Ndugu Rais, Tanzania kama sehemu nyingine ya Afrika tulikuwa na mambo
mengi sana ya asili ambayo tumeyatelekeza baada ya wakoloni kuja kutuamulia yapi tuyaendeleze na yapi tuyatupe kabisa.

Ni kweli sikumbuki ni lipi la asili ambalo wakoloni walituachia wakitutaka tuliendeleze. Mambo yetu mengi na hasa ya kitamaduni yalionekana ni ya kishenzi tu. Na sisi bila kudadisi ushenzi wetu ni nini tukakubali kuyatupa yote.
Nakumbuka enzi za ujana wetu, mwanakijiji alipoibiwa kuku wake hakuwa na haja ya kwenda kuripoti polisi hata kama wangekuwapo. Alichotakiwa kufanya ni kutangaza kijiji kizima kuwa kaibiwa kuku na kutoa siku tatu mwizi au hao wezi wawe wamemrudisha kuku wake. Baada siku tatu kupita bila kuku kupatikana, ulifanyika utamaduni ambao ulimfanya mwizi au wezi kujitokeza wenyewe wakiwa na matumbo makubwa yaliyovimba kiasi cha kutaka kupasuka. Hizi si hadithi za kusimuliwa, ni mambo tuliyojionea kwa macho yetu wenyewe.

Kuyasema haya leo kunahitaji uwe na moyo mpana. Kizazi cha leo haya kwao ni ushamba. Ni ushamba vipi wakati utamaduni huu ulivifanya vijiji vyetu visiwe na mtu au watu walioitwa wezi? Leo nchi imetiwa hofu na watu wasiojulikana. Siku zile, watu wasiojulikana wangejulikana kwa siku tatu tu.

Ndugu Rais, wote tulishuhudia msisimko mkubwa katika nchi yote pale mama yetu Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais alipokwenda kumjulia hali Tundu Lissu hospitalini! Hisia hizo kali zikiwa bado hazijafifia katika vifua vya wananchi, vyombo vya habari vinawapasha Watanzania kwa mara nyingine, kuwa mzee wetu Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ndugu Ali Hassan Mwinyi naye amemtembelea Ndugu Tundu Lissu hospitalini. Habari hizi kwa namna fulani zimewatia faraja wananchi wote wenye mapenzi mema! Kama ugonjwa wa Tundu Lissu ungekuwa umetokana na mambo mengine hata kama ingekuwa ni kwa ajali mbaya kama ile ya watoto wetu wa shule
ya Lucky Vincent iliyotokea Arusha, bado, hisia za Watanzania zisingevutwa pa kubwa hivi kwa viongozi wetu hawa kuamua kwenda kumjulia hali! Kinachovuta hisia kubwa ni namna ugonjwa ulivyomwingia!
Ni wazo linalotembea katika vichwa vya Watanzania wengi kuwa watu wasiojulikana walimshambulia kinyama na kwa ukatili mkubwa kwa lengo la kumuua! Wanawema ni kweli tumefikia mahali pa kutaka kuuana! Hili ndilo linaloamsha hisia kali kila linapotokea tendo kama hili kubwa kwa viongozi wetu waandamizi kumtembelea hospitalini. Ikumbukwe kwamba hawa ni viongozi wetu waandamizi. Tendo la kwenda kumjulia Lissu hali, linaonyesha jinsi walivyo na utu kwa watu wao wanaowaongoza, yaani, Watanzania wenzao.

Kila wanapofanya hivi wanatukumbusha kuwa sisi Watanzania ni wamoja! Hivi ndivyo alivyotulea Kambarage Julius Nyerere mpaka tukaonekana na mataifa mengine kuwa Watanzania ni wana wa familia moja.
Ndugu Rais, bado Watanzania wanakumbuka Taifa lilivyozizima wakati wa mazishi ya watoto wetu wa Lucky Vincent baada ya ajali iliyotokea kule Arusha! Ulikuwa msiba mzito, lakini kutokana na malezi Watanzania wote waliungana, wakawa kitu kimoja! Wako wanawema ambao hawakupata fursa ya kuhudhuria mazishi kule Arusha. Kukosekana kwa baadhi yetu katika mazishi yale ya kutisha na kusikitisha, yaliyoifanya nchi yote izizime kwa kihoro, lilikuwa ni jambo la bahati mbaya sana! Nina hakika wako wanawema wengi ambao wangependa kwenda kumjulia hali mgonjwa kule Nairobi, lakini kutokana na hali ilivyobana wanashindwa!

