo yake?

Tuliposikia watu wakishangilia ilipopigwa mbiu ya ‘Mtwara kuchele’ tukaikumbuka siku ile ya uzinduzi wa ujenzi wa barabara ya njia nane pale Ubungo. Baba ulipotangaza kuwa wote walioathiriwa na bomoabomoa kupisha ujenzi huo hawatalipwa fidia, watu walishangilia. Ukatangaza mara ya pili kuwa hakuna fidia, watu wakashangilia.

Hata uliporudia kwa mara ya tatu kuwa hakuna fidia kwa waathirika, bado watu walishangilia. Kuamini kuwa watu wanaweza kuwa wanachomwa visu vya mbavu halafu wakawa wanashangilia, haiwezi kuwa ni imani inayomhusisha Mungu kama mashahidi wa Uganda!
Tulikuona baba ukimwita mwanao Godbless Lema pale msibani. Mlichoongea hatukusikia ila lile tendo la kumwita lilionyesha kuwa wewe ni baba mwema!
Baba anapoonyesha upendo kwa mwanae hata mmoja, watoto wote humpenda baba yao hata zaidi. Ulimwita Godbless Lema ukijua kabisa kuwa yuko msibani, wamefiwa. Laiti baba ungemwita Godbless Lema siku zile alipokuwa akisota gerezani kwa miezi mingi na kwa mujibu wa hukumu yake, hakuwa na hatia yoyote, hakika baraka zake Muumba wetu zingekushukia kichwani pako kama umande wa asubuhi. Nawe ungestawi kama mtende! Wako wengi bado wanasota magerezani bila kuwa na hatia yoyote! Baba, waite ukae nao mzungumze! Ni watoto wa mama mmoja Tanzania na wewe ndiye baba yao.
Godbless Lema huyu huyu aliwaonya wabunge wenzake bungeni akisema:
“Mnacheka sasa anapotupitisha kwenye magumu, eleweni kuwa atakapokuwa amekwisha kutumaliza sisi, atawageukia nyinyi!’’ Godbless Lema sasa anakabiliwa na tuhuma. Amemuunga mkono Halima Mdee kuwa Bunge ni dhaifu. Adhabu yake imedhihirisha udhaifu wa Bunge! Halima Mdee amekwisha kuhukumiwa kwa kumuunga mkono CAG kuwa Bunge ni dhaifu. Hili linaupaka matope utawala wa baba.

Ni Halima Mdee aliyeliuliza Bunge iweje mapesa mengi kiasi hiki yatumike kufanya ununuzi bila kibali cha Bunge? Mpaka leo Bunge halijachukua hatua yoyote. Linachokifanya sasa Bunge, linathibitisha yanayosemwa juu yake.
Baba waweke wazi watu wako. Mitandao inasema shida hii si kati ya Bunge na CAG, bali ni kati ya baba na Musa Assad kama CAG, kusema hakuona Sh trilioni 1.5 zilipotumika. Ulituambia baba kuwa Watanzania wana uwezo wa ‘kuanalaizi’ mambo.

Wakianalaizi kupata ubunge baada ya kumzimisha mshindani wake kwa kumtwisha rungu la kichwa, unatarajia watatarajia uongozi wa aina gani kutoka kwake? Hili lisituharibie taswira njema ya uongozi wa nchi hii.

By Jamhuri