Ndugu Rais, maandiko yanasema, nautamani mji mpya. Mji ule ambao chochote kinyonge hakitaingia. Nao utafanana na Yerusalem mpya.

Nami naitamani nchi mpya. Nchi ambayo manyang’au na wanaofifisha haki za raia hawatakuwamo. Nayo ndiyo Tanzania mpya ninayoitamani! Hakuna mwingine kwa sasa, ila ni wewe baba, wa kutufanyia nchi mpya. Nchi ambayo ndani yake Watanzania tutaishi kama watoto wa baba mmoja.

Ndugu Rais, sikuwahi kuiona Bustani ya Edeni kwa macho yangu, lakini maandiko katika vitabu vitakatifu yamewafikisha waumini wengi huko,

Paradiso! Mwanzo nchi yangu wewe Tanzania ulikuwa paradise, lakini sasa manyang’au na wakuu wa ufisadi wamekufanya ufanane na jehenam! Umekuwa mgumu kwa masikini na mzigo mzito kwa wanyonge!

Nilibahatika kutembelea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro miaka kadhaa iliyopita. Na hasa tulipoteremka kule chini, wengine wanaita shimoni, wakuja wanaita ‘crater’ ingawa Kiswahili sanifu ni “kasoka” yaani shimo la katikati ya mlima lililotokea baada ya mpasuko, niliiona Bustani ya

Edeni aliyoifanya Mwenyezi Mungu kwa waja wake wa Tanzania.

Viongozi wetu wanatumia nguvu nyingi na rasilimali lukuki katika sehemu hii ya nchi kibiashara zaidi, halali na haramu badala ya kuchimbua historia yake ambayo inaweza hata ikafanya biashara ikawa kubwa zaidi.

Ndugu Rais, wanaosema Ngorongoro ni kati ya maajabu ya dunia na wanaoiheshimu Ngorongoro kuwa ni urithi wa dunia, wanakiri kuwa sehemu hiyo ya nchi haina mfano wake mahali pengine popote duniani au tuseme ulimwenguni. Na kwa kuwa vitabu vyote vitakatifu havituambii Bustani ya Edeni ilipoteaje, tukiamini kuwa bado ingalipo ila wakutuonyesha hajatokea, kuna ubaya gani? Mpaka hapa je, hatujapata sababu ya kutafuta sababu ya kujua kwa nini Bustani ya Edeni isiwe ni sehemu hii ya dunia? Waliotuletea vitabu vitakatifu na mabingwa wa kuichambua historia ya dunia wote siyo wakwetu. Nao waliliona Bara la Afrika kama bara jeusi, Mungu asingeweza kuja huku kuwaumba Adamu na Eva.

Utu wa Mwafrika umeanza kuheshimiwa juzi tu. Leo wote hawa wamekubali kuwa binadamu wa kwanza alitokea sehemu hii ya dunia, Olduvai (Odipai) sehemu hiyo hiyo ya Ngorongoro! Walichotufanyia manyang’au na mafisadi katika nchi hii ni sawa na kile nyoka alichowafanyia Adamu na Hawa! Leo kwa jasho letu tunakula huku dada zetu na mama zetu wakijifungulia machakani.

Baadhi ya viongozi waliingia madarakani wakiwa hawana mali yoyote ya kustaajabisha. Muda mfupi tu baada ya kuwa madarakani walianza kutukuka na kujaa mali. Wao na familia zao wakaanza kuishi maisha ya peponi katikati ya Jehenam ya umasikini wa wananchi walio wengi.

Wahenga walisema mali ilivunja nguu na vilima vikalala. Tukisema wanasema tunalia ngoa. Tunapiga mbiu ganjoni tutasikiwa na nani?

Maandiko yanasema: “Nitaigeuza furaha yenu kuwa maombolezo na hapo mtanitafuta msinione. Mtaiomba milima iwafukie, haitawasikia. Chakula chenu cha anasa kitageuka moto wenu, maana mnaichimba kaburi kwa pesa zenu!” Mtu kaiibia serikali milioni saba kila dakika kwa mwezi mzima, kwa mwaka mzima, kwa miaka mitano mfululizo! Serikali iliyopita haikuwa na viongozi?

