Home Makala UWT ‘Ilivyomkuna’ JPM Wakati UVCCM Ikimsononesha

UWT ‘Ilivyomkuna’ JPM Wakati UVCCM Ikimsononesha

by Jamhuri

Mikutano ya uchaguzi kwa jumuiya mbili za Chama Cha Mapinduzi (CCM) imefanyika mkoani Dodoma wiki iliyopita, yote ikihutubiwa na Mwenyekiti wake, Rais John Magufuli.

Jumuiya ya Wanawake (UWT) ikafanya mkutano wa uchaguzi uliomchagua Gaudencia Kabaka kuwa Mwenyekiti, wakati Kheri James akichaguliwa kuiongoza Jumuiya ya Vijana (UV-CCM).    

Hata hivyo, mkutano wa UWT ndiyo uliodhihirika kumfurahisha zaidi Rais Magufuli, ambaye hakuficha hisia kwa namna anavyotambua utendaji kazi bora na uadilifu wa viongozi wanawake.

Lakini hali ikawa tofauti katika mkutano wa UV-CCM ambao hata Rais Magufuli alipokuwa akihutubia, Mwenyekiti wa jumuiya hiyo aliyekuwa akimaliza muda wake, Sadifa Juma Khamis, akakamatwa kwa tuhuma za rushwa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Sadifa, ambaye pia ni Mbunge wa Donge, akatuhumiwa kuwanunulia wajumbe soda na kuahidi kuwalipia nauli.

Kwenye mkutano wa UWT, Rais Magufuli akaelezea kuridhishwa na utendaji kazi, uwajibikaji na uaminifu wa wanawake viongozi wakiwamo aliowateua kushika nyadhifa tofauti.

Akasema hali kama imejidhihirisha upande wa Zanzibar, akinukuu mawasiliano yake na Rais Visiwa hivyo, Dk Ali Mohamed Shein.

Hata wanawake walioteuliwa kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), nimeelezwa na Rais Shein kwamba wanatumia nyadhifa walizonazo kutumikia vizuri umma; hawajawaangusha,” amesema.

Rais Magufuli akaongeza, “Ninawaahidi kila nafasi itakayotokea, nitawapa kipaumbele wanawake, kwa sababu nimejiridhisha nyie waaminifu, mna upendo wa kweli, mnachapa kazi na hamuendekezi vitendo vya rushwa.”

UV-CCM WAMFEDHEHESHA

Wakati hali ikiwa hivyo upande wa UWT, Mkutano Mkuu wa Tisa wa UV-CCM) umefanyika kwa fedheha.

Badala ya kuuongoza mkutano huo, akawa mikononi mwa Takukuru. Taarifa za kukamatwa kwake zikathibitishwa na Kamanda wa Takukuru mkoani Dodoma, Emma Kuhanga.

TUHUMA ZA RUSHWA

Tuhuma za rushwa miongoni mwa wana-UVCCM zikaibuliwa kwenye mkutano huo, mbele Rais Magufuli. Pia walikuwapo Rais wa Zanzibar, Dk Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif  Ally Idi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na Katibu Mwenezi wa chama hicho, Hamphrey Polepole.

Aliyeibua hoja hiyo ni Wakili wa kujitegemea aliyejiunga CCM akitokea ACT-Wazalendo, Albert Msando, aliyejitambulisha kuwa msemakweli asiyetaka kuwasifia (vijana), bali kuwajulisha ukweli utaowauma baadhi yao.

Akawakosoa vijana kwa kutoa taarifa ya idadi ya wanachama kwa Rais Magufuli isiyo ya kweli, huku akisisitiza kwamba kubadilika na kujielekeza katika tafiti zinazofanikisha kupatikana kwa taarifa sahihi.

Mnajiita moyo na mkono wa kuume wa chama (CCM), lazima mfahamu sifa hiyo ina wajibu, mnao wajibu wa kukomesha rushwa na vitendo vya kifisadi; ni aibu, fedheha na kumdhalilisha Rais Magufuli ikiwa mnashiriki vitendo vya rushwa na ufisadi,’’ akasema.

Akaongeza, “Wala sichelei kusema baadhi ya wajumbe mmepokea rushwa na baadhi wagombea mmetoa rushwa.”

JPM APIGILIA MSUMARI

Akifungua Mkutano wa UVCCM, Rais Magufuli hakutaka kuingia kwa kina kuzungumzia sakata la kukamatwa wa Sadifa, lakini akasema wapo viongozi ambao unapofika uchaguzi wa jumuiya hiyo, wanapigana vikumbo kupandikiza watu wao kwa kutumia rushwa.

Rais Magufuli, amesema ana ‘majeraha’ yaliyosababishwa na UV-CCM kuwa na viongozi wa aina hiyo.

Sikuwahi kupewa orodha ya majina ya vijana wenye sifa za kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali, nawaasa mbadilike kwa kuchagua viongozi waadilifu, vinginevyo hata miaka mitano iliyosalia mtaendelea kusota,” akasema.

Amesema vijana walioteuliwa naye wamepatikana kwa jitihada zake binafsi, kwamba hiyo ni moja ya hasara za watu kukosa umakini wakati wa kuchagua viongozi.

Kuhusu rushwa ndani ya uchaguzi wa jumuiya za chama hususani UV-CCM, akasema kumekuwa na taarifa kwenye mitandao ya kijamii zikimtaja mmoja wa watoto wa mmoja wa Rais wastaafu, kwamba amekuwa akifanya vikao kwenye baa moja maarufu mjini Dodoma.

Akasema lengo la vikao hivyo ikawa ni kuratibu vitendo vya rushwa ili mgombea wanayemtaka apate nafasi ya uenyekiti wa UV-CCM.

Hata Bodi ya Wadhamini haisaidii chochote, nayo iondoke ingawa ninafahamu yumo na William Lukuvi (Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi),’’ akasema.

You may also like