Ndugu Rais, hawa waliokuja kutuambia tuache ya kwetu, kule kwao waliziacha hadithi. Hadithi ambazo hakuna mahali zinamtaja Yesu Kristu Mwana wa Mungu aliye hai wala mahali zinapomtaja Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mohamad (SAW), lakini zote ziko katika vitabu vya dini zetu.

Maandiko yanasema alikuwapo mtu aliyeitwa Yona. Zamani watu hawa walijaliwa kuongea na Mwenyezi Mungu moja kwa moja. Na hata wakati mwingine walimdanganya asiyedanganyika! Tunasoma kuwa Yona alitumwa na Mungu aende Dinawi akahubiri neno ili watu wa Mungu wapone. Yona akidhani anaweza kumdanganya Mwenyezi Mungu aliamua kuuhama mji wake. Akazamia chombo (sisi tungeita meli au jahazi) ili aende mbali.

Akajificha katikati ya wasafiri naye akawa mtu asiyejulikana! Bahari ilipochafuka chombo kikaanza kusukwasukwa na kuyumba huku na kule. Manahodha wakadhani chombo kimezidiwa na mizigo. Lakini hata walipoitupa mizigo mingi baharini hali ilibaki vilevile. Ndipo wakasemezana kuwa, “Jamani, tutaangamia wote, na tupige kura tujue ni nani mwenye shida hii?” Yona kusikia hivyo wala hakungoja wamtambue
akasema mwenyewe, “Nitupeni mimi” Wakamtupa baharini hali ya amani na
usalama ikarejea katika chombo! Na hivi ndivyo itakavyokuwa kwa watu wasiojulikana.

Watu wasiojulikana wametutia Watanzania wote katika orodha ya nchi zinazofanya unyama! Lakini baba, wala usihangaike kuwatafuta hao watu wasiojulikana. Madhali nchi inawayawaya, saa ikienea, hawatangoja kutambuliwa. Watafanya kama alivyofanya Yona! Wenyewe watasema, “Tutupeni sisi!”
Ndugu Rais, watu wasiojulikana yawapasa kuelewa kuwa kama upanga ungekuwa na uwezo wa kuileta amani katika nchi, basi Uganda ya Iddi Amini Dada ingeongoza kuwa nchi ya amani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki na ya Kati. Na Zaire ya Mobutu ingekuwa nchi ya kuigwa kwa namna ambavyo amani ingekuwa imetamalaki katika nchi hiyo. Na tuzitumie fikra zetu japo kwa muda kidogo tusimame na kuitazama Afrika Kusini ya Nelson Mandela. Tuitazame Zambia ya Kenneth Kaunda, Msumbiji ya Samora Michael na hata Kenya ya Jomo Kenyatta. Baba tulikuwa wakubwa, ni lini tulisikia tishio la upanga katika nchi hizo?

Kumbukumbu zetu zimeenda wapi! Tumeshindwa kuhifadhi kumbukumbu zetu
hata tusiikumbuke Tanganyika na baadaye Tanzania ya Julius Nyerere? Upanga lilikuwa ni neno la Kiswahili tu lililopatikana katika kamusi ya Kiswahili. Leo neno upanga limeondoa amani katika mioyo ya watu wetu! Wanawema, tunachogombania hasa ni kipi? Tutaziendeleza hizi tofauti zetu mpaka lini? Na haya yote tunayafanya kwa faida ya nani? Maandiko yanasema, atumiaye upanga atakufa kwa upanga!

937 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!