Ndugu Rais, sisemi mimi, umesema wewe baba, kuwa kila unapogusa ni jipu. Jipu lenyewe wizi. Yaani miaka mitano ya lala salama ulikuwa ni wizi mtupu. Sasa soma ukurasa wa 103 katika kitabu cha Mwalimu Mkuu wa

Watu pameandikwa: “Wananchi wanapoiona hali hii na viongozi wao wapo na wanaiona, lakini si tu hawafanyi chochote kuizuia, bali wameiridhia, unadhani wanasemaje? Lazima watasema viongozi wetu ni sehemu ya hao wezi. Ndiyo, kumbe wasemeje?”

Kiongozi lofa lazima atakuwa mwizi! Walitumia fedha za wananchi wakishinda nje, wakikusanya vya kukusanya kwa jina la wananchi, lakini wakirudi wanavifanya kuwa vyao peke yao na kuwaambia wananchi eti nchi yao ni masikini. Ubarikiwe wewe baba kwa sababu ndiye kiongozi uliyewaambia wananchi ukweli kuwa nchi yao ni tajiri sana.

Hawa hawataikwepa hukumu. Hukumu ya wananchi ni kama kiu isiyozimwa- huendelea kulisumbua koo. Watahukumiwa tu, lakini si kama ninavyotaka mimi, bali huo ndiyo ukweli wa dunia! Kweli itashinda kesho kama leo haitoshi! Hukumu ya Muumba wao itabaki imesimama juu ya vichwa vyao!

Na kama ni kweli kuwa mamlaka inatoka kwa Mungu, basi mamlaka iliyopo isipowahukumu ili wavirudishe walivyowaibia masikini wa Mungu, Mwenyezi Mungu atawahukumu walio na mamlaka sasa siku yao ya mwisho itakapofika!

Ndugu Rais, wakati nilipokuwa nayaandika haya, gazeti moja (siyo hili) liliandika habari kuwa mtuhumiwa wa milioni saba kila dakika uliyesema yuko katika mikono salama alikuwa ameitoroka nchi alipokuwa kwenye mahojiano Polisi. Habari hizi hazijakanushwa mahali popote. Ni vema ukatolewa ufafanuzi kwa maana ziliwafikia wananchi.

Sasa tuambie baba, wewe ulijisikiaje ulipopata habari kwamba muuaji aliyechinja waumini watatu katika Msikiti wa Rahman kule Mwanza amewatoroka polisi akiwa chini ya ulinzi! Anatuhumiwa kwa matukio mbalimbali ya uhalifu yakiwamo ya uporaji wa maduka ya miamala ya kifedha. Hamisi Juma ametoroka akiwa chini ya ulinzi wa polisi wakati akiwapeleka mlimani Kiloleli Nyasaka, usiku, kuonesha wenzake walikojificha.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi anakiri kuwa ni jambazi sugu wa matukio mbalimbali ya uhalifu. Alikuwa na uwezo wa kutumia silaha na kareti. Waliwezaje kutembea naye usiku bila tahadhari angalau ya kumfunga hata pingu tu? Kamanda mzima anasema katika mapigano hayo, polisi walikamata bunduki aina ya shotgun iliyotupwa na majambazi hao. Ndugu Rais, tuambie wewe; kilichotupwa kinakamatwa au kinaokotwa? Huku ni kufikiri kwa kutumia kiungo gani? Hadithi ya kutengeneza inahitaji mtu anayefikiri kwa kutumia kichwa chake!

Ndugu Rais, kwa u-polisi huu wa Kamanda Ahmed Msangi ujambazi utakwisha? Mauaji yatakoma? Na katika hili Mkuu wa Jeshi la Polisi yupo kama hayupo! Ah! Baba, tengeneza kwanza polisi yako! Tuliandika huko nyuma kuwa ni jukumu la Jeshi la Polisi kuwathibitishia wananchi kuwa wao polisi, si sehemu ya majambazi hao na wala si washirika wao!

By Jamhuri